Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 19 Novemba 2022 amekutana na kuzungumza na Madaktari Wenza wa Afrika, CUAMM. Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 19 Novemba 2022 amekutana na kuzungumza na Madaktari Wenza wa Afrika, CUAMM.  

Papa Francisko: CUAMM: Afya, Chakula na Maji ni Sehemu ya Haki Msingi za Binadamu!

Mambo msingi: Afya, chakula na majii kama sehemu ya haki msingi za binadamu; Hija ya Kitume nchini Sudan ya Kusini, Ushirikiano wa CUAMM na Makanisa mahalia; Madhara ya majanga asilia. Vijana Barani Afrika wajengewe uwezo ili waweze kushiriki kikamilifu katika maendeleo pamoja na kuendelea kuwa ni Wasamaria wema, mashuhuda wa Injili ya upendo kwa watu Barani Afrika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hayati Padre Francesco Canova, ni daktari aliyebahatika kutekeleza utume wake nchini Yordan, kunako miaka 1950 ndiye Muasisi wa Madaktari Wenza wa Afrika, CUAMMMissionary Doctors, Doctors with Africa CUAMM”, wanaoongozwa na kauli mbiu “Euntes curate infirmos” yaani “Nendeni mkawahudumie wagonjwa” kwa kutambua kwamba, afya ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza katika maendeleo na maboresho ya sekta ya afya, kama kikolezo cha maendeleo fungamani ya kibinadamu. Lengo la mwanzo kabisa la CUAMM lilikuwa ni kuwaandaa wanafunzi madaktari ambao wangesadaka maisha yao kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa katika Nchi za Bara la Afrika, hususan: Tanzania, Uganda, Msumbiji, Angola, Ethiopia, Sierra Leone na Sudan ya Kusini. CUAMM wamekuwa wadau muhimu katika huduma hospitalini, vyuo vya wakunga na wauguzi pamoja na kutoa mafunzo kwa wanafunzi kwenye taasisi za elimu ya juu pamoja na vyuo vikuu. Serikali ya Italia ndiye mfadhili mkuu wa Madaktari Wenza wa Afrika, CUAMM ambao wanaendelea kujipambanua katika huduma hospitalini, tiba muafaka na katika mchakato wa kuzuia magonjwa. Kimsingi hawa ni Wamisionari Madaktari Wenza wa Afrika wanaoendelea kutekeleza Agizo la Shirika la Afya Duniani, WHO la Mwaka 1978 kwamba, afya bora ni sehemu ya haki msingi za binadamu na kichocheo kikuu cha maendeleo fungamani ya binadamu.

CUAMM ina mshikamano wa dhati na Bara la Afrika
CUAMM ina mshikamano wa dhati na Bara la Afrika

Madaktari Wenza wa Afrika, CUAMM, kwa mwaka 2022 wanaadhimisha Kumbukizi ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwao, kielelezo cha upendo na huduma ya mshikamano dhidi ya magonjwa yanayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 19 Novemba 2022 amekutana na kuzungumza na Madaktari Wenza wa Afrika, CUAMM. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amekazia kuhusu: Afya bora, chakula, maji safi na salama kama sehemu ya haki msingi za binadamu; Hija ya Kitume nchini Sudan ya Kusini, mwanzoni mwa Mwezi Februari 2023; Ushirikiano wa CUAMM na Makanisa mahalia; Madhara ya majanga asilia katika maisha ya watu wa Mungu Barani Afrika. Vijana Barani Afrika wajengewe uwezo ili waweze kushiriki kikamilifu katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wao pamoja na kuendelea kuwa ni Wasamaria wema, mashuhuda wa Injili ya upendo kwa watu wanaoteseka. Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru Madaktari Wenza wa Afrika, CUAMM kwa huduma ya Injili ya Upendo Barani Afrika katika kipindi cha miaka 70 iliyopita, kwa kujikita zaidi katika majiundo ya madaktari mahalia. Barani Afrika kuna rasilimali watu inayopaswa kuendelezwa na kudumishwa na kwamba, Bara la Afrika linapaswa kuendelezwa na wala si kunyonywa na kugeuka kuwa ni uwanja wa vita.

Madaktari Wenza wa Afrika, miaka 70 ya huduma ya afya Barani Afrika
Madaktari Wenza wa Afrika, miaka 70 ya huduma ya afya Barani Afrika

Afya bora, chakula pamoja na maji safi na salama ni sehemu ya haki msingi za binadamu zinazojitokeza hata katika ile Sala kuu ya Baba Yetu wa mbinguni. Hata katika Karne ya Ishirini na Moja, bado utu, heshima na haki msingi za binadamu zinaendelea kusigimwa na magonjwa. Hii ni aibu kubwa sana kwa Jumuiya ya Kimataifa ambayo inatumia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kukuza na kudumisha viwanda vya silaha. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwekeza katika huduma bora za afya ili kuokoa maisha ya Mama na Mtoto, ambao wengi wao wanapoteza maisha wakati wa kujifungua. Kwa mara ya kwanza, Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2015 alifanya hija ya kitume nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati na kuzindua rasmi Maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei ya Huruma ya Mungu. Hii ni kumbukumbu ambayo imekita mizizi yake katika akili na kuzama katika sakafu ya moyo wake. Mwanzoni mwa mwezi Februari 2023, Baba Mtakatifu ametia nia ya kutembelea Sudan ya Kusini, ambako bado watu wengi wanateseka kwa sababu ya vita, njaa na ukame wa kutisha. Madaktari Wenza wa Afrika, CUAMM, wamekuwa Wasamaria wema, vyombo na mashuhuda wa Injili ya huruma na mapendo; huduma ambayo imetolewa kwa ujasiri mkubwa, changamoto na mwaliko kwa Madaktari hawa kutokukata tamaa hata kidogo, bali waendelee kuwa ni wahudumu na wajenzi wa haki na amani.

CUAMM Nchini Tanzania
CUAMM Nchini Tanzania

Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza Madaktari hawa kwa kushirikiana na kushikamana na Makanisa mahalia kwa ajili ya huduma ya tiba kwa watu wa Mungu Barani Afrika. Wamekuwa ni wadau muhimu katika huduma kwa kushirikiana pia na Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Barani Afrika kwa ajili ya huduma kwa maskini. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, vita, majanga asilia, myumbo wa uchumi Kitaifa na Kimataifa sanjari ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, -UVIKO-19 yanaendelea kuwaathiri watu wengi Barani Afrika, kiasi cha kuanza kusuasua katika mchakato wa maendeleo kutokana na umaskini, njaa na magonjwa. Magonjwa ni vita nyingine inayoendelea chini kwa chini Barani Afrika kana kwamba haipo vile, lakini watu wengi wanateseka na kupoteza maisha. CUAMM inapaswa kugeuka na kuwa ni sauti kwa watu wasiokuwa na sauti Barani Afrika na hasa zaidi wawe ni sauti ya maskini na wanyonge. Wajipange vyema, ili kuhakikisha kwamba, wanasaidia kuwaandaa vijana ambao ni rasilimali watu na wadau katika mustakabali wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. 

CUAMM wekezeni kwa vijana Barani Afrika.
CUAMM wekezeni kwa vijana Barani Afrika.

CUAMM ijenge madaraja ya kuwakutanisha madaktari kutoka Afrika na wale wa Italia katika masuala ya masomo ya Chuo kikuu, tafiti pamoja na kukuza kipaji cha ubunifu. Lengo ni kusaidia kunogesha mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Baba Mtakatifu mwishoni mwa hotuba yake, amewakumbuka wamisionari wanaendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu Barani Afrika. Anawakumvìbuka na kuwaombea wamisionari na madaktari walipoteza maisha yao Barani Afrika wakati wakitoa huduma katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Madaktari Wenza wa Afrika, CUAMM, wapige moyo konde na waendelee kutangaza na kushuhudia Injili ya Upendo inayosimikwa katika huduma makini kwa watu wa Mungu Barani Afrika.

Papa Cuamm
19 November 2022, 16:11