Kongamano la 25 la Shughuli za Kichungaji Kijamii: Changamoto
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mafundisho Jamii ya Kanisa yanapata chimbuko lake mintarafu kanuni na muundo wa elimu fahamu, taalimungu, hususan taalimungu maadili ambayo ni dira na mwongozo wa maisha ya watu. Yanachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa na imani thabiti ambayo inamwilisha Neno la Mungu katika matendo, kielelezo cha imani tendaji. Mambo msingi katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu: Amani katika ukweli, haki, upendo na uhuru. Hizi ni tunu ambazo ni urithi mkubwa kwa binadamu wote kwani zinabubujika kutoka katika asili ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu hivyo zinapaswa kulindwa, kutetewa na kuheshimiwa na wote; kwa kuzingatia kwamba, haki inakwenda sanjari na wajibu; hakuna haki pasi na wajibu. Hii ni haki ya kuishi, kupata huduma bora ya makazi, afya, elimu, kuabudu, uhuru wa dhamiri, uhuru wa kuchagua mfumo wa maisha; haki za kiuchumi na kisiasa pamoja na uhuru wa kwenda unakotaka kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo. Kanisa Katoliki lina amana na utajiri mkubwa wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayopata chimbuko lake katika Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Leo XIII; Mambo Mapya; Rerum Novarum.
Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” anawaalika waamini kujikita katika mchakato wa uinjilishaji mpya wenye mhuri wa furaha ambayo daima ni mpya na ambayo waamini wanapaswa kuwashirikisha jirani zao, baada ya kukutana na Kristo Yesu katika maisha yao. Hii ni furaha inayoinjilisha, inayopendeza na kufariji. Furaha ya Injili ni chachu ya kutangaza na kushuhdia imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Baba Mtakatifu anakazia ari na mwamko wa kimisionari ndani ya Kanisa; mambo yanayopaswa kujikita katika shughuli za kichungaji zinazofumbatwa katika majadiliano, toba na wongofu wa kichungaji na kimisionari. Jumuiya za Kikristo zinapaswa kusoma alama za nyakati, tayari kujibu changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu mamboleo, hasa uchu wa mali na madaraka; uvunjifu wa utu, heshima na haki msingi za binadamu; tayari kujikita katika mchakato wa utamadunisho na ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili.
Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo, kwa kutambua kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Wakristo wote wanashiriki: Unabii, Ufalme na Ukuhani wa Kristo Yesu. Kumbe, wote ni wafuasi wamisionari! Tafakari ya Neno la Mungu, Ibada kwa Bikira Maria, Katekesi ya kina na endelevu ni kati ya mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa! Anasema, mchakato wa uinjilishaji hauna budi kuwa na mwelekeo wa kijamii, kwa kukazia Mafundisho Jamii ya Kanisa; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kwa kujikita katika kutafuta na kudumisha misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Juhudi zote hizi zinakwenda sanjari na majadiliano ya kidini, kiekumene, kitamaduni na kisiasa ili kukuza uhuru wa kidini, utu na heshima ya binadamu! Huu ndio msukumo mpya wa wainjilishaji waliojazwa nguvu ya Roho Mtakatifu, kwa kuwa na ari na mwelekeo mpya wa kimisionari. Kwa ufupi haya ndiyo mawazo makuu yanayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili.
Hivi karibuni, kuanzia tarehe 31 Oktoba hadi tarehe 12 Novemba 2022, Jimbo kuu la Buenos Aires, nchini Argentina, limeadhimisha Kongamano la 25 la Shughuli za Kichungaji Kijamii, kwa kuangalia uhalisia wa matatizo, changamoto na fursa zilizopo kwa watu wa Mungu jimboni humo kwa kuongozwa na kauli mbiu “Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema” Rum 12:21. Huu ni mwaliko wa kuwa makini katika sera na mikakati ya kichungaji kwa kujikita katika ubunifu, kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja, kwa ajili ya mustakabali wa Mama Kanisa kwa sasa na kwa siku zijazo. Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa washiriki wa Kongamano la 25 la Shughuli za Kichungaji Kijamii Jimbo kuu la Buenos Aires. Changamoto za Kitaifa na Kimataifa zinajionesha kwa namna ya pekee katika: Utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za atomiki kwa ajili ya vita, jambo ambalo ni kinyume cha maadili na hatari yake ni kubwa sana. Vita, Magonjwa ya Mlipuko kama Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 na madhara yake; athari za mabadiliko ya tabianchi; wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; kukua na kupanuka kwa mfumo wa utandawazi usiojali utu, heshima na haki msingi za binadamu.
Litania ya changamoto hizi inaweza kuwa ndefu sana, na kwamba, familia ya Mungu Jimbo kuu la Buenos Aires inaweza kuongeza changamoto zake pia. Jambo la msingi ni kuwa na sera na mikakati ya pamoja, kwa kujenga utamaduni wa kukutana, kujadiliana, kuamua na kutenda kwa pamoja kama sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi; daima, utu, heshima, haki msingi, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi vikipewa kipaumbele cha pekee. Huu ni mwaliko wa kujikita katika ujenzi wa utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi unaosimikwa katika umoja na utofauti. Jambo hili linawezekana ikiwa kama waamini watajenga ujirani mwema, utamaduni wa kusikiliza na kusikilizana; wa kufahamiana na kusaidiana kwa kutambua kwamba, katika muktadha kama huu, kamwe magugu hayawezi kukosekana. Rej. Mt 13: 24-30. Jambo la msingi ni kukubali uhalisia wa mambo ili kuweza kujenga Argentina kama nchi lengwa. Jambo la msingi ni waamini kujisadaka bila ya kujibakiza, kwa kujikita katika huduma na uaminifu kwani hakuna cha bure, lazima watu watokwe jasho. Rej. Evangelium gaudium, 96.