Jubilei ya Miaka 50 ya Utume wa FOCSIV: Amani, Upendo na Maendeleo!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Shirikisho la Mashirika ya Kikristo ya Huduma ya Hiari ya Kujitolea Kimataifa lilianzishwa kunako mwaka 1972 na kwa sasa lina jumla ya Mashirika 94 yenye wanachama 27, 000 wanaotekeleza dhamana na majukumu yao katika nchi 80 Ulimwenguni. Kama dira yake, FOCSIV inapenda kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa Ulimwengu unaosimikwa katika msingi wa haki, amani na udugu wa kibinadamu kati ya jamii na watu. Huu ni Ulimwengu unaojengwa kwa kushirikiana, kwa kuheshimiana na kuthamini kazi ya Uumbaji, ambamo kila mtu anaweza kupata utimilifu wa utu wake kama binadamu. Utume wake ni kujishughulisha na ujenzi wa jamii inayoongozwa kwa tunu msingi za Kiinjili, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza ili kujenga na kudumisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu; Ushirikiano wa Kimataifa; kwa kujenga na kuimarisha mitandao ya kimataifa ili kukuza na kuhudumisha mahusiao na mafungamano, daima likijitahidi kutumia fursa zilizopo kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoendelea kuibuliwa katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu.
FOCSIV pamoja na mambo mengine inapania: kuragibisha sera, mipango na mikakati ya ujenzi wa jamii inayoheshimu haki msingi za binadamu, usawa na umoja wa Kitaifa na Kimataifa ndani na nje ya nchi husika. Ni katika muktadha huu, Shirikisho la Mashirika ya Kikristo ya Huduma ya Hiari ya Kujitolea Kimataifa, FOCSIV linaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Ulimwengu mikononi mwako, lakini ndoto moyoni mwako.” Huu ni mwaliko wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika umoja, upendo na ukarimu. Katika kipindi cha miaka 50 ya uwepo, maisha na utume wake, wamekuwa ni wasanii na wajenzi wa amani; mashuhuda wa Injili ya upendo; Wasamaria wema na chachu ya maendeleo fungamani ya binadamu sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa wanachama hawa alikazia: haki msingi za binadamu, mchango mkubwa unaotolewa na watu wanaojitolea Kimataifa; umuhimu wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika msingi wa amani; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wawe ni wajenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, FOCSIV imekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya mifumo ya umaskini na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo; kwa kujikita katika utu, heshima na haki msingi za binadamu mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Bado kashfa ya baa la njaa duniani inaendelea kusigina utu, heshima na haki msingi za binadamu, changamoto ni watu wote wa Mungu kushirikiana na kushikamana ili kukabiliana kikamilifu na changamoto hizi. Umefika wakati wa kunyamazisha silaha zinazoendelea kukoleza Vita Kuu ya Tatu ya Dunia inayopiganwa vipande vipande, ili kujenga na kudumisha amani. Watu wa kujitolea katika ngazi mbalimbali wamekuwa ni mifano bora, mashuhuda na vyombo vya Injili ya huruma na mapendo, kielelezo makini cha mshikamano wa upendo wa kidugu, mwaliko na changamoto kwa waamini kuwa kweli ni Wasamaria wema wanaotekeleza dhamana na wajibu wao kila kukicha. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, utamaduni wa kifo unatishia usalama, haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa.
Haki na Amani ni fadhila muhimu sana katika kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Lakini, amani haina budi kupata chimbuko lake kutoka katika sakafu ya moyo wa mwanadamu.Amani ya kweli inajengwa katika msingi wa majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Maendeleo ya kweli hayana budi kugusa mahitaki ya mtu mzima: kiroho na kimwili na kwamba, amani ni jina jipya la maendeleo. Kumbe, maendeleo hayana budi kusaidia maboresho katika huduma ya elimu, afya, fursa za ajira, majadiliano na uhuru wa kidini. Kimsingi, huu ni mchakato unaosimikwa katika haki jamii. Leo hii kuna makundi makubwa ya vijana wanaolazimika kuzikimbia nchi zao kwa kutafuta maisha bora zaidi; kuna wanawake na watoto wanaotafuta: hifadhi, usalama na uhakika wa maisha. Athari za mabadiliko ya tabianchi, madhulumu, nyanyaso na ukatili ni kati ya mambo yanayopelekea wimbi kubwa la umaskini duniani.