Papa kwa wanahija:kila mbatizwa aeneze utamaduni wa kukutana
Na Angella Rwezaula; – Vatican.
Jumatatu tarehe 10 Oktoba 2022, Baba Mtakatifu Francisko amekutana na wanahija waliokuja kuudhuria misa Takatifu mjini Vatican, kwa ajili ya kutangazwa Mtakatifu Giovanni Battista Sacalabrini ambapo amewasalimia na kuwashukuru ujio na kukaa nao pamoja kidogo katika maadhimisho ya tarehe 9 Oktoba. Papa amesema jinsi ambavyo wao ni mkutano mkubwa na mzuri, kwa sababu kuna wamisionari, watawa wamisionari, wamisionari walei na kuna waamini wa majimbo ya Como na Piacenza; baadaye kuna hata wahamiaji kutoka nchi nyingi. Kwa namna hiyo wao wanawakilishwa vizuri upande wa shughuli za Askofu Scalabrini, hasa wa kuwa na ufunguzi wa moyo wake wazi ambapo inawezekana kusema kwamba jimbo lake lilikuwa hata halitoshi.
Papa amesema kwamba kiukweli yeye alifanya utume wake kwa ajili ya wahamiaji waitalia. Katika wakati huo walikuwa wanaondoka mamia elfu kuelekea Amerika. Scalabrini alikuwa akiwatazama kwa mtazamo wa Kristo, mahali ambapo Injili ya Matayo inazungumza hivi: “Na alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji”, (Mt 9,36). Na aliwahangaikia kwa upendo mkubwa na akili ya kichungaji ili kuwahikishia utunzaji wa kutosha wa kimwili na kiroho. Hata leo hii, Baba Mtakatifu Francisko amesema, uhamiaji unajikita ndani ya changamoto kubwa sana. Ndani mwake unabainisha juu ya swali la lazima kujiuliza kuhusu udugu uliokataliwa na mshikamano katika sintofahamu. Leo hii, kila mbatizwa anaitwa kutafakari mtazamo wa Mungu kuelekea kaka na dada wahamiaji na wakimbizi; kuacha hata mtazamo wake upanuke katika mtazamo wetu, shukrani kwa mkutano na ubinadamu katika safari, kwa njia ya ukaribu wa dhati, kwa mfano wa askofu Scalabrini.
Baba Mtakatifu Francisko amesisitiza kuwa leo hii tunaitwa kuishi na kueneza utamaduni wa kukutana, katika kukutana sawa kati ya wahamiaji na watu wa nchi inayowakaribisha. Huu ni uzoefu wenye utajiri, kwa kile ambacho kinaonesha uzuri wa utofauti. Na hata wenye wenye kuzaa matunda kwa sababu, imani, matumani, na huruma kwa wahamiaji inawezekana kuwa mfano na kuhuisha kwa wale ambao wanataka kujibidisha kujenga ulimwengu wa amani na ustawi kwa wote. Na ili uweze kuwa hivyo kwa wote, wao wanajua vyema kwamba inahitajika kuanzia na walio wa mwisho. Kwa kutoa mfano amesema “Kama ilivyo kawaida wakati wa kupanda mlima ni kwamba ikiwa wa kwanza wanakimbia, kikundi kunajigawa, na baadaye kupasuka, kinyume chake ikiwa wanatembea kwa mwendo wa wale walio wa mwisho, basi watafika pamoja juu ya kilima”. Kwa mfano huo, Papa ameongeza kusema “ Hii ni kanuni yenye hekima. Tunapokuwa tunatembea wakati tunapofanya hija ni lazima kufuata hatua za watu walio wa mwisho. Ili kufanya ukue udugu na urafiki kijamii, sisi sote tunaitwa kuwa wabunifu, kufikiria nje ya mikakati.
Baba Mtakatifu amesema kwa wote tunaitwa kufungua nafasi mpya, mahali ambapo sanaa, muziki na kukaa kwa pamoja vinageuka kuwa vyombo vya mwendelezo wa kiutamaduni, mahali ambapo inawezekana kuonja ladha ya utajiri wa kukutana katika tofauti”. Katika hilo Baba Mtakatifu amewaalika wamisionari wote Wascalabrini kuacha kuongozwa daima na Mtakatifu mwanzilishi, Padre wa wahamiaji wote. Karama yake ipyaishwe ndani mwao furaha ya kukaa na wahamiaji. Ya kuwa wahudumu wao na kuwafanya kuwa na imani inayoongozwa na Roho Mtakatifu, kwa kuelewa kwamba kila mmoja wanaye kutana naye, wanakutana na Bwana Yesu. Hii itawasaidia kuwa na mtindo wa ukarimu wa bure na bila kupoteza rasilimali nguvu bure na uchumi kwa ajili ya kuhamasisha wahamiaji kwa namna ya kuwafungamanisha; na hii itawasaidia hata kufanya kazi kwa umoja wa maelewano, kama familia uliyoungana katika utofauti.
Baba Mtakatifu Francisko amesema, utakatifu wa Giovanni Battista Scalabrini, uweze kuwaambukiza ili wawe na shauku ya kuwa watakatifu, kila mmoja kwa namna asili, ya kipekee kama walivyoumbwa, na kama inavyo pendezwa na ubunifu wa Mungu. Kwa maombezi yake awapatie furaha na matumaini ya kutembea pamoja kuelekea Yerusalemu mpya, ambapo ni maelewano na watu, kuelekea Ufalme wa haki, udugu na wa amani. Amewabariki wao na wote wanaosindikizana katika njia zile wanazoishi.