Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni Ngazi ya Kijimbo 20 Novemba 2022
Na Padre Philemon Anthony Chacha, SDB., - Vatican.
Tunapoadhimisha Sherehe ya Bwana wetu Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu katika Kipindi cha mwaka C wa Kanisa na tunapojiandaa kuingia kwenye mwaka mpya wa Kanisa, yaani Mwaka A, Baba Mtakatifu Francisko anatoa ujumbe kwa vijana wote ulimwenguni katika maadhimisho ya Siku ya Vijana kwa Makanisa mahalia. Hii ni siku ambayo vijana wanaungana na Maaskofu pamoja na viongozi wa Makanisa mahalia kusherekea Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni katika ngazi ya kijimbo. Ujumbe huu unaambatana na maandalizi ya tukio kubwa ambalo litafanyika katika jimbo kuu la Lisbon nchini Ureno kuanzia tarehe 1-6, Agosti 2023 katika Maadhimisho ya siku ya Vijana Duniani. Ujumbe huu wa Baba Mtakatifu unabebwa na Kauli mbiu isemayo: “Basi Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda” (Lk 1:39). Haya ni maneno tunayosikia kutoka kwa mwinjili Luka baada ya Mariamu kutokewa na Malaika Gabrieli na kupewa Habari kuwa atakuwa Mama wa Mungu. Mariamu baada ya kusikia hayo anaiunuka na kuanza safari ya kwenda kwa Elizabeti, kwa kuwa ana hakika kwamba mpango wa Mungu ndio mpango bora zaidi kwa Maisha yake. Hii inaonyesha shauku ambayo Bikira Maria alikuwa nayo ya kuwatangazia na kuwashuhudia wengine Habari Njema ya Wokovu, yaani, Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu.
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika vijana wote kuiga mfano wa Mama Bikira Maria ambaye alikataa daima kujifikiria yeye mwenyewe bali alitoka na kumwelekea Mwenyezi Mungu ambaye ni Mkuu pamoja na kuwaelekea jirani zake, hasa wale walio na mahitaji makubwa, kama binamu yake Elizabeti. Bikira Maria aliwafikiria wengine zaidi kuliko kujifikiria yeye mwenyewe. Baba Mtakatifu anawaalika vijana wote kujiuliza na kutafakari maswali yafuatayo: “Ninaitikiaje mahitaji ninayoona kunizunguka pande zote? Je, ninafikiria wakati mwingine sababu fulani ya kutojihusisha? Au ninaonesha kupendezwa na utayari wa nia ya kusaidia? Katika ulimwengu huu wetu wa leo ambao umeghubikwa na mambo mengi kama vile Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, vita, uhamaji wa kulazimishwa, umaskini, vurugu na majanga asilia au athari za mabadiliko ya tabianchi; kuna kishawishi cha kujiuliza maswali mengi ya kwanini yote haya yanatokea. Baba Mtakatifu anawaalika vijana kutokulalamika wala kutokukata tamaa, badala yake waweze kujiuliza: ninaishi kwa ajili ya nani? (Rej. Christus Vivit, 286). Hili ni swali muhimu ambalo linapelekea vijana kujua na kutambua kuwa Maisha yao si kwa ajili yao tu pekee yao bali ni kwa ajili ya wengine. Hivyo hawana budi kujitoa kikamilifu, kuzika ubinafsi na uchoyo, ili kuweza kuwafikia watu wengi zaidi hasa wale wanohitaji msaada wao.
Bikira Maria, kijana wa Nazareth aliweza kutoka kwa haraka kwenda kushirikisha wengine ile zawadi ambayo alikuwa ameipokea; anakuwa ni mfano wa kijana ambaye anashirikiana na kushikamana na wengine katika kukutana, kushiriki, upendo na huruma ya Mungu. Anakuwa mfano wa kijana ambae anakataa kusimama mbele ya kioo ili kujitafakari mwenyewe; ambaye anakataa kuwa mbinafsi na mchoyo; kijana ambaye anakataa kunaswa kwenye “wavu wa utandawazi” usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Baba Mtakatifu anaendelea kwa kutofautisha kati ya haraka nzuri ambayo hutupeleka juu na kuwaelekea wengine, bila uwekezaji wowote wa kibinafsi; na ile haraka isiyofaa, inayowasukuma kuishi kijujuu na kuchukulia kila kitu kirahisi. Kumbe, tukiwa na haraka nzuri itapelekea kuangalia wengine zaidi na kutambua kuwa wana shida na wanahitaji wakati wetu na msaada wetu. Baba Mtakatifu anawataka vijana wawe na moyo wa ukarimu wa kweli kama waliouonesha Elizabeti na Zakaria walipowakaribisha nyumbani kwao Bikira Maria na Mtoto Yesu. Elizabeti aliposikia ile salamu ya Bikira Maria, alijawa na nguvu ya Roho Mtakatifu. Mshangao kama huo na kumiminiwa kwa nguvu ya Roho huja pale tu tunapoonesha ukarimu wa kweli, tunapotoa kipaumbele cha kwanza kwa wengine wala sio sisi wenyewe.
Kristo Yesu alikuja ulimwenguni na akataka kukaa pamoja nasi na kushirikisha maisha yake, hivyo hatuna budi nasi pia kumkaribisha katika maisha yetu kwa sababu yeye ni jibu la Mungu kwa changamoto zinazowakabili wanadamu katika kila zama. Ndivyo Baba Mtakatifu anavyowataka vijana kumkaribisha Yesu na kumwangalia Bikira Maria kama mfano wa mtu anayewaonesha jinsi ya kukaribisha zawadi hii, kushiriki na wengine na hivyo kumleta Kristo Yesu, upendo wake wa huruma na huduma yake ya ukarimu kwa wanadamu wote waliojeruhiwa na kupondeka moyo! Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika vijana wote kushiriki katika hija kubwa ya vijana wa Mataifa yote itakayofikia kilele chake katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko Jimbo kuu la Lisbon, Ureno mwezi Agosti 2023. Ni katika nchi hii ya Ureno, huko Fatima, ndipo Bikira Maria alipowatokea na kuwashirikisha watu wa marika yote ujumbe wenye nguvu na adhimu wa upendo wa Mungu unaookoa; upendo unaotuita kufanya toba na wongofu wa ndani na uhuru wa kweli. Baba Mtakatifu anawataka vijana wote kuinuka. Kama Bikira Maria kwenda kwa haraka. Kumbeba Yesu ndani ya mioyo yao na kumleta kwa wale wote wanaokutana nao. Roho Mtakatifu daima aendelee kuwasha mioyoni mwao hamu ya kuinuka na furaha ya kusafiri pamoja, kwa mtindo wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Ewe Kijana unasubiri nini. Mkaribishe Yesu katika maisha yako, umbebe ndani ya moyo wako na uende ukamtangaze na kumpeleka kwa watu wote katika ulimwengu wetu wa leo. Wakati ndio sasa, changamkia fursa!