Maadhimisho ya Kongamano la 53 Ekaristi Takatifu Kimataifa 8-15 Septemba 2024: Ecuador
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, Fumbo la Ekaristi Takatifu linawakirimia waamini chakula cha uzima wa milele na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, ili hatimaye, kuweza kushiriki katika maisha, uzima na utukufu wa Baba wa milele! Ekaristi Takatifu inajenga fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Mwili na Damu yake Azizi inayotolewa kwa ajili ya kurutubisha maisha ya walimwengu. Kwa kumpokea Kristo Yesu kwa imani, mwamini anakuwa sawa na Yesu na hivyo kufanyika kuwa mwana katika Mwana. Kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Kristo Yesu anaandamana na wafuasi wake kama ilivyokuwa kwa wale Wafuasi wa Emau! Anasafiri na waja wake katika historia ili kuwakirimia imani, matumaini na mapendo; kwa kuwafariji wakati wa majaribu na magumu ya maisha; na hatimaye, kuwaunga mkono katika mchakato wa mapambano ya kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa; ni chemchemi ya utakatifu wa maisha ya waamini, kumbe, linapaswa lisadikiwe kwa dhati, liadhimishwe kwa ibada na uchaji na limwilishwe kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Umoja, inayowaunganisha waamini kuwa ni mwili mmoja na watu watakatifu wa Mungu.
Mwamini anayepokea Ekaristi takatifu anakuwa ni chombo cha umoja, kwani ndani mwake kunaibuka “vinasaba ya maisha ya kiroho” vinavyosaidia kujenga umoja. Mkate wa Umoja unasaidia kuvunjilia mbali maamuzi mbele sanjari na tabia tabia ya kujiona kuwa ni bora zaidi kuliko wengine; watu wanaopenda kuwagawa wengine kwa mafao binafsi; watu wenye wivu na umbea unaohatarisha umoja na mshikamano. Waamini kwa njia ya kuliishi kikamilifu Fumbo la Ekaristi Takatifu: wana mwabudu na kumshukuru Kristo Yesu, kwa zawadi hii kubwa; kumbukumbu hai ya upendo wake unaowaunganisha wote kuwa ni mwili mmoja na kuwaelekeza katika ujenzi wa umoja. Tume ya Kipapa ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa ilianzishwa rasmi na Papa Leo XIII kunako mwaka 1876 ili kusaidia mchakato wa kumwezesha Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu: Kufahamika, kupendwa na kutumikiwa kwa njia ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Kumbe, Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kitaifa na Kimataifa katika maisha na utume wa Kanisa ni katekesi fungamani na endelevu inayogusa: Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Mwanga linalobubujika kutoka katika Neno la Mungu linalohitaji: Kusomwa, kutangazwa na kushuhudiwa kama kielelezo cha imani tendaji. Ni fumbo Linalohitaji usikivu wa kiibada na ukimya wa kitafakari uwezeshao Neno la Mungu kugusa akili na nyoyo za watu.
Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya kiroho na kielelezo cha uwepo angavu na endelevu wa Kristo Yesu kati ya waja wake. Ekaristi takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti na shule ya Upendo; ni zawadi na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani; kielelezo cha huduma inayomwilishwa na kuwasha mapendo kwa Mungu na jirani. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko ameridhia kwamba, Maadhimisho ya Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “53rd International Eucharistic Congress” (IEC) yaadhimishwe Jimbo kuu la Quito lililoko nchini Ecuador. Maadhimisho haya yataanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 8-15 Septemba 2024. Maadhimisho haya yananogeshwa na kauli mbiu “Udugu wa kuponya Ulimwengu: “Nanyi nyote ni ndugu.” Mt 23: 8. Ujumbe wa udugu wa kibinadamu unagusa masuala mbalimbali ya kijamii, ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kukimbilia Moyo Mtakatifu wa Yesu ili a pate kuwaganga na kuwaponya. Maadhimisho haya yanakwenda sanjari na maadhimisho ya miaka 150 tangu Ecuador ilipowekwa chini ya ulinzi na mambolezi ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kisima cha huruma na upendo tarehe 25 Machi 1874. Hii ikawa ni nchi ya kwanza kabisa duniani kujiweka chini ya ulinzi na maombezi ya Moyo Mtakatifu wa Yesu.
Kwa sasa Kanisa nchini Ecuador linataka kupyaisha Ibada hii katika maisha na utume wake, ili kuganga na kuponya nyoyo za watu waliojeruhiwa kwa matukio mbalimbali katika maisha yao. Haya ni matukio makuu katika maisha na utume wa Kanisa yanayopata chimbujko lake katika Fumbo la Pasaka kwa ajili ya kunogesha mchakato wa uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda tayari kupyaisha imani inayomwilishwa katika huduma kwa watu wa Mungu Amerika ya Kusini. Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kwenda Ecuador katika Ibada ya Misa Takatifu ya kufunga rasmi Maadhimisho ya Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Kimataifa. Itakumbukwa kwamba, Kongamano la Ekaristi Kimataifa kufanyika Amerika ya Kusini ilikuwa ni mwaka 2004 kule Guadalajara. Baada ya Miaka 20 Kongamano linarejeshwa tena Amerika ya Kusini. Lengo ni kuhakikisha kwamba, matunda ya Ekaristi Takatifu yanasaidia mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili sanjari na kupyaisha imani ya watu wa Mungu Amerika ya Kusini. Huu ni mwaliko kwa waamini kuanza maandalizi mapema ili kuendelea kudumisha uwepo angavu wa Mungu katika maisha ya watu. Fumbo la Ekaristi Takatifu lipewe nafasi yake katika maisha na vipaumbele vya waamini, kwa kujitahidi kumwilisha matendo yake.