Tafuta

Don Giuseppe Bernardi Paroko na Don Mario Ghibaudo, Paroko Msaidizi waliouwawa kutokana na chuki dhidi ya imani (Odium fidei). Don Giuseppe Bernardi Paroko na Don Mario Ghibaudo, Paroko Msaidizi waliouwawa kutokana na chuki dhidi ya imani (Odium fidei).  

Wenyeheri Giuseppe Bernardi & Mario Ghibaudo: Imani na Upendo

Hata katika hatari ya kifo kilichokuwa kinawakodolea macho, Mapadre hawa wawili walisimama kidete na kushikamana na waamini wao kiasi hata cha kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Ushuhuda wa maisha na utume wao wa Kipadre uwe ni mfano bora wa kuigwa kadiri ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, mchungaji mwema, ambaye daima yuko kati pamoja nao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ilikuwa ni tarehe 19 Septemba 1943, utawala wa Kinazi ulipouvamia mji wa Boves, Cuneo, ulioko Kaskazini mwa Italia na kufanya mauaji ya kinyama yaliyosababisha watu 24 kuuwawa kikatili na nyumba 350 kuchomwa moto. Kati yao walikuwemo akina Don Giuseppe Bernardi Paroko na Don Mario Ghibaudo, Paroko Msaidizi waliouwawa kutokana na chuki dhidi ya imani (Odium fidei). Baba Mtakatifu Francisko ameyasema hayo Dominika tarehe 16 Oktoba 2022 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Hata katika hatari ya kifo kilichokuwa kinawakodolea macho, Mapadre hawa wawili walisimama kidete na kushikamana na waamini wao kiasi hata cha kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Ushuhuda wa maisha na utume wao wa Kikasisi anasema Baba Mtakatifu uwe ni mfano bora wa kuigwa na Mapadre wanaotaka kuwa ni mifano bora kadiri ya Moyo Mtukufu wa Kristo Yesu, mchungaji mwema, ambaye daima yuko kati pamoja na wafuasi wake. Matumaini ya Kikristo ni nguvu ya mashuhuda na waungama imani. Kristo Yesu, aliwaonya na kuwaambia kwamba, utangazaji, ushuhuda na ujenzi wa Ufalme wa Mungu una magumu na changamoto zake kwani watachukiwa kwa sababu ya jina lake.

Wenyeheri hawa ni mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika upendo
Wenyeheri hawa ni mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika upendo

Hili ni jambo la kushangaza sana kwani Wakristo kwa asili ni watu wanaopenda, lakini daima wanachukiwa sana. Imani thabiti inashuhudiwa katika mazingira kinzani na hatarishi! Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Wakristo ni watu wanaopambana na mawimbi makali ya maisha na kwamba, ulimwengu umejeruhiwa sana na uwepo wa dhambi. Hali hii inashuhudiwa kutokana na ubinafsi uliokithiri sanjari na ukosefu wa haki msingi za binadamu hasa kwa wafuasi wa Kristo, kwani wao wanajitahidi kukita maisha yao katika mantiki ya matumaini yaliyofunuliwa na Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Changamoto ya kwanza inayotolewa na Kristo Yesu kwa wafuasi wake ni ufukara kwa kujinasua na malimwengu, ili kuweza kutumia: amana, rasilimali, utajiri na mapaji ambayo wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hija na maisha ya Wakristo hapa duniani inapaswa kufumbatwa katika upendo na kuondokana na kishawishi kinachoweza kuwatumbukiza katika: vita, machafuko na tabia ya kulipizana kisasi! Daima wakumbuke kwamba, wanaitwa na kutumwa na Kristo Yesu kama kondoo kati ya mbwamwitu! Amani ndiyo silaha yao madhubuti, daima wakijitahidi kujivika fadhila ya busara na hekima mintarafu mwanga wa Injili. Wajitahidi kushinda ubaya kwa kutenda wema!

Ni kielelezo madhubuti cha ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.
Ni kielelezo madhubuti cha ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Nguvu na jeuri ya Wakristo ni Injili ya Kristo mwenyewe katika kipindi cha shida na karaha kwani wanatambua kwamba, Yesu daima yupo pamoja na kati yao! Mateso, dhuluma na nyanyaso ni sehemu ya vinasaba vya Injili kwani hata Kristo Yesu mwenyewe alitendwa jeuri, akateswa, akafa lakini siku ya tatu akafufuka kwa wafu. Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini Kuwa Wenyeheri na Watakatifu, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 16 Oktoba 2022 amewatangaza watumishi wa Mungu Don Giuseppe Bernardi na Don Mario Ghibaudo, Wafiadini kuwa ni Wenyeheri. Hawa sasa ni mihimili ya sala na maombezi kwa watu wa Mungu kama ilivyokuwa kwa Mtumishi wa Mungu Musa wakati Waisraeli wanapambana na Waamaleki kule Refidimu. Sala ya Musa ni mfano wa kustaajabisha wa Sala ya maombezi ambayo ilitimilizwa katika Kristo Yesu. Mababa wa Kanisa wanasema Msalaba ni sadaka ya pekee ya Kristo Yesu ambaye peke yake ni “mpatanishi kati ya Mungu na mwanadamu.” Anawapa waja wake nguvu ya kushiriki Fumbo la Pasaka kwa jinsi anavyoijua Mwenyezi Mungu. Anawaita na kuwaalika wafuasi wake kuchukua Msalaba wao na kumfuata, kwani Kristo Yesu ni kielelezo na mfano bora wa kuigwa. Rej KKK. 2574 na 618.

Waliuwawa kutokana na chuki ya imani, Odium fidei
Waliuwawa kutokana na chuki ya imani, Odium fidei

Kristo Yesu ni mwombezi kati ya Mungu na wanadamu. Huu ni mwaliko wa kuendelea kumwilisha huruma na upendo wa Mungu katika uhalisia wa maisha; utume unaotekelezwa kwa namna ya pekee na Makleri waliowekwa wakfu, tayari kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Don Giuseppe Bernardi na Don Mario Ghibaudo waliuwawa kikatili na utawala wa Nazi tarehe 19 Septemba 1943. Kanisa ni Mama, Mwalimu na Shule ya Sala, mwaliko na changamoto kwa wazazi na walezi kuwa ni vyombo na mashuhuda wa sala, kama ilivyokuwa kwa Ibrahimu na Musa Mtumishi wa Mungu. Wazazi na walezi, wasimame kidete kuwalinda na kuwatetea watoto wao mbele ya Mwenyezi Mungu, ili hatimaye, waweze kuonja huruma, upendo na msamaha wa Mungu. Kumbe, Wenyeheri wapya Don Giuseppe Bernardi na Don Mario Ghibaudo, Wafiadini wawe ni waombezi wa watu wa Mungu mbele ya Mwenyezi Mungu.

Wafiadini
17 October 2022, 16:36