Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Siku ya 96 ya Kimisionari Ulimwenguni 23 Oktoba 2022
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kristo Yesu Mfufuka kabla ya kupaa kwenda zake mbinguni aliwaambia wafuasi wake “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.” Mdo 1:8. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 96 ya Kimisionari Ulimwenguni inayoadhimishwa na Mama Kanisa Dominika tarehe 23 Oktoba 2022 unanogeshwa na kauli mbiu “Mtakuwa mashahidi wangu” Mdo 1:8. Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anafafanua utume wa Mkristo kuwa ni shuhuda wa Kristo, kiini na utambulisho wa Kanisa linaloinjilisha, daima wakiwa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Utume wa uinjilishaji ulimwenguni kote ni mchakato dumifu, kuelekea pembezoni mwa vipaumbele vya maisha ya mwanadamu. Nguvu ya Roho Mtakatifu iwatie ujasiri wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Mkazo wa pekee umewekwa kwenye nguvu ya sala kwa kutambua kwamba, Roho Mtakatifu ndiye mhimili mkuu wa mchakato mzima wa uinjilishaji. Mwaka 2022, Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 400 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, “Propaganda fide” wakati ule wa mwaka 1622, chimbuko lake ni ile hamu ya kutekeleza Agizo la Kimisionari la kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia.
Mwenyeheri Pauline-Marie Jaricot (1799-1862) ndiye muasisi Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimisionari, dhamana aliyoitekeleza kwa muda wa miaka 15 bila kuchoka! Aliteseka sana kiroho na kimwili, lakini akaimarishwa kwa Sakramenti za Kanisa sanjari na mahusiano na mafungamano ya dhati na Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala na sadaka ya maisha yake. Mwenyeheri Pauline-Marie Jaricot akajipambanua katika huduma kwa Mungu na jirani maskini na wagonjwa. Ni huduma iliyotolewa kwa njia ya sala kwa ajili ya toba na wongofu wa watu kwa njia ya uinjilishaji ulimwenguni. Mwenyeheri Pauline-Marie Jaricot alitamani sana kuona Kristo Yesu anapendwa kuliko jambo lolote hapa duniani, kama Kristo Yesu alivyowapenda waja wake, kiasi hata cha kuyamimina maisha yake ili kuwaokoa kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Ari na moyo wake wa kimisionari bado unaendelea kupenya sehemu mbalimbali za dunia kwa njia ya misaada ya hali na mali katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kumbe, Mwaka 2022, Mama Kanisa anamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kuadhimisha miaka 200 ya imani na uinjilishaji sehemu mbalimbali za dunia. Mama Kanisa anawakumbuka pia mashuhuda wa imani kama vile Askofu Charles de Forbin-Janson kutoka Ufaransa aliyeanzisha Shirika la Utoto Mtakatifu ili kuhamasisha mchakato wa uinjilishaji miongoni mwa watoto wadogo. Ni matamanio halali ya Baba Mtakatifu Francisko kuona Wakristo wote wakiwa ni Manabii na Mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, wito wa kila Mkristo ni kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, kiini cha mafundisho ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ndiye aliyetumwa wa kwanza kuwa “Mmisionari” na “shuhuda” wa Baba wa milele. Watoto wa Kanisa wanatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu na kwamba, huu ni utambulisho wa Kanisa linaloinjilisha. Hulka ya ushirika wa Kikanisa ni umisionari ndani na nje ya Kanisa kwa kutambua kwamba, wanatumwa kwa niaba ya Kanisa na kwamba, hili ni tendo la Kikanisa linalotekelezwa na mihimili yote ya Uinjilishaji, kwa sababu kuna muungano wa neema usioonekana. Uwepo wa Jumuiya hauna budi kupewa kipaumbele cha kwanza. Wakristo watambue kwamba, wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda wa Kristo Yesu Mfufuka na fahari kubwa ya Mkristo ni kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka kwa furaha na ujasiri kama ilivyokuwa kwa Wakristo wa Kanisa la mwanzo. Wakristo wanapaswa kuwa ni mashuhuda waaminifu wa upendo wa Kristo Yesu uliomsukuma kujisadaka Msalabani kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi n amauti. Hii inatokana na ukweli kwamba, imani hutokana na kusikia, ili iweze kutangazwa; ndiyo maana ushuhuda na uinjilishaji ni chanda na pete katika muktadha wa umisionari. Ushuhuda ni kivutio kikuu cha ukuaji wa Kanisa sehemu mbalimbali za dunia.
Wakristo wanaitwa na kutumwa kutangaza Habari Njema hadi miisho ya dunia, hali inayoonesha ile tabia ya kiulimwengu, yaani kutangaza na kushuhudia na wala si wongofu wa shuruti. Wakristo wawe tayari kukabiliana na hali mbalimbali wanazoweza kukutana nazo katika maisha na utume wao. Baba Mtakatifu anagusia pia wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutokana na sababu mbalimbali katika maisha ya mwanadamu, wajibu wa Wakristo ni kuwapokea na hivyo kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa, ili liweze kuonakena zaidi kuwa na utambulisho wa Kikatoliki. Huduma ya kichungaji kwa wahamiaji na wakimbizi ipewe kipaumbele cha kwanza kama sehemu ya shughuli za kimisionari, ili kuweza kuwashirikisha wengine utambuzi wa furaha ya imani waliyoipokea kutoka kwa Kristo Yesu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa linatumwa hadi miisho ya dunia kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu; mazingira mapya ya kijiografia na ya jamii. Huu ni mchakato wa kumshuhudia Kristo Yesu kwa watu wa Mataifa kwa kuinjilisha na kutamadunisha upendo wa Kristo Yesu kwa watu wa Mataifa. Shukrani zinawaendea Wamisionari wa nyakati zote ambao wamekuwa mstari wa mbele kumwilisha upendo huo kwa wale wote waliokutana nao katika hija ya maisha yao.
Mitume walipata nguvu ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo kwa watu wa Mataifa baada ya kushukiwa na Roho Mtakatifu, kumbe, nguvu ya sala ni muhimu katika maisha ya Wakristo, ili kuwachangamotisha tena kutangaza Injili na kukiri imani yao kwa Kristo Yesu. Roho Mtakatifu ndiye Mhimili mkuu wa Uinjilishaji, ndiye anayetoa Neno sahihi, kwa wakati na kwa njia inayofaa. Roho Mtakatifu ndiye aliyetenda kazi zake ndani ya Kanisa leo hii, Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 400 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu; Miaka 200 ya imani na uinjilishaji sehemu mbalimbali za dunia utume uliotekelezwa kwa ari na moyo mkuu wa kimisionari na Mwenyeheri Pauline-Marie Jaricot, Askofu Charles de Forbin-Janson kutoka Ufaransa aliyeanzisha Shirika la Utoto Mtakatifu na Mwenyeheri Paulo Manna aliyezaliwa miaka 150 iliyopita. Hawa ni waasisi wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa ambayo yamekuwa mstari wa mbele kuenzi na kutegemeza shughuli za kimisionari sehemu mbalimbali za dunia pamoja na kupandikiza roho na kimisionari miongoni mwa watu wateule wa Mungu. Wakristo wanaitwa kuwa ni mashuhuda na watangazaji wa Habari Njema ya Wokovvu hadi miisho ya dunia kwa mujibu wa Sakramenti ya Ubatizo inayowawezesha kuwa ni: Manabii, Mashuhuda na Wamisionari wa Kristo Yesu. Bikira Maria Malkia wa Wamisionari, awaombee Wakristo wote.