Hayati Askofu Mkuu Chrysostomos II 10-Aprili 1941 - 7 Novemba 2022
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Askofu mkuu Chrysostomos II “Χρυσόστομος Β”, wa Jimbo kuu la Cyprus nzima, Kanisa la Kiorthodox aliyezaliwa kijijini Irodotos Dimitriou, “Ηρόδοτος Δημητρίου” tarehe 10 Aprili 1941, amefariki dunia tarehe 7 Novemba 2022 huko mjini Nicosia kwa ugonjwa wa Saratani ya ini, akiwa na umri wa miaka 81. Aliteuliwa kuwa Askofu wa Pathos tarehe 25 Februari 1978 na kuwekwa wakfu kuwa Askofu, tayari kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu tarehe 26 Februari 1978. Tarehe Mosi Oktoba 2006 akateuliwa na kusimikwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cyprus nzima na hatimaye, amefariki dunia tarehe 7 Novemba 2022. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake Jumatano tarehe 9 Novemba 2022 aliungana na watu wa Mungu nchini Cyprus kumwombolezea Askofu mkuu Chrysostomos II, wa Jimbo kuu la Cyprus nzima, Kanisa la Kiorthodox. Ni kiongozo aliyejipambanua katika shughuli za kichungaji, akiwa na maono ya mbali. Ni mtu aliyejikita katika majadiliano, alipenda kukuza na kudumisha amani. Kwa hakika alikuwa ni chombo na shuhuda wa upatanisho, haki na amani ndani na nje ya Cyprus. Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee kabisa anamkumbuka kwa uwepo wake, wakati wa hija yake ya kitume nchini Cyprus na Ugiriki.
Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake alikazia umuhimu: wa kukuza na kudumisha ushirika katika utofauti wao; kukuza fadhila ya uvumilivu kwa sababu watu wanataka kuona Kanisa ambalo limejengwa na kusimikwa kwenye fadhila ya uvumilivu. Historia na maisha ya Mtakatifu Barnaba Mtume, aliyebahatika kukutana na Sauli huko Tarso na huo ukawa ni mwanzo wa kukuza na kudumisha udugu wa kibinadamu. Ndiyo maana waamini wanahitaji kuona Kanisa la kidugu, kama wakala wa mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu Francisko anamwombea mwanga wa milele, maisha na pumziko la amani miongoni mwa wateule wa Mungu huko mbinguni. Hayati Askofu mkuu Chrysostomos II “Χρυσόστομος Β”, ni kiongozi aliyesimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha kanuni msingi, maadili na utu wema. Alitambua na kuhimiza umuhimu wa shule na taasisi za elimu kuwa ni mahali pa malezi, makuzi na majiundo makini ya watoto na vijana wa kizazi kipya: Kiakili, kimaadili na utu wema. Hii ni misimamo iliyomletea taabu katika maisha na utume wake, lakini akapiga moyo konde na kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo. Baba Mtakatifu Francisko alisikitishwa sana na uamuzi wa Serikali ya Uturuki kuligeuza Kanisa kuu la Mtakatifu “Hagia Sophia” lililoko mjini Instanbul kuwa msikiti kwa ajili ya waamini wa dini ya Kiislam.
Hayati Askofu mkuu Chrysostomos II aliungana na viongozi mbalimbali ya dini ya Kikristo kulaani maamuzi haya yaliyokuwa yanakinzana na uhuru wa kuabudu sanjari na uhuru wa kidini. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walitangaza “declarat” kwamba binadamu anayo haki ya uhuru wa dini. Uhuru huo ndio huu, kwamba, kila binadamu lazima akingiwe na shurutisho la mtu mmoja mmoja, la makundi ya kijamii, au la mamlaka yoyote ya kibinadamu. Hivyo kwamba, katika mambo ya dini mtu yeyote asishurutishwe kutenda dhidi ya dhamiri yake, wala asizuiliwe, katika mipaka inayokubalika kutenda kulingana na dhamiri yake binafsi au hadharani, peke yake au katika muungano na wengine. Haki ya uhuru wa dini msingi wake ni hadhi ya binadamu ijulikanayo kwa njia ya Neno la Mungu lililofunuliwa na ya akili. Haki hii ya binadamu ya uhuru wa dini yatakiwa kuzingatiwa katika sheria za jamii ili iwe haki ya raia. Rej. DH 2.
Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ulizingatia hasa: mema ya kiroho kwa kila mtu; ukweli na haki; Mapokeo na Mafundisho ya Kanisa. Mwenyezi Mungu ndiye chemchemi ya wokovu wa mwanadamu. Kanisa linawajibu wa kutangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, linahimiza umuhimu wa kulinda dhamiri nyofu pamoja na wajibu wa kimaadili. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipania pamoja na mambo mengine, kuhakikisha kwamba: wanaendeleza Mafundisho ya Kanisa kuhusu haki msingi za binadamu zisizoondosheka na katika sheria za muundo wa jamii. Kumbe, kuna haja ya kuendelea kufunda dhamiri za watu, ili kutambua utu, heshima na haki msingi za binadamu. Rej. DH.1. Hayati Askofu mkuu Chrysostomos II “Χρυσόστομος Β”, tarehe 16 Juni 2007 alikutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na kuzungumzia kuhusu madhulumu dhidi ya Wakristo Ukanda wa Mashariki ya Kati. Viongozi hawa wakakutana tena tarehe 28 Machi 2011. Mara kadhaa wamekutana na kusali na Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi chote cha uongozi wake.