Tafuta

Jubilei ya Mwaka 2025 inanogeshwa na kauli mbiu “Mahujaji wa Matumaini” Jubilei ya Mwaka 2025 inanogeshwa na kauli mbiu “Mahujaji wa Matumaini”  

Papa: Jubilei ya Mwaka 2025: Kauli Mbiu: Mahujaji wa Matumaini: Sala

Mkutano mkuu wa 37 wa Shirika la “Wamisionari wa Oblate wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili” kauli mbiu: “Mahujaji wa Matumaini katika Ushirika.” Baba Mtakatifu katika hotuba yake amewataka wawe ni: Waiinjilishaji, Mahujaji wa matumaini katika ushirika; wajikite katika utunzaji wa mazingira na Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili awe ni mwandani wa hija ya maisha yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jubilei ya Mwaka 2025 inanogeshwa na kauli mbiu “Mahujaji wa Matumaini” baada ya dhoruba ya maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 pamoja na patashika nguo kuchanika kutokana na vita inayoendelea sehemu mbalimbali za dunia. Jubilei hii ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo thabiti, kwa kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kusikiliza pamoja na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. Ni muda wa toba na wongofu wa ndani na wa Kiikolojia, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Ni muda muafaka kwa waamini kujikita katika kutangaza na kushuhudia imani na matumaini yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa kukazia umoja na utofauti wa wateule watakatifu wa Mungu. Jubilei ni muda uliokubalika na Mwenyezi Mungu wa kuhakikisha kwamba, waamini wanajitahidi kumwilisha karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Lengo ni kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Kumbe, kama sehemu ya maandalizi ya Jubilei ya Mwaka 2025, waamini wanahamasishwa kujikita katika sala, chemchemi ya baraka na neema zote. Sala ya maombi inayokita mizizi yake katika msamaha sanjari na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha; sala ya kushukuru kwa kila jambo na mwishoni ni sala ya kusifu na kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa uwepo wake wa daima.

Nembo ya Jibilei 2025
Nembo ya Jibilei 2025

Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025, Baba Mtakatifu Francisko amekita hotuba yake alipokutana na kuzungumza na “Wamisionari wa Oblate wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, O.M.I,” tarehe 3 Oktoba 2022 waliokuwa wanashiriki katika mkutano mkuu wa 37 wa Shirika ambalo lilianzishwa na Mtakatifu Charles-Joseph-Eugène de Mazenod kunako tarehe 25 Januari 1816. Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa 37 wa Shirika la “Wamisionari wa Oblate wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili” yamenogeshwa na kauli mbiu “Mahujaji wa Matumaini katika Ushirika.” Baba Mtakatifu katika hotuba yake amewataka wawe ni: Uinjilishaji, Mahujaji wa matumaini katika ushirika; umuhimu wa kujikita katika utunzaji wa mazingira nyumba ya wote na Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili awe ni mwandani wa hija ya maisha na utume wao hapa duniani. Baba Mtakatifu Francisko anasema, maadhimisho ya Mkutano mkuu wa Shirika imekuwa ni fursa kama Shirika kutafakari mustakabali wa Shirika lao kama sehemu ya uinjilishaji, kwa kutambua kwamba, wao ni mahujaji wa matumaini wanaotumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini, furaha na amani kwa watu wa Mataifa. Ni fursa ya kuondokana na utumwa unaowakandamiza na kuwatumbukiza katika wimbi la uchoyo na ubinafsi; mipasuko na kinzani mbalimbali katika maisha ya binadamu.

Mahujaji wa matumaini katika Ushirika
Mahujaji wa matumaini katika Ushirika

Huu ni mwaliko wa kusikiliza na kujibu kwa umakini mkubwa kilio cha maskini na dunia mama kutokana na kinzani, vita na mipasuko mbalimbali. Kuna mamilioni ya wakimbizi na wahamiaji ambao wanatafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Mwenendo wa uchumi unawawezesha matajiri kuendelea kutajirika zaidi wakati ambapo maskini wanazidi “kulamba vumbi.” Kumbe, ni wajibu wao kuhakikisha kwamba, walau wanatangaza na kushuhudia Injili ya Matumaini. Watambue kwamba, wao ni mahujaji hapa ulimwenguni wanaopaswa kushikamana na maskini pamoja na watu wote wa Mungu katika nchi 70 wanazozihudumia. Wawe ni mfano wa Kanisa ambalo ni “Mama na Mwalimu, yaani: “Materi et Magistra” kwa kumwilisha karama ya Shirika lao katika vipaumbele vya maisha; kwa kutangaza na kushuhudia upendo na uaminifu, unaomwilishwa katika huduma ya upendo. Huu ni mchango mkubwa unaotolewa na Shirika hili. Wawe ni mahujaji wa matumaini pamoja na watu wapendwa wa Mungu, waaminifu katika wito wao wa kimisionari, kwa kushirikishana karama yao na waamini walei, ili kwa kumtazama na kumtafakari Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka, aweze kuwa ni chemchemi ya matumaini yao. Wamisionari hawa wawe ni mahujaji wa matumaini yanayowaletea watu wa Mungu ile furaha ya kweli na kuendelea kusoma alama za nyakati.

Mashuhuda wa imani na mtumaini
Mashuhuda wa imani na mtumaini

Wamisionari hawa wajifunze kutambua matumaini miongoni mwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Baba Mtakatifu anawataka watawa hawa kuwa ni mashuhuda wa matumaini katika ushirika, unaopata chimbuko lake miongoni mwao, ili hatimaye, waweze kuwa ni wamisionari wa ushirika, ili kuishi na watu wote bina ubaguzi. Ni mwaliko wa kujikita katika mshikamano wa udugu wa kibinadamu; ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, udugu wa kibinadamu, huku wakijitahidi kuwa ni wasamaria wema, ili watu waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu. Wajenge na kudumisha ujirani mwema. Rej Lk 10: 29-37. Ni fursa muhimu ya kuondokana na tabia ya uchoyo na ubinafsi. Wawe ni wamisionari wanaosimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira nyumba ya wote, yanayohitaji wongofu wa ndani na wongofu wa kiikolojia, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili umisionari. Wakite maisha yao katika wosia na karama ya mwanzilishi wa Shirika lao, kwa ajili ya wokovu wa watu wa Mungu. Kristo Yesu na Mtakatifu Eugenio wawe ni mifano bora ya kuigwa katika kuwatangazia na kuwashuhudia watu wa Mungu upendo unaofumbatwa katika huduma. Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili awe ni mwandani wa safari zao katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake.

Jubilei mwaka 2025

 

04 October 2022, 15:54