Sherehe ya Watakatifu Wote: Ushirika wa Watakatifu: Imani, Sakramenti na Karama
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kila mwaka ifikapo tarehe Mosi Novemba, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Watakatifu wote. Ushirika wa Watakatifu “Sanctorum communio” ni sehemu ya kiri ya imani ya Kanisa kwa kutambua ushirika wa mema ndani ya Kanisa kunakofanyika kwa njia ya Sakramenti za Kanisa pamoja na kuchota katika hazina ya pamoja. Huu ni ushirika wa mambo matakatifu na ushirika kati ya watakatifu. Ni ushirika wa imani, Sakramenti za Kanisa, Karama katika mchakato wa ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Ni ushirika wa upendo unaosimikwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, Ibada ya Kanisa kwa watakatifu wa Mungu, au visakramenti na hasa zaidi kwa Bikira Maria, ni kwamba, imani ya Kanisa inawaelekeza waamini kujenga na kudumisha uhusiano mwema na Kristo Yesu unaofumbatwa katika kiungo cha ushirika wa watakatifu. KKK 946-962.
Kimsingi Kanisa ni Jumuiya ya watakatifu na wa dhambi wanaojitahidi kutubu na kumwongokea Mungu. Utakatifu ni matokeo ya huruma na upendo wa Mungu uliofunuliwa katika Kristo Yesu, anayetakatifuza kwa kuwapenda waja wake na hivyo kuwakomboa kutoka katika udhaifu wao wa kibinadamu. Kwa njia ya Kristo Yesu, wote wanafanyika kuwa ni sehemu ya viungo vyake. Kumbe, furaha, mateso na mahangaiko ya mwanajumuiya mmmoja ni mahangaiko na mateso ya Kanisa zima. Ushirika wa watakatifu ni kiungo cha nguvu kiasi kwamba, hata kifo hakiwezi kuwatenganisha. Ushirika wa watakatifu ni muungano wa Kanisa la Mbinguni na Duniani. Kanisa lina Ibada ya pekee kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na kwa Mtakatifu Yosefu. Waamini wanakimbilia sana ulinzi na tunza ya Bikira Maria na ya Mtakatifu Yosefu kwa sababu ya dhamana na utume wao kwa Kristo Yesu. Ushirika wa watakatifu unawawezesha waamini kujisikia kwamba, wanao walinzi na waombezi mbinguni, wanaoweza kuzungumza nao mubashara. Watakatifu ni mifano bora ya maisha na tunu msingi za Kikristo, ndiyo maana waamini wanakimbilia, kuomba ulinzi na maombezi yao.