Papa Francisko kwa Vijana wa Ubelgiji:Muwe na uhusiano thabiti na Yesu,rafiki mwaminifu
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kikundi cha hija ya vijana kutoka Ubelgiji, Jumatatu 10 Oktoba 2022. Katika hotuba yake, amefurahi kukutana nao na kuwasalimia kwa upendo kupitia wao na kuonesha ukaribu wa kiroho kwa vijana wote ambao wanajshughulisha kwenye parokia zao na jumuiya za kikristo nchini Ubelgiji. Ameshangazwa na imani yao kubwa, jitihada zao na ushuhuda wao wa kikristo katika jamii ya sasa ambayo inazidi kubobea malimwengu. Ni vizuri kuona vijana wa rika lao wako tayari kabisa kujitolea katika mipango ya Uinjilishaji na kuusha ujumbe wa Kristo katikati ya mahangaiko ya kila siku. Wao kama vijana sio wa wakati ujao wa Kanisa lakini hasa wa wakati uliopo, kwa sababu, kanisa linawahitaji wao, ukaribu wao, furaha yao , utashi wao wa kuweza kujenga ulimwengu tofauti uliounganishwa na thamani za kidugu, amani na upatanisho.
Vijana hao wanafanya uzoefu wa furaha na shauku, lakini wakati mwingine hata hofu, matatizo, majeraha, kukabiliana na vizingiti vyao na migogoro. Vijana wasiwe na hofu. Ndiyo matatizo yanakufanya uwe hivi na hivi, lakini lazima kwenda mbele na kutatua matatizo. Papa amewaomba wasichanganye kati ya shida na mgogoro. Kwa sababu mikasa hufanya kukua. Kwa maana hiyo ukiwa na uhusiano na Kristo unapaswa kuwa thabiti. Yeye ni rafiki mwaminifu ambaye hakatishi tamaa kamwe. Mkutano na Yesu unawaruhusu kuwa na mtazamo mpya juu ya hali halisi na kuweza kupata majibu ya maswali yao, kujigundua wenye uwezo wa kuchukuwa hatua za uwajibikaji, wa kwenda mbele katika maisha na kuimarisha imani yao kwa njia ya mazungumzo kuhusu kile wanachokiamini. Na zaidi, wasiwe na woga wa kukubali udhaifu wao, ulegevu wao, lakini waupokee kwa unyenyekevu. Vizingiti hivyo havikosi kwa kila mmoja, lakini licha ya kuhisi kuchanganyikiwa lazima waende mbele bila hofu.
Hawana haja ya kuwa mashujaa, lakini zaidi kuwa watu walio wazi, wa kweli na walio huru. Baba Mtakatifu Francisko amewaeleza vijana hao kwamba kama mabalozi wa vijana wa Ubelgi kwa ajili ya kuandaa Siku ya vijana Ulimwenguni 2023 nchini Ureno, amewaalika wakuze ukaribu na vijana wote hasa wale ambao wanaishi katika hali ngumu, vijana wahamiaji na wakimbizi, vijana wa mitaani, bila kusahau wengine hasa wale ambao wanafanya uzoefu wa maisha ya upweke na huzuni. Baba Mtakatifu hata hivyo anatambua jinsi ambavyo wana kiu ya Kanisa la kweli na tahabiti, lililotengenezwa na wanaume na wanawake wa imani hai na inayoambukiza. Na kwa maana hiyo Papa amewapatia maswali ya kujiuliza: Je mimi ninajichukulia vipi ili kukaribia hatima hiyo? Ni mchango wangu ni upi kwa ajili ya jumuiya ya kikristo yenye kuwa na furaha? Kwa kujibu ameongeza kwamba: “Furaha lazima iwe ya kila wakati, kwa sababu, Wakristo wenye uso wa mkesha wa maombolezo hawafanyi kazi, wao si Wakristo. Ikiwa wewe ni Mkristo, utakuwa na furaha”, papa Francisko amesema.
Baba Mtakatifu Francisko amesema kuwa jambo moja muhimu sana ni kuacha kuangaziwa na mashauri na ushuhuda wa wazee. Kiukweli mahali ambapo vijana wanazungumza na wazee kuna wakati ujao; ikiwa hakutakuwapo na mazungumzo hayo kati ya wazee na vijana, wakati ujao utakuwa na mashaka(rej. Katekesi 17 Agosti 2022). “Kufanya mazungumzo na mizizi, na wazee, na mababu, na tunasonga mbele”. Ni kukua katika mazungumzo na wazee, ambapo sisi sote tunaweza kufundwa kibinafsi, thabiti kwa ajili ya kupambana kila sikuna zaidi unatufanya kueneza imani na kuimarika kidini”. Kwa kuongeza Papa amesema “Moja ya mapambano hayo ni kwa ajili ya amani. Kama jinsi ambavyo wao wanajua kuwa tuko tunapitia kipindi kigumu cha ubinadamu, ambacho ni hatari kubwa.” Hii ni kweli: tuko katika hatari kubwa”, Papa amesisitiza.
Papa zaidi ya hayo amewaeleza vijana kwamba wao wawe mafundi wa amani karibu nao na ndani yao; mabalozi wa amani ili ulimwengu upate kujigundua uzuri wa upendo, wa kuishi pamoja, wa kidugu na mshikamano. Maisha yao ni jitihada ya dhati kuanzia na imani kwa ajili ya kujenga jamii moja mpya, ni kuishi katikati ya ulimwengu na katika jamii ya uinjilishaji wake, ili kufanya kukuza amani, imani, usawa, haki za binadamu, huruma, hivyo kupanua Ufalme wa Mungu katika ulimwengu (rej, Christus vivit, 168). Mbele ya changamoto hizo, Papa amesema wao wanaweza kuhisi kukata tamaa, wasio na uwezo na kukosa nguvu. Lakini wasiwe na hofu. Wao ni wabunifu, magwiji, wawe na mtazamo wao kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za maisha! Kwa kujazwa na neema ya Bwana na kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, wasisubiri hadi kesho ili kushirikiana katika kufanya mabadilisho ya ulimwengu na nguvu zao, shauku yao na ubunifu wao (Christus vivit, 178).
Baba Mtakatifu Francisko kwa vijana hao amewaomba wasichoke kamwe kuwa wabebaji wa Injili kila mahali waendako. Aidha Papa anatambua jinsi ambavyo wao ni wakarimu, waliojaa shauku, wako tayari kuushinda ulimwengu. Papa amesema kwamba wasikengeushwe na mambo yasiyo na maana katika maisha, na kuna mengi sana. Badala yake wazingatie mambo muhimu, yanayotokana na urafiki pamoja na Yesu Kristo. Kwa kuhitimisha amewametia moyo na kuwasifu sana kwa shughuli yao wanayojikita nayo katika Jumuiya. Amewakabidhi chini ya usimamizi wa Bikira Maria na Rozari yake ambayo amesema ni shule ya sala na ya maisha na kwa maombezi ya watakatifu vijana. Anawasindikiza wote kwa baraka pamoja na familia zao na vijana wote wa Ubelgiji. Wasisahau kusali kwa ajili yake pia.