Tafuta

Papa Francisko akizungumza na Hayati Kardinali Richard Kuuia Baawobr wa Jimbo la Wa nchini Ghana Papa Francisko akizungumza na Hayati Kardinali Richard Kuuia Baawobr wa Jimbo la Wa nchini Ghana 

Kardinali Richard Kuuia Baawobr, MAfr., Askofu wa Jimbo la Wa Ghana: 1959-2022

Baba Mtakatifu anapenda kutumia fursa hii kutuma salam zake za rambirambi. Anamkumbuka Hayati Kardinali Richard K. Baawobr, WF., kwa ushuhuda na uaminifu wake katika kutangaza Habari Njema ya Wokovu na huduma kwa watu wa Mungu nchini Ghana. Ni kiongozi aliyekuwa na jicho la pekee sana kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maana ya Kikristo ya Fumbo la kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu ambaye ndani yake mna tumaini la Wakristo. Mkristo anayekufa katika Kristo huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote! Kwa Mkristo, siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo, kufanana kamili na sura ya Mwana, kulikotolewa kwa Mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme, uliotangulizwa katika Ekaristi, hata kama ana lazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi! Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha waamini kulitafakari Fumbo la kifo, kama sehemu ya matumaini ya Kikristo kwani, Kristo Yesu mwenyewe anasema, ndiye ufufuo na uzima na kwamba, yeyote anayemwamini ajapokufa atakuwa anaishi na kwamba, heri yao wale wote wanaokufa katika Kristo Yesu.

Kardinali Richard Kuuia Baawobr 1959-2022
Kardinali Richard Kuuia Baawobr 1959-2022

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa simanzi kubwa taarifa ya kifo cha Kardinali Richard Kuuia Baawobr, MAfr., Askofu wa Jimbo la Wa, nchini Ghana kilichotokea tarehe 27 Novemba 2022 katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, mjini Roma ambako alikuwa anapatiwa matibabu. Baba Mtakatifu anapenda kutumia fursa hii kutuma salam za rambirambi kwa watu wote wa Mungu walioguswa na kutikiswa na msiba huu mzito. Anamkumbuka Hayati Kardinali Richard Kuuia Baawobr, MAfr., kwa ushuhuda na uaminifu wake katika kutangaza Habari Njema ya Wokovu na huduma kwa watu wa Mungu nchini Ghana. Ni kiongozi aliyekuwa na jicho la pekee sana kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu anaungana na watu wote wa Mungu kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Hayati Kardinali Richard Kuuia Baawobr, MAfr., ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aweze sasa kumwangazia mwanga wa maisha ya uzima wa milele, ili aweze kupumzika kwa amani. Baba Mtakatifu anapenda kutoa baraka zake za kitume kwa wale wote wanaomwombolezea Hayati Kardinali Richard Kuuia Baawobr, MAfr., wapate faraja na matumaini kwa Kristo Yesu, Mwana Mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu!

Kardinali Baawobr alikuwa na jicho la pekee kwa maskini
Kardinali Baawobr alikuwa na jicho la pekee kwa maskini

Itakumbukwa kwamba, Hayati Kardinali Richard Kuuia Baawobr, MAfr., alizaliwa tarehe 21 Juni 1959, Jimboni Wa, nchini Ghana. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa na kikasisi, tarehe 5 Desemba 1986 akaweka nadhiri zake za daima. Tarehe 18 Julai 1987 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tangu wakati huo, amekuwa ni Paroko msaidizi kwenye Parokia la Livulu, Jimbo kuu la Kinshasa, DRC. Kuanzia mwaka 1991 hadi mwaka 1996 alikuwa masomoni kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian akichukua masomo ya Sayansi ya Biblia na baadaye akatunukiwa Shahada ya Uzamivu katika somo la Taalimungu Biblia. Kunako mwaka 1996 hadi mwaka 1999 akatumwa nchini Tanzania kama mlezi kwenye nyumba ya Shirika la Wamissionari wa Afrika, huko Kahangala, Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania, hapa watu wa Mungu Jimbo kuu la Mwanza wanamkumbuka kwa utume wa familia kama Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Hapa ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Kuanzia mwaka 1999 hadi mwaka 2004 akateuliwa kuwa Mkurugenzi wa nyumba ya malezi huko Tolosa, nchini Ufaransa. Kunako mwaka 2004 hadi mwaka 2010 akachaguliwa kuwa ni kati ya washauri wakuu wa Shirika la Wamisionari wa Afrika, maarufu kama “White Fathers.”

Amekuwa ni Rais wa SECAM kwa kipindi kifupi sana.
Amekuwa ni Rais wa SECAM kwa kipindi kifupi sana.

Kunako mwaka 2010 akachaguliwa kuwa Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Afrika, akiwa ni Mwafrika wa kwanza kuchaguliwa kuliongoza Shirika hili tangu kuanzishwa kwake! Amekuwa pia ni Makamu mkuu wa Taasisi ya Masomo ya Kiarabu na Kiislam mjini Roma, PISAI. Kunako mwaka 2015 alishiriki katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia baada ya kuchaguliwa kuwakilisha Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Duniani kuanzia tarehe 4-25 Oktoba 2015. Tarehe 17 Februari 2016 akateuliwa kuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Wa nchini Ghana na kuwekwa wakfu tarehe 7 Mei 2016. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, kuanzia tarehe 25 Julai hadi tarehe 1 Agosti 2022, liliadhimisha mkutano wake mkuu wa 19 huko Accra, nchini Ghana kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Umiliki wa SECAM: Usalama na Uhamiaji Barani Afrika na Visiwani na kumchagua Askofu Richard Kuuia Baawobr, WF., kuwa Rais wa SECAM. Tarehe 27 Agosti 2022, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa ni Kardinali. Tarehe 27 Novemba 2022 akafariki dunia katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, iliyoko mjini Roma. Kwa ufupi kabisa, Hayati Kardinali Richard Kuuia Baawobr, MAfr., amelitumikia Kanisa kama Padre kwa muda wa miaka 35, kama Askofu akifundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa muda wa miaka 6 na kama Kardinali, Mshauri wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa muda wa miezi miwili tu, matendo makuu ya Mungu.

Msiba SECAM
Kiswahili 30112022
30 November 2022, 17:52