Tafuta

Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Mtoto Duniani 20 Novemba 2022 ni “Usawa zaidi; Kushirikishwa kwa kila mtoto.” Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Mtoto Duniani 20 Novemba 2022 ni “Usawa zaidi; Kushirikishwa kwa kila mtoto.”  

Maadhimisho Siku ya Mtoto Duniani 20 Novemba 2022: Ushirikishwaji wa Watoto

Kauli mbiu Maadhimisho ya Siku ya Mtoto Duniani 20 Novemba 2022 ni “Usawa zaidi; Kushirikishwa kwa kila mtoto.” Watoto wanapaswa kushirikishwa ili kutambua athari za mabadiliko ya tabianchi; umuhimu wa kupata elimu bora, kuganga na kuponya magonjwa ya afya ya akili; kutokomeza mifumo ya ubaguzi; kuwajengea mazingira bora, kuwasikilia na kutekeleza madai yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya Watoto Duniani ilianzishwa kwa mara ya kwanza kunako mwaka wa 1954 kama Siku ya Watoto Wote na huadhimishwa na Jumuiya ya Kimataifa tarehe 20 Novemba ya kila mwaka ili kukuza umoja, mshikamano na mafungamano ya kimataifa, ufahamu miongoni mwa watoto duniani kote, na kuboresha ustawi, maendeleo na mafao ya watoto wote. Tarehe 20 Novemba 1959 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Tamko la Haki za Mtoto na Mwaka 1989 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Mkataba wa Haki za Mtoto. Tangu 1990, Siku ya Watoto Duniani pia inaadhimisha kumbukumbu ya tarehe ambayo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Azimio na Mkataba wa haki za watoto. Hii ni siku muhimu sana kwa maisha ya watoto kijamii na Kimataifa. Hii ni siku ya kusimama kidete kutetea, kukuza na kudumisha haki msingi za watoto kwa kutafsiri haki hizi kwa vitendo vinavyopania kuboresha ulimwengu wa watoto. Kauli mbiu inayonogesha ya Maadhimisho ya Siku ya Mtoto Duniani 20 Novemba 2022 ni “Usawa zaidi; Kushirikishwa kwa kila mtoto.” Watoto wanapaswa kushirikishwa ili kutambua athari za mabadiliko ya tabianchi; umuhimu wa kupata elimu bora, kuganga na kuponya magonjwa ya afya ya akili; kutokomeza mifumo mbalimbali ya ubaguzi, kwa kutoa sauti yao ili watu wazima waweze kuwajengea mazingira bora zaidi, kwa kusikiliza na kutekeleza madai yao halali.

Siku ya Mtoto Duniani 20 Novemba 2022 Ushirikishwaji wa watoto
Siku ya Mtoto Duniani 20 Novemba 2022 Ushirikishwaji wa watoto

Ulinzi wa utu, heshima na haki msingi za mtoto ni dhamana na wajibu wa kisiasa na kijamii na Kanisa linatambua haki hizi msingi katika maisha na utume wake; kama ilivyo kwa “Tamko la Haki za Mtoto la Mwaka 1959” na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa haki za Mtoto wa Mwaka 1989 na kama haki hizi zinavyofafanuliwa kwenye Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kuwawezesha watoto kukua na kukomaa katika mazingira bora na salama katika maisha na utu wao. Mama Kanisa anasema, hawa ni watoto walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, walipewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kristo Yesu. Unyenyekevu wa watoto ni mfano bora wa kuigwa kwa wale wanaotaka kuingia kwenye Ufalme wa Mungu. Lakini, Yesu anaonya kwamba, ole wake atakayemkwaza mtoto mdogo, itabidi afungiwe jiwe la kusagia shingoni na kuzamishwa baharini! Changamoto pevu kwa wakati huu ni ulinzi wa utu, heshima na haki msingi za watoto na vijana; ukuaji wao makini na salama; furaha na matumaini yao kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kulinda na kudumisha haki msingi za watoto, hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba, watoto wanapata elimu bora na huduma msingi ya afya hasa kwa wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi.

Kuna watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi
Kuna watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi

Watoto hawa wamejikuta wakitumbukia na kutumbukizwa katika wimbi la wakimbizi na wahamiaji sehemu mbalimbali za dunia. Matokeo yake ni kwamba, baadhi yao wana nyanyaswa, wanadhulumiwa na kutumbukizwa katika biashara ya binadamu na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo! Kuna watoto wanaofariki dunia kutokana na baa la njaa na utapiamlo mkali; magonjwa yanayoweza kuzuilika na kutibika pamoja na ujinga! Watoto hawa ni mboni ya jicho la Kristo! Kanisa litaendelea kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, haki za watoto zinalindwa na kuheshimiwa na kwamba, watoto wanapewa haki ya kufurahia utoto wao katika mazingira: salama, ya amani na utulivu na kwamba, watoto hawa wasipokwe furaha na matumaini yao kwa sasa na kwa siku za usoni! Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika Nia zake za Jumla kwa Mwezi Novemba 2022, katika ujumbe wake kwa njia ya video, inayosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali na kuwaombea watoto wanaoteseka kwa sababu mbalimbali; watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; wahanga wa vita na wale wanaopelekwa mstari wa mbele kama chambo; wote hawa wapewe fursa ya kupata elimu na kuonja upendo kutoka katika familia zao.

Watoto wana haki ya kupata faraja, amani na utulivu kutoka kwenye familia zao
Watoto wana haki ya kupata faraja, amani na utulivu kutoka kwenye familia zao

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, katika ulimwengu mamboleo kuna watoto wanaoteseka na kuishi katika mazingira magumu na hatarishi mithili ya utumwa. Hawa ni watoto wenye majina, sura na utambulisho ambao wamepewa na Mwenyezi Mungu na wala si namba au idadi yao inayowafanya watu kuwavutia hisia. Watu wanasahau dhamana na wajibu wao kwa watoto hawa na matokeo yake, wanawanyanyasa, wanawanyonya na kuwadhulumu, kiasi cha kupokwa haki yao ya kucheza, kusoma na kuwa na ndoto ya maisha bora zaidi. Hawa ni watoto ambao kamwe hawafurahii hata kidogo fukuto na maisha na upendo wa kifamilia. Kwa mtoto yoyote anayedhulumiwa, anayetelekezwa, bila kupelekwa shule au kupatiwa matibabu muafaka ni kilio kinachopaa mbinguni kwa Baba wa milele na hii ni aibu kwa miundo mbinu ambayo imejengwa na watu wazima na kwamba, kutelekezwa kwa watoto katika mazingira magumu na hatarishi ni makosa ya familia na jamii katika ujumla wake. Kimsingi watoto wanayo haki ya kupata elimu, kupendwa na watambue kwamba, kwa hakika Mwenyezi Mungu kamwe hajawasahau. Kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali na kuwaombea watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, yatima na wahanga wa vita. Wawe na uhakika wa kupata elimu na fursa ya kufurahia upendo wa kifamilia.

Siku ya watoto duniani
21 November 2022, 15:26