Tafuta

Papa Francisko anashiriki katika maadhimisho ya Kongamano la Bahrain la Majadiliano: Mashariki na Magharibi Kwa Ajili ya Kuishi Pamoja Kwa Binadamu. Papa Francisko anashiriki katika maadhimisho ya Kongamano la Bahrain la Majadiliano: Mashariki na Magharibi Kwa Ajili ya Kuishi Pamoja Kwa Binadamu.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Bahrain: Hotuba Kwa Viongozi wa Kisiasa, Kidiplomasia na Kiraia

Papa amekazia umuhimu wa familia kama inavyofafanuliwa kwenye Katiba ya Bahrain kama mti wa maji ya uhai yanayojenga na kuimarisha udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika misingi ya kuheshimiana, maridhiano na uhuru wa kidini. Wahamiaji na wakimbizi wamekuwa na mchango mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu kwenye Ufalme wa Bahrain.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya 39 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa nchini Bahrain kuanzia Alhamisi tarehe 3 hadi Dominika tarehe 6 Novemba 2022, ni kwa ajili ya kushiriki katika maadhimisho ya Kongamano la Bahrain la Majadiliano: Mashariki na Magharibi Kwa Ajili ya Kuishi Pamoja Kwa Binadamu. Ni fursa pia ya kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo sanjari na ujenzi wa udugu wa kibinadamu, kama sehemu ya mchakato wa kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Ni wakati wa kunogesha majadiliano ya kidini ili kujenga na kudumisha amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu katika ulimwengu mamboleo ambao umegubikwa kwa kiasi kikubwa na: vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Majadiliano ya kiekumene na kitamaduni pia ni muhimu katika kukuza mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu. Lengo la dini, kimsingi ni kudumisha majadililiano ya kidini na kitamaduni; umoja, mshikamano na ushirikiano wa Kimataifa, ili kujielekeza zaidi katika ujenzi wa utamaduni wa amani, maridhiano, mshikamano wa kidugu na upatanisho wa Kitaifa na Kimataifa. Mambo makuu yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza ni: Udugu wa kibinadamu, Mshikamano na Amani.

Papa Francisko amekazia umuhimu wa kudumisha tunu msingi za kifamilia
Papa Francisko amekazia umuhimu wa kudumisha tunu msingi za kifamilia

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Awali amelakiwa na wenyeji wake na baadaye akaelekea kwenye Ikulu ya Mfame iliyoko Sakhir na hapo akamtembelea kwa faragha Mfalme Hamad bin Isa bin Salman Al Khalifa pamoja na familia yake na hapo akapata mapokezi ya Kitaifa, akakagua gwaride la heshima na kupigiwa mizinga ishirini na moja kwa heshima yake. Baadaye, Baba Mtakatifu akakutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, Wanadiplomasia pamoja na Viongozi wa vyama vya kiraia. Katika hotuba yake, amekazia umuhimu wa familia kama inavyofafanuliwa kwenye Katiba ya Ufalme wa Bahrain kama mti wa maji ya uhai yanayojenga na kuimarisha udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika misingi ya kuheshimiana, maridhiano na uhuru wa kidini. Wahamiaji na wakimbizi wamekuwa na mchango mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu kwenye Ufalme wa Bahrain. Baba Mtakatifu amezungumzia pia kuhusu: changamoto ya ukosefu wa fursa za ajira duniani, haki sawa pamoja na maboresho ya maisha ya wafanyakazi. Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, madhara ya kinzani na vita sehemu mbalimbali za dunia na kwamba, imani ni msingi wa amani duniani.

Papa: Umuhimu wa kudumisha utandawazi wa mshikamano na udugu
Papa: Umuhimu wa kudumisha utandawazi wa mshikamano na udugu

Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza watu wa Mungu kwenye Ufalme wa Bahrain kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya kifamilia sanjari na utunzaji bora wa mazingira unaouwezesha Ufalme huu, kuwa na uhakika wa maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya binadamu licha kwamba sehemu kubwa ya nchi ni jangwa tupu na ukame. Ni nchi ambayo imefanikiwa kutumia nafasi yake ya kijiografia kukuza na kuendeleza vipaji vya wananchi wake; pamoja na ushiriki wao katika matukio mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa, ambayo kimsingi yamekuwa ni utajiri mkubwa kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wa Ufalme wa Bahrain.  Baba Mtakatifu ameusifia umoja wao unaosimikwa katika tofauti msingi, zinazowawezesha wote kuishi kwa amani, upendo na mshikamano na watu kutoka katika makabila na mataifa mbalimbali. Huu ndio utandawazi wa mshikamano unaojenga dunia na kuifanya kuwa kama Kijiji, kielelezo makini cha udugu wa kibinadamu na ukarimu unaokoleza amani, upendo na mshikamano. Inasikitisha kuona kwamba, katika baadhi ya nchi misimamo mikali ya kidini na kiimani na tabia ya baadhi ya watu katika jamii kutaka kujimwambafai, ni mambo ambayo yamepelekea uvunjifu wa haki, amani na usalama. Kumbe, maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia imekuwa ni fursa ya mchakato wa ujenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu wa Mungu.

Udugu wa kibinadamu ni chanzo cha amani na upendo
Udugu wa kibinadamu ni chanzo cha amani na upendo

Baba Mtakatifu anawahamasisha wananchi wa Ufalme wa Bahrain kuendelea kujikita katika ujenzi wa umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kwa kujenga madaraja yanayowakutanisha kutoka katika tamaduni na dini mbalimbali kwa lengo la kufanya kazi pamoja na kuendelea kupandikiza mbegu ya amani duniani. Hii ndiyo dhima ya Maadhimisho ya Kongamano la Bahrain la Majadiliano: Mashariki na Magharibi Kwa Ajili ya Kuishi Pamoja Kwa Binadamu. Changamoto kubwa kwa sasa ni kushiriki katika ujenzi wa urafiki wa kijamii, ambao umeoneshwa kwa namna ya pekee kabisa na viongozi mbalimbali wa dini ya Kiislam katika miaka ya hivi karibuni. Hii ni safari ya udugu wa kibinadamu inayolenga kudumisha amani duniani. Ufalme wa Bahrein umeendelea kujipambanua katika kukuza na kudumisha heshima, maridhiano na uhuru wa kidini; mambo msingi yanayopewa uzito wa pekee katika Katiba ya Ufalme wa Bahrain, dhidi ya ubaguzi, kwa kukazia uhuru wa dhamiri pamoja na uhuru wa kuabudu. Haya ni mambo muhimu sana yanayopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu kwa kuyasimika katika misingi ya: utu, fursa sawa kwa wote sanjari na kujikita katika utekelezaji wa haki msingi za binadamu; yaani Injili ya uhai dhidi utamaduni wa kifo.

Haki, amani, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu
Haki, amani, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu

Baba Mtakatifu Francisko ameishukuru Serikali ya Ufalme wa Bahrain kwa kuonesha ukarimu, mshikamano na mafungamano na wakimbizi pamoja na wahamiaji, ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Ufalme wa Bahrein. Huu ni mwaliko wa kupambana kufa na kupona na ukosefu wa fursa za ajira duniani, kwani kuna baadhi ya watu wanageuza changamoto hii kwa ajili ya kuwatumbukiza watu wengine katika mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo. Huu ni wakati muafaka kwa watu kuendeleza haiba yao kwa njia ya kazi safi na inayojali: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Wafanyakazi watazamwe kama watu huru na wanaowajibika kwa kumwangalia binadamu katika utu wake mzima, kwa kuimarisha pia afya ya kiroho na kimwili kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu katika maisha ya kiuchumi na kijamii katika ujumla wake. Rej. Gaudium et spes, 9, 27, 60, 67. Baba Mtakatifu anaipongeza Serikali ya Ufalme wa Bahrein kwa kujenga shule ya kwanza kwa ajili ya wanawake Ukanda wa Ghuba pamoja na kufuta Biashara ya Utumwa, changamoto ni kuendelea kujikita katika msingi wa haki sawa, maboresho ya maisha ya wafanyakazi na maeneo ya kazi; kwa kuwaheshimu na kuwasaidia wasiokuwa na ajira, maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, hawa ni kipimo cha ustawi na maendeleo ya nchi husika.

Utunzaji Bora wa Mazingira ni wajibu wa kimaadili.
Utunzaji Bora wa Mazingira ni wajibu wa kimaadili.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa hana budi hawana budi kujizatiti katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sanjari na utunzaji bora wa mazigira nyumba ya wote, ili kuweza kukabiliana vyema na athari za mabadiliko ya tabianchi. Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) utakaofanyika nchini Misri, Mwezi Novemba 2022, unaonesha umuhimu wa utunzaji wa bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na deni kubwa la kiikolojia linalohitaji wongofu wa Kiikolojia. Ni wakati wa kusimama kidete kujenga na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika vita, kielelezo makini cha ubinafsi, kinzani na ukosefu wa uaminifu. Ni wakati wa kuondokana na gharama kubwa ya ununuzi wa silaha na badala yake, rasilimali fedha hii itumike katika mchakato wa mapambano dhidi ya umaskini magonjwa na njaa yanayoendelea kusigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu amewakumbuka sana watu wa Mungu nchini Yemen wanaoendelea kuteseka kutokana na vita ambayo inaonekana kana kwamba, imesahauliwa. Huu ni wakati wa kuondokana na vita nchini Yemen na kuanza kujikita katika ujenzi wa amani ya kudumu. Amewataka waamini wa dini mbalimbali kuwa ni wajenzi na vyombo vya amani duniani! Itakumbukwa kwamba, Ijumaa tarehe 4 Novemba 2022, Baba Mtakatifu atashiriki kufunga Maadhimisho ya Kongamano la Bahrain la Majadiliano: Mashariki na Magharibi Kwa Ajili ya Kuishi Pamoja Kwa Binadamu. Atakutana na kuzungumza na wajumbe wa Baraza Kuu la Wazee wa Kiislam kwenye Msikiti mkuu wa Sakhir. Atahitimisha siku kwa Sala ya Kiekumene itakatoadhimishwa kwenye Kanisa Kuu la Bikira Maria wa Uarabuni.

Bahrain: Viongozi

 

03 November 2022, 16:30