Padre Sabino Maffeo SJ: Miaka 100 ya Kuzaliwa & Miaka 85 ya Utawa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu wote, tarehe 1 Novemba ya kila Mwaka, Mama Kanisa anapenda kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa, shukrani na utukufu kwa ajili ya watakatifu wote hata wale ambao bado hawajatambuliwa rasmi na Kanisa lakini ni sehemu ya umati mkubwa wa wateule wa Mungu “Baada ya hayo nikaona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za Mwana-Kondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao.” Ufu 7:9. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema kwamba, watu wote wanaitwa kuwa ni watakatifu na wakamilifu kama alivyo Baba yao wa mbinguni. Wafuasi wa Kristo wanaitwa kuwa watakatifu kadiri ya neema na hivyo kuhesabiwa haki katika Kristo Yesu katika Ubatizo wa imani unaowafanya kuwa kweli ni watoto wa Mungu na washiriki wa tabia ya Mungu, na hivyo watakatifu halisi.
Kumbe, wanapaswa kujivika moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu na wawe na matunda ya Roho ili wafanywe watakatifu. Watambue kwamba, huku bondeni kwenye machozi, mara nyingi wanajikwaa ndiyo maana wanapaswa kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu. Rej. Lumen gentium 40. Maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu wote ni kutambua utakatifu wa Kanisa unaosimikwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Rej. Lumen gentium 39. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Wote, tarehe Mosi Novemba 2022, Padre Sabino Maffeo, SJ., ameadhimisha Jubilei ya Miaka 100 ya kuzaliwa na Miaka 85 tangu alipojiunga na Shirika la Wayesuit. Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii ya Jubilei ya Miaka 100 ya kuzaliwa na Miaka 85 ya wito na upendo unaofumbatwa katika huduma, kumpongeza Padre Sabino Maffeo, SJ. Katika maisha na wito wake, kuanzia mwaka 1968 hadi mwaka 1973 aliteuliwa kuwa ni mkuu wa Shirika la Wayesuit, Kanda ya Roma. Na kuanzia mwaka 1973 hadi mwaka 1985 aliteuliwa kuwa ni Mkurugenzi Idara ya Ufundi ya Radio Vatican.
Kati ya Mwaka 1985 hadi mwaka 2017 aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Anga ya Vatican na Mtunza Pango Hifadhi ya Nyaraka za Vatican. Padre Sabino Maffeo, SJ. anasema Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, ni kiongozi ambaye amejisadaka na kujiachilia kuwa ni chombo cha huduma mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Hii ni huduma ambayo ameitekeleza wakati wote kwa furaha, upendo, ari na moyo mkuu wa huduma. Katika hali ya uzee, sasa amekabidhiwa dhamana yak usali kwa ajili ya Kanisa na Shirika la Wayesuit. Mtakatifu Augustino Askofu na Mwalimu wa Kanisa anasema, nguvu ya mwanadamu inajionesha kwa namna ya pekee katika udhaifu wa Mungu. Baba Mtakatifu anamsihi sana Padre Sabino Maffeo, SJ., kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala. Hatimaye, mwishoni, amemweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Kanisa pamoja na kumpatia baraka zake za kitume!