Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu 27 Novemba 2022 amekutana na washiriki wa mkutano wa shule nchini Italia zinazounda Mtandao wa Elimu ya Amani Kitaifa, Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu 27 Novemba 2022 amekutana na washiriki wa mkutano wa shule nchini Italia zinazounda Mtandao wa Elimu ya Amani Kitaifa,  

Papa Francisko: Elimu, Amani na Utunzaji wa Mazingira Nyumba ya Wote

Papa anakazia kuhusu: Janga na maana ya elimu, umuhimu wa kupyaisha mfumo wa elimu na hatimaye, mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika maboresho ya mfumo wa elimu Kimataifa. Hii ni pamoja na kuragibisha utunzaji bora wa mazingira; haki na amani; mafao ya wengi, ukarimu kwa wageni pamoja na ujenzi wa udugu wa kibinadamu, changamoto kwa wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Yohane XXIII katika Waraka wake wa Kitume “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” uliochapishwa tarehe 11 Aprili 1963, mwaka 2023, Kanisa litaadhimisha kumbukizi ya Miaka 60 tangu kuchapishwa kwake. Mtakatifu Yohane XXIII anasema, amani inasimikwa katika misingi ya ukweli, haki, upendo na uhuru kamili. Kila mwanadamu ni nafsi yenye haki na wajibu. Hii ni haki ya kuishi na kuwa na maisha na haki za tunu za kimaadili na kiutamaduni. Kutokana na haki ya asili, watu wote wana haki ya kushiriki ukuaji wa ustaarabu; na kwa hiyo ni lazima kila mtu aweze kupata elimu nzuri ya msingi, na mafunzo ya ufundi na ya elimu ya juu yanayolingana na kiwango cha maendeleo ya elimu cha nchi yake. Ni lazima kila bidii na juhudi zifanywe ili kila mtu aweze kufikia viwango vya juu vya elimu, kadiri iwezekanavyo kulingana na karama zake, na kuchukua dhima na majukumu katika jamii zinazolingana na karama hizo za maumbile na ujuzi alioupata. Kuna haki ya kumwabudu Mungu kulingana na maongozi ya dhamiri nyofu. “Tumezaliwa kwa ajili ya kumpa Mungu aliyetuumba heshima inayompasa, iliyo ya haki, na kumtambua na kumfuata yeye peke yake. Nasi tumefungamana na kushikamana na Mungu kwa njia ya kifungo hicho cha utauwa, ambacho hata jina la dini yenyewe linatokana nacho” na hiki ni kielelezo cha ukweli.

Muhimu: Elimu bora, amani na utunzaji bora wa mazingira
Muhimu: Elimu bora, amani na utunzaji bora wa mazingira

Haki ya mtu kuchagua hali ya kuishi anayoipenda zaidi. Haki ya kuwatunza na kuwalea watoto kwanza kabisa ni juu ya wazazi wao. Haki zinazohusu uchumi lazima ziungane na haki ya kufanya kazi katika hali na mazingira visivyoathiri uzima wa mwili au maadili ya mtu, wala visivyodhuru mchakato wa kukua kwa vijana hadi wafikie ukomavu wa utu. Na kuhusu wanawake, lazima waweze kufanya kazi kwa namna inayopatana na haja na wajibu vinavyotokana na hali yao ya wake na mama. Kutokana na hadhi yake, mtu ana pia haki ya kujishughulisha na utendaji wa uchumi kulingana na kiwango chake cha uwajibikaji. Inabidi kusisitiza haki ya mfanyakazi ya kupata ujira unaolingana na vigezo vya haki, ambao kwao, kadiri iwezekanavyo kutokana na uwezo wa kifedha wa nchi, mfanyakazi pamoja na familia yake aweze kuwa na kiwango cha maisha unaopatana na hadhi ya kibinadamu. Wanadamu wana tabia ya kijamii, ndiyo sababu wana haki ya kukusanyika pamoja na kuunda vyama. Wana pia haki ya kuvipa vyama hivyo mifumo inayofikiriwa kufaa zaidi kutimiza malengo yake, na ya kutenda ndani ya vyama hivyo kwa uhuru na kadiri ya uwajibikaji wao ili kuyafikia malengo hayo. Kuna uhusiano usiovunjika baina ya haki na wajibu wa kila mtu. Haki ya kuwa na maisha mazuri inahusisha wajibu wa kuishi kwa kujiheshimu; haki ya kuwa huru katika kutafuta ukweli, inaendana na wajibu wa kufanya juhudi katika kutafuta kwa upana na kina huo ukweli.

Mtakatifu Yohane XXIII Pacem in terris 60 years mwaka 2023
Mtakatifu Yohane XXIII Pacem in terris 60 years mwaka 2023

Kuwiana haki na wajibu kati ya watu mbalimbali. Katika kushirikiana na moyo wa uwajibikaji: hakuna ubinadamu katika jamii ambayo imeunganishwa pamoja kwa kulazimishwa. Maana hali hiyo, mbali na kuhamasisha, kama ilivyo ada, maendeleo na ukamilifu wa mtu, inakuwa kikwazo kwa uhuru wake.Ni muhimu watu kuishi jamii katika ukweli, haki, upendo na uhuru. Utaratibu wa kimaadili wenye kama msingi halisi Mungu wa kweli. Kimsingi amani inasimikwa katika misingi ya ukweli, haki, upendo na uhuru kamili. Kwa upande mwingine, Mtakatifu Francisko wa Assisi alijikita zaidi katika mambo makuu matatu: Amani, Mazingira na Upendeleo kwa maskini. Kumbe, vijana wa kizazi kipya hawana budi kufundwa katika misingi itakayowawezesha kuwa ni vyombo na mashuhuda wa amani sehemu mbali mbali za dunia. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu 27 Novemba 2022 amekutana na washiriki wa mkutano wa shule nchini Italia zinazounda Mtandao wa Elimu ya Amani Kitaifa, mradi ambao utafikia kilele chake Mwezi Mei 2023, kwa wanafunzi kufanya upembuzi yakinifu ili kupima mafanikio na hatimaye, kutoa mapendekezo yanayopaswa kufanyiwa kazi na Jumuiya ya Kimataifa. Mji wa Assisi ni maarufu sana katika mchakato wa kuragibisha amani duniani kwa kuiga mfano wa Mtakatifu Francisko wa Assisi aliyejitenga na familia pamoja na utajiri mkubwa aliokua nao akaamua kuambata Ufukara wa Kiinjili. Mtakatifu Francisko wa Assisi leo hii mfano bora wa kuigwa katika kukuza na kudumisha: Amani, udugu wa kibinadamu, upendo kwa ajili ya mskini, ikolojia pamoja na uchumi fungamani.

Mtakatifu Francisko wa Asisi: Elimu, Mazingira na Amani
Mtakatifu Francisko wa Asisi: Elimu, Mazingira na Amani

Mtakatifu Francisko wa Assisi ana mvuto kwa watu wengi, kiasi hata cha Papa mwenyewe kuamua kumchagua kuwa ni mlinzi na mwombezi wake kwa kujikita katika; Amani, Maskini na Mazingira. Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education” ulitiwa mkwaju hapo tarehe 15 Oktoba 2020. Baba Mtakatifu Francisko anakazia kuhusu: Janga la elimu duniani, maana ya elimu, umuhimu wa kupyaisha mfumo wa elimu na hatimaye, mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika maboresho ya mfumo wa elimu Kimataifa. Hii ni pamoja na kuragibisha utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; haki na amani; mafao ya wengi, ukarimu kwa wageni, wakimbizi na wahamiaji pamoja na ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Hii ni changamoto ambayo imeanza kuvaliwa njuga na viongozi wa kidini, shule, taasisi za elimu ya juu pamoja na vyuo vikuu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, amani ya kweli inafumbatwa katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na kwamba, amani inapaswa kulindwa na kudumishwa na wote daima. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordia et misera” yaani “Huruma na amani” anasema, huruma ni kielelezo makini cha upendo wa Mungu unaosamehe, unaoongoa, unaopyaisha na kubadili mwelekeo wa maisha. Ni kielelezo cha ufunuo wa Fumbo la Mungu ambalo ni huruma ya milele, inayowakumbatia na kuwaambata wote pasi na ubaguzi, kiasi cha kuwakirimia maisha mapya, chemchemi ya furaha na matumaini mapya, yanayovunjilia mbali ubaguzi, ubinafsi na uchoyo ili kutenda wema, kufikiri vyema na kuondoa huzuni moyoni.

Someni tena Waraka wa Yohane XXIII: Amani Duniani
Someni tena Waraka wa Yohane XXIII: Amani Duniani

Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona alimhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza. Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu, na cho chote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa. Waonaje wewe, katika hao watatu, ni yupi aliyekuwa jirani yake yule aliyeangukia kati ya wanyang’anyi? Akasema, Ni huyo aliyemwonea huruma. Yesu akamwambia, Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo.” Lk 10: 25-37. Baba Mtakatifu anasema, leo hii kuna mashuhuda wa amani pamoja na taasisi mbalimbali zinazotekeleza dhamana na wajibu wake katika hali ya ukimya pasi na makuu. Mtakatifu Yohane XXIII, Papa Mwema na Baba wa Amani Duniani alichapisha Waraka wake wa Kitume “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” tarehe 11 Aprili 1963, wakati ambapo kulikuwa na kipeo cha Vita Baridi, Ujenzi wa Ukuta wa Berlin, Machafuko ya Kisiasa nchini Cuba pamoja na tishio la mashambulizi ya silaha za kinyuklia. Mtakatifu Yohane XXIII akawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika mchakato wa majadiliano kama suluhu ya kupambana na tishio la vita, mwaliko huu, ukapokelewa kwa mikono miwili. Leo hii vijana wa kizazi kipya wanaitwa na kuhamasishwa kuusoma waraka huu, ili kufuata njia hii kwa ajili kulinda na kudumisha amani duniani.

Muhimu: Amani. Elimu na Mazigira bora
Muhimu: Amani. Elimu na Mazigira bora

Baba Mtakatifu Franciko amemkumbuka Martin Luther King aliyetunukiwa Nishani ya Amani Kwa Mwaka 1964, alionesha kwamba, alikuwa na ndoto ya amani ambayo ingeweza kufutilia mbali mifumo mbalimbali ya ubaguzi, kwa kujikita katika: haki, uhuru wa kweli na usawa. Baba Mtakatifu anawaalika vijana wa kizazi kipya kuwa na ndoto na kuwataka kushiriki katika hija kubwa ya vijana wa Mataifa yote itakayofikia kilele chake katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko Jimbo kuu la Lisbon, Ureno kuanzia Jumanne tarehe 1 hadi Dominika tarehe 6 Agosti 2023 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Basi, Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda.”Lk 1:39. Utakuwa ni wakati wa kukutana na vijana wengine wenye ndoto ya amani na udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika imani Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kwa wale watakaoshindwa washiriki kwa njia ya mitandao. Amewatakia wote safari ya Kipindi cha Majilio kinachosimikwa katika: amani, ukarimu, watu kukutanika, kufahamiana na ujenzi wa ujirani mwema, msamaha na huduma.

Elimu na Amani

 

29 Novemba 2022, 15:16