Jukwaa la Kimataifa la Vijana Wakatoliki: Uinjilishaji, Ushuhuda na Utamadunisho wa Injili
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Jukwaa la Kimataifa la Vijana Wakatoliki kuanzia “Forum Internazionale di Azione Cattolica, FIAC” tarehe 26-27 Novemba 2022 limefanya mkutano mkuu ambao umehudhuriwa na wanachama kutoka Bara la Amerika, Ulaya, Asia; na Bara la Afrika linawakilishwa na nchi za: Burkina Faso, Burundi, Cameroon, Kenya, Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rwanda, Senegal, Zambia na Zimbabwe. Maadhimisho ya Jukwaa hili yamenogeshwa na kauli mbiu: Matendo ya Vijana wa Katoliki: Shauku ya ubinadamu uliopyaishwa katika Kristo Yesu, Jukwaa la Kimataifa la Vijana Wakatoliki. Wakati wa Sinodi; katika ulimwengu uliojeruhiwa; Pamoja na kila mtu na kwa kila mtu. Jukwaa la Kimataifa la Vijana Wakatoliki ni matunda ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ya Mwaka 1987 iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu “Wito na utume wa walei katika Kanisa na Ulimwengu.” Sinodi ilihudhuriwa na viongozi walei kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Wakaona hitaji la kujenga Jukwaa ambalo lingeweza kuwakutanisha kama waamini walei ndani ya Kanisa Katoliki. Wazo hili lilipata baraka kutoka kwa Mtumishi wa Mungu, Kardinali Eduardo Francisco Pironio, aliyekuwa Rais wa Baraza la Kipapa la Walei.
Kwa mara ya kwanza Baraza kuu la Jukwaa la Kimataifa la Vijana Wakatoliki likakutana kunako mwaka 1991. Nchi wanachama waasisi ni: Argentina, Austria, Malta, Hispania na Italia. Mkutano mkuu uliomalizika Dominika tarehe 27 Novemba 2022 amefanya marekebisho katika Katiba pamoja na kuwachagua viongozi wapya watakaoongoza katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2023-2026. Viongozi wakuu wanatoka Italia, Argentina na Burundi. Pia kuna mwakilishi mmoja mmoja kutoka katika kila Bara. Ni katika muktadha wa Uchaguzi Mkuu, Baba Mtakatifu Francisko amewatumia ujumbe wa pongezi, kwa viongozi waliochaguliwa kuliongoza Jukwaa la Kimataifa la Vijana Wakatoliki, ambalo katika maisha na uwepo wake takribani miaka 30 iliyopita limeendelea kushiriki katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda na utamadunisho. Watambue kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, watu ambao wanapaswa kuwa tayari kujisadaka kwa ajili ya uinjilishaji unaopania kuleta upyaisho katika maisha ya watu na kama njia ya kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili.
Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba hii ni huduma makini hasa baada ya wanachama kushindwa kukutana kutokana na changamoto za kiafya zilizosababishwa na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Huu ni mwaliko wa kupambana kufa na kupona dhidi ya uchoyo na ubinafsi; ubabe na tabia ya baadhi ya Mataifa kutaka kujimwambafai. Jukwaa la Kimataifa la Vijana Wakatoliki liwe ni shuhuda wa mchakato wa ujenzi wa matumaini, tayari kupambana na shida zinapojitokeza, kinzani na migawanyiko pamoja na kuwa tayari kuibeba kwa imani na matumaini Misalaba inapojitokeza katika hija ya maisha ya mwanadamu hapa ulimwenguni. Baba Mtakatifu anasema Mama Kanisa kwa sasa anajielekeza zaidi katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, mwaliko wa kutembea pamoja na katika mwelekeo mmoja kuelekea katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo. Kumbe, kuna haja ya kuragibisha na kumwilisha mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi katika ngazi mbalimbali za maisha na utume wa Kanisa. Kwa roho ya Kisinodi, watu wa Mungu wanapaswa kujenga utamaduni wa kusikilizana, kupyaisha ustadi wa kuzungumza na jirani, bila kuweka vizuizi au ubaguzi, bali kujenga ujirani mwema, kwani huu ndio utendaji wa Mwenyezi Mungu.
Baba Mtakatifu anawataka viongozi wapya waliochaguliwa kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na wajibu wao kadiri ya sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na Jukwaa hili, jambo la msingi ni kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini, makundi mbalimbali ya watu kutoka katika uhalisia wa maisha yao na kuwa tayari kujibu kilio chao. Viongozi wajifunze kusikiliza kwa saburi, katika ukweli na uwazi, huku wakiwa na moyo wa Msamaria mwema. Viongozi wawe tayari kugusa na kuganga madonda ya jirani zao kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini. Wawe tayari kusoma alama za nyakati, kwani Mama Kanisa anataka kuwa ni mshiriki mwaminifu wa historia na matukio ya watu wa Mungu. Kanisa la Kisinodi ni Kanisa la Kinabii linalohitaji kusoma alama za nyakati na kuzipatia tafsiri sahihi, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu, katika kazi na nguvu ya huduma ya upendo. Ili kuweza kufanikisha yote haya anasema Baba Mtakatifu kuna haja ya kumsikiliza Roho Mtakatifu, tayari kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kipaumbele ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko; huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; utume pamoja na kuongeza bidii ya kujikomboa, tayari kutumwa ulimwenguni, kielelezo cha mitume wamisionari.