Papa:Kazi ya kuwasiliana ni pamoja na kutoa sauti kwa wasio nayo!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amekutana mjini Vatican Jumamosi tarehe 12 Novemba 2022 na wafanyakazi na washiriki wa Mkutano Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano, ambapo hotuba yake ameikabidhi na kuzungumza bila kusoma. Katika hotuba aliyokabidhi, Baba Mtakatifu Francisko awali ya yote anamshukuru Dk. Paulo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano kwa maneno yake na kuwasalimia wote na wale ambao wameshiriki Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ulioongozwa mada Sinodi na Mawasiliano. Mchakato wa njia ya kuendelezwa. Baba Mtakatifu Francisko amebainisha kwamba Sinodi sio zoezi rahisi la mawasiliano na wala namna ya kutafuta kufikiria Kanisa kwa mantiki ya walio wengi na walio wachache ambao wanatakiwa kutafuta makubaliano. Aina hiyo ya mgawanyiko ni ya kidunia, na inafuata mitindo ya uzoefu mwingi wa kijamii, kiutamaduni na kisiasa. Kinyume chake umuhimu wa mchakato wa kisonodi unajikita katika ukweli msingi ambao hatupaswi kamwe kupoteza katika mtazamo wetu, kwani huo una lengo la kusikiliza, kuelewa na kujiweka katika matendo ya mapenzi ya Mungu.
Baba Mtakatifu Francisko amebainisha kwamba ikiwa kama Kanisa, tunataka kujua mapenzi ya Mungu ili kuifanya nuru ya Injili iendelee kuwapo katika wakati wetu, hivyo basi ni lazima turudi kuwa na ufahamu kwamba kamwe haitolewi kwa mtu binafsi, bali daima kwa Kanisa katika ukamilifu wake. Ni katika maisha ya mahusiano yetu ya kikanisa tu ndipo tunakuwa na uwezo wa kumsikiliza na kumwelewa Bwana anayezungumza nasi. Bila "kutembea pamoja", tunaweza tu kuwa taasisi ya kidini, ambayo hata hivyo imepoteza uwezo wa kuruhusu mwanga wa ujumbe wa Mwalimu wake kuangaza, na imepoteza uwezo wa kuleta ladha kwa matukio mbalimbali ya ulimwengu. Yesu anatuonya juu ya mchepuko kama huo. Yeye anarudia tena kusema kwetu kwamba Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imepoteza ladha yake, itakolezwa na nini? Haifai kitu ila kutupwa na kukanyagwa na watu. Ninyi ni nuru ya ulimwengu; mji ulio juu ya mlima hauwezi kufichwa, wala taa haiwezi kuwashwa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya taa hiyo, iwaangazie wote waliomo nyumbani (Mt 5:13-16). Hii ndiyo sababu mwelekeo wa sinodi ni mwelekeo wa Kanisa na tafakari ambalo limetufanya tuwe na shughuli nyingi katika miaka ya hivi karibuni lina lengo la kuleta kwa nguvu kile ambacho Kanisa limekuwa likiamini kwa ukamilifu, Baba Mtakatifu anabainisha.
Biblia imejaa historia nyingi za wanaume na wanawake ambao kwa nyakati fulani tunawaona na kuwafikiria kuwa mashujaa wa pekee. Kwa mfano, Ibrahamu, wa kwanza ambaye Mungu alizungumza naye neno lake, si mtu mpweke anayeanza safari, lakini ni mtu anayechukua sauti ya Mungu kwa uzito, aliyemwalika aondoke katika nchi yake, na kufanya hivyo pamoja na familia yake. [Mwanzo 12:1-9). Historia ya Ibrahim ni historia ya mafungamano ya Ibrahim. Hata Musa, mkombozi wa Israeli, asingeweza kutimiza kazi yake isipokuwa kwa msaada wa kaka yake Harun, dada yake Maria, baba mkwe wake Yethro, na kundi la wanaume na wanawake wengine waliomsaidia kusikiliza neno la Bwana na kulitenda kwa wema wa wote. Yeye ni mtu aliyejeruhiwa katika historia yake ya kibinafsi, na hakuwa na ujuzi wa kuzungumza, kinyume chake, yeye alikuwa na kigugumizi. Tunaweza karibu kusema kwamba yeye alikuwa ni mtu ambaye ana shida kwa usahihi katika kuwasiliana, lakini pia aliyekuwa karibu naye alitengeneza kutoweza kwake mwenyewe (rej. Kut 4:10.12-16).
Maria wa Nazareti hasingeweza kuimba wimbo wa [Magnificat] yaani sifa kwa bwana bila uwepo na urafiki wa binamu yake Elisabeti (rej. Lk 1: 46-55), na hasingeweza kumlinda mtoto Yesu kutokana na chuki ya wale waliotaka kumuua kama hasingekuwapo Yosefu karibu naye (Mt 2:13-15.19-23). Yesu mwenyewe analikuwa na uhitaji wa vifungo, na ilipobidi akabiliane na vita vya maana vya utume wake huko Yerusalemu, usiku wa kukamatwa kwake alikuwa na rafiki zake Petro, Yakobo na Yohana pamoja naye kwenye bustani ya Gethsemane (rej. Mt 26) : 36-46). Mchango wa mawasiliano hasa ni ule wa kuwezesha mwelekeo huu wa jumuiya, uwezo huu wa uhusiano, wito huu wa vifungo vya uhusiano. Na kwa hivyo tunaelewa jinsi ilivyo kazi ya mawasiliano ya kukuza ukaribu, kutoa sauti kwa wale ambao wametengwa, kuvutia umakini kwa kile ambacho kwa kawaida tunatupa na kudharau. Mawasiliano ni kusema, ufundi wa mahusiano ambayo ndani yake sauti ya Mungu inasikika na kujifanya isikike.
Mambo matatu Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba hiyo amependa kusisitiza zaidi kama kuelekeza uwezekano wa njia kwa ajili ya wakati wa baadaye wa mchakato wa kutafakari katika muktadha huo. Kazi ya kwanza ya mawasiliano inapaswa kuwa kufanya watu wasiwe wapweke. Ikiwa haipunguzi hisia ya upweke ambayo wanaume na wanawake wengi wanahisi kulaaniwa, basi mawasiliano hayo ni burudani tu, na sio ufundi wa vifungo vya mahusiano kama tulivyosema hapo awali. Ili kutekeleza utume huo ni muhimu kuwa wazi kwamba mtu hasihisi kuwa peke yake anapogundua kuwa maswali, matumaini, shida anazobeba ndani zinajidhihirisha nje. Ni Kanisa pekee ambalo limezama katika uhalisia linajua kile kilicho ndani ya moyo wa mwanadamu wa sasa. Kwa hivyo, kila mawasiliano ya kweli hufanywa juu ya usikilizaji kamili, unajumuisha kukutana, nyuso, na historia. Ikiwa hatujui jinsi ya kukaa katika hali halisi, tutajiwekea kikomo tu kwa kuelekeza ambayo hakuna mtu atakayesikiliza. Mawasiliano yanapaswa kuwa msaada mkubwa kwa Kanisa, kuishi kwa uthabiti katika uhalisia, kupendelea kusikiliza na kupitia maswali makuu ya wanaume na wanawake wa leo. Kuhusiana na changamoto hiyo ya kwanza, Papa amependa kuongeza nyingine ile ya kutoa sauti kwa wale ambao hawana sauti.
Baba Mtakatkfu Francisko amebanisha kwamba mara nyingi sana tunaona mifumo ya mawasiliano ambayo inaweka pembeni na kuhakiki kile ambacho kinatusumbua na ambacho hatutaki kuona. Kanisa, shukrani kwa Roho Mtakatifu, linajua vyema kwamba ni wajibu wake kuwa na mambo madogo zaidi,na makazi yake ya asili ni yale ya pembezoni zinazokuwepo. Lakini vipengee vya maisha vilivyopo sio tu wale ambao kwa sababu za kiuchumi wanajikuta kwenye ukingo wa jamii, lakini pia wale ambao wamejaza mkate lakini hawana maana, pia ni wale wanaoishi katika hali ya kutengwa kwa sababu ya chaguzi fulani, au kushindwa kwa familia au kwa matukio ya kibinafsi ambayo yameweka alama bila kufutika katika historia yao. Yesu hakumwogopa kamwe mwenye ukoma, maskini, mgeni, hata kama watu hawa walikuwa wametiwa alama na unyanyapaa wa kimaadili. Yesu hakuwahi kuwapuuza watu wasio wa kawaida wa aina yoyote. Baba Mtakatifu anajiuliza ikiwa kama Kanisa yaani sisi pia tunajua jinsi ya kutoa sauti kwa ajili ya hawa kaka na dada, ikiwa tunajua jinsi ya kuwasikiliza, ikiwa tunajua jinsi ya kutambua mapenzi ya Mungu pamoja nao, na hivyo kuzungumza nao Neno ambalo linaokoa.
Mwisho,changamoto ya tatu ya mawasiliano ambayo Baba Mtakatifu amependa kubainisha ni ile ya kuelimisha katika juhudi za ugumu wa kuwasiliana. Sio mara chache katika Injili pia kuna kutoelewana, ucheleweshaji wa kuelewa maneno ya Yesu, au kutoelewana ambako nyakati fulani huwa misiba halisi, kama ilivyotokea kwa Yuda Iskariote, ambaye analichanganya utume wa Kristo na umasiya wa kisiasa. Kwa maana hiyo, tunapaswa pia kukubali mwelekeo huu wa ugumu katika mawasiliano. Mara nyingi sana wale wanaolitazama Kanisa kutokea nje wanatatanishwa na mivutano tofauti iliyopo ndani yake. Lakini yeyote anayejua jinsi Roho Mtakatifu anavyofanya kazi anajua vizuri kwamba anapenda kuunda umoja kati ya tofauti, na kuunda maelewano kutoka katika mikanganyiko. Umoja kamwe sio usawa, lakini ni uwezo wa kuweka pamoja ukweli wa tofauti sana. Kwa maana hiyo Papa amefikiria kwamba tunapaswa pia kuwasiliana na ugumu huo, bila kujifanya kutatua au kuuficha.
Upinzani si lazima uwe mtazamo wa mpasuko, lakini unaweza kuwa mojawapo ya viungo vya umoja. Mawasiliano lazima pia yafanye utofauti wa mitazamo kwa kufanya iwezekane, huku kila mara kwa kujaribu kuhifadhi umoja na ukweli, na kupiga vita kashfa, vurugu za maneno, kujithibitisha na itikadi kali ambazo kwa kisingizio cha kuwa mwaminifu kiukweli, ulieneza migawanyiko tu na mifarakano. Ikiwa inajitokeza kwa uharibifu huo, mawasiliano, badala ya kufanya mengi kuwa mazuri, huishia kufanya madhara mengi. Kwa maana hiyo Baba Mtakatifu Francisko amebainisha kwamba, kazi ya Baraza la Kipapa la mawasiliano si ya kiufundi tu. Wito wake, kama alivyoeleza, unagusa kwa namna sawa ya kuwa Kanisa. Ametoa shukrani kwa kile wanachokifanya na hivyo kuwahimiza waendelee mbele kwa njia ya uamuzi na ya kinabii. Kutumikia Kanisa kunamaanisha kuwa wa kuaminika na pia ujasiri katika njia mpya za kuthubutu. Kwa maana hiyo, daima kuwa wa kuaminika na mwenye ujasiri. Anawabariki wote kutoka moyoni mwake. Na tafadhali wasisahau kumweombea.