Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 21 Oktoba 2022 amekutana na kuzungumza na viongozi wa Kanisa na wa umma kutoka Jimbo kuu la Cambrai, Ufaransa. Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 21 Oktoba 2022 amekutana na kuzungumza na viongozi wa Kanisa na wa umma kutoka Jimbo kuu la Cambrai, Ufaransa.  

Papa Francisko Wanasiasa Lindeni Maisha, Utu, Heshima Na Haki Msingi za Binadamu: Mshikamano!

Papa Francisko amewapongeza kwa ushirikiano wao unaopania kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Katika hotuba yake amekazia kwamba, uongozi ni huduma inayomwilishwa katika ukarimu na huduma bora ya afya kwa wazee na wagonjwa walioko kufani. Uongozi unapaswa kuwa ni kiungo cha umoja, daima wakijitahidi kutekeleza matakwa ya wapiga kura wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema amani ni sawa na matumaini yanayosongwa na changamoto pamoja na magumu yanayowaandama walimwengu, hasa kutokana na uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka na matokeo yake ni matumizi mabaya ya madaraka na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu. Siasa safi ni nyenzo inayosaidia ujenzi wa huduma kwa binadamu, lakini ikitumiwa vibaya inaweza kuwa ni chombo cha dhuluma, mipasuko na hatimaye, kusababisha madhara makubwa kwa jamii. Siasa safi inafumbatwa katika unyenyekevu, kielelezo makini cha huduma katika ngazi mbalimbali za maisha ya binadamu. Lengo ni kukuza na kudumisha dhamana, utu, heshima na tunu msingi za maisha zinazoiwezesha jamii kutekeleza mafao ya wengi. Kumbe, utekelezaji makini wa siasa safi ni changamoto endelevu kwa viongozi wanaopewa dhamana ya kuongoza, kwani wanapaswa kuwalinda raia wao; kwa kushirikiana kikamilifu ili kuboresha maisha ya wananchi wao katika misingi ya haki, uhuru, utu na heshima ya binadamu na kwa njia hii, siasa safi inakuwa ni chombo cha upendo!

Mafundisho Jamii ya Kanisa ni muhimu katika uwanja wa kisiasa
Mafundisho Jamii ya Kanisa ni muhimu katika uwanja wa kisiasa

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 21 Oktoba 2022 amekutana na kuzungumza na viongozi wa Kanisa na wa umma kutoka Jimbo kuu la Cambrai, Ufaransa. Ametumia fursa hii kuwapongeza kwa ushirikiano wao unaopania kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Katika hotuba yake amekazia kwamba, uongozi ni huduma inayomwilishwa katika ukarimu na huduma bora ya afya kwa wazee na wagonjwa walioko kufani. Uongozi unapaswa kuwa ni kiungo cha umoja, daima wakijitahidi kutekeleza matakwa ya wapiga kura wao. Jimbo kuu la Cambrai nchini Ufaransa katika karne ya 19 lilikuwa maarufu sana kutokana na Mapinduzi ya viwanda, lakini kutokana na myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa, eneo hili limejikuta katika hali ngumu sana ya kijamii, kitamaduni na kiuchumi kiasi cha wafanyakazi wengi kushindwa kuchangia katika ukuaji wa uchumi na hivyo kuathiri pia mchango wao utu na heshima yao. Hii ni changamoto kwa viongozi wa kisiasa kuwa karibu zaidi na wapiga kura wao, ili kusikiliza na kujibu matamanio yao ya ndani.

Utu, Heshima na Haki Msingi za Binadamu zilindwe.
Utu, Heshima na Haki Msingi za Binadamu zilindwe.

Binadamu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika masuala ya kiuchumi na kijamii; kwa kutambua kwamba, kazi ni utambulisho na utimilifu wa maisha ya binadamu, makuzi ya kiutu na kimaadili ili kuendeleleza vipaji vyao na kuziishi kikamilifu tunu za maisha; kwa kushikamana na wengine, ili kumtukuza Mungu. Kipaumbele cha kwanza kiwekwe kwenye upatikanaji wa fursa za ajira bila kujikita sana kutafuta maslahi binafsi kiuchumi na kibiashara. Rej Laudato si, no, 127. Kuhusu huduma ya afya hasa kwa wazee wanaotunzwa kwenye nyumba za wazee na kwa watu walioko kufani, lazima wapewe huduma shupaa, ili kuwafariji. Wahudumu wa sekta ya afya kwa asili wanapaswa kulinda na kudumisha uhai wa binadamu na wala si vinginevyo, ili kwenda kinyume kabisa cha utamaduni wa kutupa. Kama binadamu ataweza kuua kwa kuhesababiwa haki, Baba Mtakatifu anasikitika kusema, kwa mtindo huu watu wataishia kuuwawa zaidi. Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika medani mbalimbali za kijamii kiasi cha kuacha amana na utajiri katika tamaduni za watu kwa sasa na kwa siku za usoni.

Kifo laini ni kinyume cha utu, heshima na haki msingi za binadamu
Kifo laini ni kinyume cha utu, heshima na haki msingi za binadamu

Hii ni amana na utajiri unaofumbatwa kwa namna ya pekee katika tamaduni, maisha ya kijamii na kiakili zinazopaswa kuboreshwa na tunu msingi walizopokea ili kuzirithisha kwa watu wengine. Baba Mtakatifu anawapongeza viongozi wa umma wanaoshika nafasi za pekee katika masuala ya kiuchumi na kijamii kuvutwa zaidi na Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayowasaidia kutambua kwamba, uongozi ni huduma na mshikamano na maskini ni jambo la heri sana. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alionesha ukaribu wa pekee kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Rej. Evangelii gaudium n. 186. Leo hii wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii ni wakimbizi na wahamiaji, wazee na wagonjwa. Hakuna umaskini mkubwa katika jamii kama upweke hasi na hali ya kutengwa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi na usalama wa maisha! Wakimbizi na wahamiaji wasitelekezwe hata kidogo, kwani hii ni hatari sana; daima wasimamie utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Wanasiasa Ufaransa
22 October 2022, 14:17