Papa Francisko: Mkazo Katika Malezi, Makuzi na Majiundo ya Kipadre: Kristo Yesu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri lilichapisha Mwongozo wa Malezi ya Kipadre unaojulikana kama “Ratio Fundamentalis Institutionis Sacerdotalis” unabainisha changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mchakato wa kulinda, kukuza na kudumisha wito na maisha ya Daraja Takatifu ya Upadre. Huu ni wito wenye thamani kubwa katika maisha na utume wa Kanisa unaopaswa kuhudumiwa kwa umakini mkubwa kwa kuheshimu dhamiri nyofu, wajibu unaotekelezwa kwa unyenyekevu na uvumilivu mkubwa, ili kweli Wakleri waweze kung’ara kati ya watu wa Mungu wanaowahudumia! Mwongozo unatoa kwa muhtasari wa sheria, kanuni na mambo msingi ambayo yanapaswa kuzingatiwa kwa ajili ya malezi na makuzi ya wito wa Daraja Takatifu ya Upadre. Unabainisha wajibu wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki; Waratibu wa Seminari kitaifa na kimataifa pamoja na mwongozo wa malezi ya Seminari moja moja. Mwongozo huu unapembua kwa kina na mapana kanuni msingi za maisha na wito wa Daraja Takatifu ya Upadre: Yaani wanapaswa kuunganika na Kristo ili kuwaongoza, kuwachunga na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wanapaswa kuungana na Kristo Yesu katika maisha, upendo na ukweli kwa ajili ya wokovu wa watu na kuendelea kuwa ni mwanga wa mataifa na chumvi ya dunia.
Dhamana ya Kanisa ni kulea, kusindikiza na kupalilia miito mitakatifu, lakini kwa namna ya pekee wito wa Daraja Takatifu. Seminari ndogo na nyumba za malezi ni mahali pa kulea na kuwasindikiza vijana katika maisha na wito wa Daraja Takatifu ya Upadre. Hapa waseminari wadogo wanapaswa kupewa malezi ya tunu msingi za maisha ya Kikristo kwa kukazia majiundo ya kiakili, kiroho, kiutu na kimaadili. Ni mahali pa kukuza ukomavu, umoja na mshikamano na Kristo Yesu kwa njia ya Sala, Neno la Mungu na Mashauri ya Kiinjili. Walezi wawe kweli ni mashuhuda wa Injili ya Kristo! Mwongozo pia unaangalia wito kwa Daraja takatifu wa watu wenye umri mkubwa, wasaidiwe na kupatiwa malezi makini katika nyumba maalum, ili waweze hatimaye, kufanya maamuzi muhimu katika maisha yao! Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 28 Novemba 2022 amekutana na kuzungumza na Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Pio cha Amerika ya Kusini. Katika hotuba yake, amefafanua umuhimu wa nafasi waliyopewa na Kanisa katika majiundo yao, Wito wa Mtakatifu Andrea Mtume na mwaliko wa kuwa ni Wamisionari Mitume.
Majandokasisi wanapaswa kutambua kwamba, wamepewa fursa na Mama Kanisa neema na baraka ya kukuza na kudumisha malezi na makuzi yao: kiakili na kitaaluma; wanayo fursa ya kuona utajiri wa umoja na utofauti unaofumbatwa katika Kanisa la Kiulimwengu, ni fursa ya kujifunza yote haya, ili hatimaye, watakaporudi Amerika ya Kusini, wawe tayari kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, daima wakijitahidi kuzungumza lugha ya upendo, hadi miisho ya dunia. Hii ndiyo dhamana na utume uliotekelezwa na Mtakatifu Andrea, Mtume, ambaye Mama Kanisa anamwadhimisha kila mwaka ifikapo tarehe 30 Novemba. Andrea na nduguye Simoni Petro, baada ya kumwona Mwanakondoo, akawakaribisha akisema, “Njoni nanyi mtaona”, wakaenda wakaona mahali alipokuwa anaishi wakakaa naye siku ile. Tangu siku ile maisha yao yakabadilika kabisa, changamoto na mwaliko kwa waamini kujitahidi kupyaisha makutano yao na Kristo Yesu, kwa kushiriki Neno lake; Katika Sala ya Kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na Sakramenti zake. Wajitahidi kuunganika kabisa na Kristo Yesu katika maisha na utume wao na kamwe wasiwe ni kikwazo kwa Kristo Yesu katika kutenda ndani mwao. Waendelee kujifunza kutoka kwa Kristo Yesu, ili waweze kuwa ni wanafunzi wake, tayari kutumwa na hii ndiyo maana ya kuwa ni wanafunzi wa Kristo Yesu.
Mtume Andrea kwa kukutana na Kristo Yesu, maisha yake yakabadilika sana na hivyo kumshirikisha ndugu yake, Simon Petro na huo ukawa ni mwanzo wa safari ya kimisionari ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu. Jambo la msingi ni kukaa pamoja na Kristo Yesu, ili kuchota neema na faraja tayari kutumwa kumtangaza na kushikamana na wagonjwa, maskini, wakimbizi na wahamiaji bila kuwasahau wale wanaotupwa na kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Haya ni maisha ya kutangaza na kushuhudia upendo usiokuwa na masharti kwa maskini, wahamiaji na wakimbizi; wagonjwa, wafungwa na wote hawa ndio utambulisho wa Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anawashauri waamini kujenga utamaduni wa kurejea na kujichotea nguvu kutoka kwa Kristo Yesu baada ya mahangaiko ya siku nzima kwa kuwa daima analo neno la kuwaambia waja wake katika hali ya ukimya na utulivu wa ndani. Bikira Maria wa Guadalupe, awasaidie kutambua umuhimu wa kuwa ni wanafunzi mitume na awasindikize katika safari ya kwenda na kurejea tena kwa Kristo Yesu, ili waweze kumlaki kwa fuaraha. Mtakatifu Andrea Mtume awakumbuke na kuwaombea katika hija ya malezi na hatimaye maisha na utume wao wa Kipadre.