Ufukara wa Kiinjili Uwe Ni Kikolezo cha Majitoleo ya Watawa kwa Kristo Yesu na Kanisa Lake
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Shirika la Wamonaki wa Cistercian; “Order of Cistercians (Latin: (Sacer) Ordo Cisterciensis” kwa kifupi wanajulikana kama “OCist au SOCist” liliasisiwa huko Cîteaux, mjini Borgogna, na Bernardo di Chiaravalle, Roberto di Molesme, Stefano Harding, Alberico di Cîteaux kunako mwaka 1098. Wanashirika wake wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanajikita katika mchakato wa ujenzi wa ushirika unaopata chimbuko lake katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, ambalo kimsingi ni chemchemi ya maisha ya kijumuiya na utambulisho wao kama wafuasi wa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni mwaliko wa kumsikiliza Kristo Yesu kwa makini na kumwangalia jinsi anavyotenda kwa upendo, ili kuchochea amani na mshikamano wa kidugu katika maisha ya kijumuiya, jambo ambalo kamwe si lelemama. Wamonaki hawa watambue kwamba, wameitwa na Kristo Yesu kwanza kabisa wajenge jumuiya itakayowawezesha kutembea kwa pamoja wakiwa wameshikamana kama ndugu wamoja, wakiwa na amana na utajiri mkubwa katika maisha yao, lakini bado pia wanaelemewa na udhaifu pamoja na mapungufu yao ya kibinadamu. Wajenge jumuiya inayosimikwa katika fadhila ya ukarimu na umisionari, tayari kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Huu ni mwaliko kwa Wanashirika kutoa nafasi kwa Roho Mtakatifu anayetenda kazi katika Kanisa, ili awawezeshe kuwa na mang’amuzi ya Pentekoste mpya katika maisha na utume wao; mang’amuzi yanayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo inayowashirikisha: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo Yesu.
Huu ni muhtasari wa hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 17 Oktoba 2022 kwa Wamonaki hawa wanaoadhimisha mkutano mkuu wa Shirika lao. Kwa njia ya Roho Mtakatifu, Mama Kanisa amekirimiwa karama na mapaji mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa, ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Licha ya tofauti za karama ndani ya Kanisa, lakini watawa wote watambue kwamba, wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili Ushirika kati ya Wamonaki unapaswa kujikita katika toba na wongofu wa ndani, matunda ya neema na baraka zinazobubujika kutoka kwenye Fumbo la Msalaba na kazi ya Roho Mtakatifu kwa mwanashirika mmoja mmoja na katika ujumla wao. Baba Mtakatifu anawaalika kukumbatia na kuambata ari na mwamko wa kimisionari; wakitambua kwamba, wanatofautiana kwa jinsia, lakini pia wanakamilishana licha ya kutoka katika nchi na mabara mbalimbali ya dunia. Hii ni safari ndefu na ngumu, lakini ni muhimu sana na imesheheni: amana na utajiri mkubwa kwa ajili ya jumuiya zao na Shirika katika ujumla wake. Waendelee kusoma alama za nyakati kwa kutambua kwamba, mchakato wa watu kukutana katika umoja na tofauti zao msingi ndio mtindo wa maisha ya kisasa. Wamonaki hawa wanachangia kwa kiasi kikubwa ujenzi wa umoja katika tofauti msingi katika maisha ya taamuli. Ni maisha yanayokita mizizi yake katika taamuli, ujenzi wa maisha ya ndani, sala na majadiliano ya maisha ya kiroho mambo msingi yanayopyaisha maisha na utume wao ndani ya Kanisa.
Baba Mtakatifu Francisko anawataka Wamonaki hawa kuzamisha maisha yao katika ufukara wa maisha ya kiroho na umiliki wa vitu, ili kujitoa na kujisadaka zaidi kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake pamoja na huduma makini kwa watu wa Mungu wanaowahudumia. Wajitoe kikamilifu bila ya kujibakiza licha ya uwepo wa dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu. Wawe ni watawa wanaomtolea Mwenyezi Mungu sifa na shukrani, kwa uzee na ujana wao; kwa kuwakirimia afya njema na hata pale wanapokabiliana na changamoto za kiafya; kwa jumuiya ambazo kwa sasa zinachungulia kaburi kwa kukosa miito na zile zinazoendelea kuchanua kama “Mwerezi wa Lebanon.” Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, katika yote, kamwe wasimpe mwanya Shetani, Ibilisi kuwapoka matumaini yao. Hii inatokana na ukweli kwamba, ufukara wa Kiinjili umesheheni matumaini na unasimikwa katika Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake. Kwa msisitizo anasema, “Heri ninyi mlio maskini, kwa sababu ufalme wa Mungu ni wenu.” Lk 6:20. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko ameliweka Shirika la Wamonaki wa Cistercian; “Order of Cistercians (Latin: (Sacer) Ordo Cisterciensis” kwa kifupi wanajulikana kama “OCist au SOCist” chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili awasindikize katika safari ya maisha na utume wao katika ufukara wa maisha ya kiroho, tayari kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili.