Tafuta

Papa Francisko 9 Oktoba 2022 anatarajia kuwatangaza Mwenyeheri Padre Giovanni Battista Scalabrini na Mwenyeheri Artemide Zatti, kuwa watakatifu. Papa Francisko 9 Oktoba 2022 anatarajia kuwatangaza Mwenyeheri Padre Giovanni Battista Scalabrini na Mwenyeheri Artemide Zatti, kuwa watakatifu. 

Watakatifu Giovanni Scalabrini na Artemide Zatti 9 Oktoba 2022

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 9 Oktoba 2022, Dominika ya 28 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican anatarajia kuwatangaza Mwenyeheri Padre Giovanni Battista Scalabrini na Mwenyeheri Artemide Zatti, kuwa watakatifu. Ikumbukwe kwamba, utakatifu ni wito na mwaliko kwa waamini wote kujibidiisha katika maisha na utume wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 9 Oktoba 2022, Dominika ya 28 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican anatarajia kuwatangaza Mwenyeheri Padre Giovanni Battista Scalabrini na Mwenyeheri Artemide Zatti, kuwa watakatifu. Padre Giovanni Battista Scalabrini alitangazwa kuwa Mwenye heri na Mtakatifu Yohane Paulo II, tarehe 9 Novemba 1997. Alizaliwa tarehe 8 Julai 1839 na hatimaye kufariki dunia tarehe Mosi Juni 1905. Alikuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Piacenza-Bobbio, Italia na Mwanzilishi wa Mashirika ya Wamisionari wa Mtakatifu Carlo Borromeo, maarufu kama Wascalabrini na pia ni Muasisi wa Taasisi ya waamini Walei Wascalabrini, iliyoanzishwa kunako mwaka 1961. Pili ni Mwenyeheri Artemide Zatti, Bruda wa Shirika la Wasalesian wa Don Bosco aliyezaliwa tarehe 12 Oktoba 1880, nchini Italia. Akafariki dunia tarehe 15 Machi 1951 huko Viedma nchini Argentina. Utakatifu wake unapata chimbuko lake katika huduma kwa maskini kwa kuongoza hospitali na duka la dawa kwa ajili ya maskini kwa muda wa miaka 40. Tarehe 14 Aprili 2002 atakatangzwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa ni Mwenyeheri.

Utakatifu ni wito na mwaliko kwa watu wote wa Mungu
Utakatifu ni wito na mwaliko kwa watu wote wa Mungu

Upendo wa dhati ni njia inayoweza kuwapeleka waamini katika utakatifu wa maisha! Wanapaswa pia kusikiliza, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao; wajitahidi kushiriki mara kwa mara Sakramenti za Kanisa; kwa kujitia uthabiti katika kusali, kujinyima pamoja na kutekeleza matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa wahitaji zaidi. Hii ndiyo changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo.” Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu Fumbo la Kanisa wanasema, Wakristo wote wanaitwa na kuhamasishwa kushiriki utakatifu mmoja, kwa kumtii na kumwabudu Mwenyezi Mungu katika roho na kweli; kwa kumfuasa Kristo Yesu aliyekuwa ni: mtii, fukara na mnyenyekevu wa moyo, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kwa njia hii, wastahilishwe kushiriki utukufu wa Kristo Yesu!

Utakatifu unamwilishwa katika ushuhuda wa maisha adili na matakatifu
Utakatifu unamwilishwa katika ushuhuda wa maisha adili na matakatifu

Watu wote wa familia ya Mungu wanaitwa kuwa ni watakatifu, kwani haya ni mapenzi ya Mungu. Kristo Yesu ndiye chemchemi na utimilifu wa utakatifu wote! Baba Mtakatifu anasema, utakatifu ni mwaliko kwa waamini wote na wala si kwa watu wachache tu ndani ya Kanisa! Huu ni mwaliko wa kuongeza jitihada za kukutana na Kristo Yesu katika maisha kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata: huruma na upendo wa Mungu katika maisha. Watakatifu ni watu wa kawaida kabisa, ni wadhambi waliotubu na kumwongokea Mungu, leo hii wamekuwa ni marafiki zake wa karibu! Watakatifu ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao! Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Wakristo wote wamejichukulia dhamana ya kuanza mchakato wa safari ya utakatifu wa maisha! Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanazungumzia kuhusu wito wa watu wote katika Kanisa kuwa watakatifu; namna nyingine za kutekeleza utakatifu ulio mmoja na mwishoni ni njia za utakatifu.

Watakatifu wapya 2022

 

07 October 2022, 14:57