Tafuta

Kipindi cha Majilio tarehe 27 Novemba na kitafikia kilele chake Jumamosi tarehe 24 Desemba 2022. Kipindi cha Majilio tarehe 27 Novemba na kitafikia kilele chake Jumamosi tarehe 24 Desemba 2022.  

Papa Francisko: Majilio Ni Kipindi cha Toba na Wongofu wa Ndani

Majilio ni kipindi cha kungoja ujio wa Kristo Yesu kwa: Imani, matumaini, mapendo, amani, toba na wongofu. Majilio ni dira, mwongozo, malezi na majiundo ya maisha ya kiroho kama sehemu ya maandalizi ya ujio wa Yesu katika maisha ya waamini kwa njia ya: Neno, Sakramenti, Matendo ya huruma: katika historia ya maisha na jirani wanaokutana nao katika safari ya maisha ya kila siku.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa ameuanza mwaka mpya wa Kanisa kwa kuadhimisha Dominika ya kwanza ya Kipindi cha Majilio tarehe 27 Novemba na kitafikia kilele chake Jumamosi tarehe 24 Desemba 2022. Majilio ni kipindi cha kungoja ujio wa Kristo Yesu kwa: Imani, matumaini, mapendo, amani, toba na wongofu wa ndani. Majilio ni dira, mwongozo, malezi na majiundo ya maisha ya kiroho kama sehemu ya maandalizi ya ujio wa Kristo Yesu katika maisha ya waamini kwa njia ya: Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa, Matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika historia ya maisha na jirani wanaokutana nao katika hija ya maisha yako ya kila siku. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Mzunguko wa Katekesi Kuhusu Utambuzi, 30 Novemba 2022, amewaalika waamini kutumia Kipindi cha Majilio ili kutakasa nyoyo zao kwa toba na wongofu wa ndani, ili kuweza kumpokea Kristo Yesu anayezaliwa tena nyoyoni mwao kwa moyo safi. Majilio ni Kipindi ch kuomba msamaha na maondoleo ya dhambi, ili kuanza kutembea tena katika njia nyofu inayomwezesha mwamini kusimamia haki. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, awakirimie waja wake moyo wa unyenyekevu na ulio wazi tayari kupokea neema na baraka katika maisha kwa ajili ya sifa na utukufu na mapendo kwa Mungu na jirani.

Majilio ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani
Majilio ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuwasha taa ya imani na hivyo kumwachia nafasi Kristo Yesu ili aendelee kuwaangazia mwanga wa matumaini katika mapito ya maisha yao. Kwa mwanga huu, waamini waweze kupita na hatimaye kushinda vikwazo vyote dhidi ya fadhila za Kimungu, ili hatimaye, waweze kufikia kilele cha furaha ya kweli katika maisha. Kumbe, waamini wanapaswa kujiandaa kikamilifu kumwendea ili kukutana na Kristo Yesu anayekuja katika maisha yao kwa kuzama katika maisha ya sala, toba na wongofu wa ndani pamoja na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Waamini wajenge utamaduni wa kusikiliza, kusoma, kutafakari Neno la Mungu na kulimwilisha katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Hii ni kwa sababu Neno la Mungu ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo. Majilio ni Kipindi cha faraja ya kweli, mwaliko kwa waamini kumwomba Kristo Yesu Mfalme wa amani awe ni faraja ya kweli kwa wale wote wanaoteseka kutokana na vita, mipasuko na misigano ya kijamii, ili amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yaweze kushika mkondo wake katika akili na nyoyo za za watu.

Majilio 2022

 

 

 

 

 

30 November 2022, 15:08