Tafuta

Watu zaidi ya 38 wamefariki dunia, kati yao wakiwemo watoto 24 na wengine 12 kujeruhiwa vibaya nchini Thailand. Papa Francisko atuma salam za rambirambi. Watu zaidi ya 38 wamefariki dunia, kati yao wakiwemo watoto 24 na wengine 12 kujeruhiwa vibaya nchini Thailand. Papa Francisko atuma salam za rambirambi. 

Papa Francisko Asikitishwa na Mauaji ya Watoto Nchini Thailand

Papa Francisko ili kuonesha uwepo wake wa karibu kwa wale wote walioathirika anapenda kuwafariji watoto waliopata majeraha, ili waweze kupona haraka. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi hiki cha majonzi mazito, waathirika wataweza kuchota nguvu na faraja kutoka katika mshikamamano wa udugu wa kibinadamu, ndugu, jamaa na majirani zao wa karibu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Watu zaidi ya 38 wameuwawa kikatili kati yao wakiwemo watoto 24 na wengine 12 kujeruhiwa vibaya na askari wa zamani aliyetambulika kwa jina la Bwana Panya Kamran, mwenye umri wa miaka 34, ambaye hivi karibuni aliachishwa kazi Jeshini kutokana na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Bwana Kamran, Alhamis tarehe 6 Oktoba 2022 ameingia Kituo cha kulelea watoto cha Uthai Sawan, baada ya kumkosa mtoto wake shuleni hapo alianza kuwafyatulia watoto risasi na baadaye kuwauwa kikatili. Hawa ni watoto waliokuwa na umri kati ya miaka 3-4. Katika harakati za kutaka kuukimbia “mkono wa Sheria”, njiani amewagonga kwa gari watu kadhaa, na alipoingi nyumbani kwake, akamfyatulia mkewe na mtoto wao risasi na baadaye yeye mwenyewe kujimaliza kwa risasi! Ukatili na unyama wa hali ya juu kabisa.

Papa Francisko asikitikiswa na mauaji ya kikatili dhidi ya watoto
Papa Francisko asikitikiswa na mauaji ya kikatili dhidi ya watoto

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wa rambirambi uliotumwa kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Thailand, ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, ameonesha masikitiko na majonzi makubwa kutokana na msiba huu mzito nchini Thailand. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua furasa hii kutuma salam zake za rambirambi kwa wote waliofikwa na kutikiswa na msiba huu mzito nchini Thailand. Baba Mtakatifu ili kuonesha uwepo wake wa karibu kwa wale wote walioathirika kwa vitendo hivi vya kikatili na anapenda kuwafariji watoto waliopata majeraha, ili waweze kupona haraka. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi hiki cha majonzi mazito, waathirika wataweza kuchota nguvu na faraja kutoka katika mshikamamano wa udugu wa kibinadamu, ndugu, jamaa na majirani zao wa karibu. Mwishoni, anawaombea amani na kuwapatia baraka zake za kitume.

Jumuiya ya Kimataifa inalaani vikali mauaji ya watoto nchini Thailand
Jumuiya ya Kimataifa inalaani vikali mauaji ya watoto nchini Thailand

Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF limesikitishwa sana na mauaji yaliyofanywa kwenye Kituo cha malezi ya watoto wadogo, huko Non Bua Lamphu, Kaskazini mwa Thailand. Watoto wengi wameuwawa kwa kuchomwa kisu, kielelezo cha ukatili wa hali ya juu kabisa dhidi ya watoto wadogo. UNICEF inalaani na kushutumu vikali kitendo hiki cha: unyanyasaji, unyama na ukatili wa hali ya juu kabisa dhidi ya watoto wadogo. Hakuna mtoto anayepaswa kuwa mlengwa au shuhuda wa unyanyasi na ukatili wakati wowote na mahali popote pale. Vituo vya kulelea watoto na maeneo ya shule yanapaswa kuwa ni salama kwa ajili ya watoto: kujifunza, kucheza na kukua katika kipindi hiki muhimu sana katika safari ya maisha yao. UNICEF inapenda kutumia fursa hii pia kutuma salam za rambirambi kwa wazazi waliowapoteza watoto wao na wale waliopatwa na majeraha. UNICEF inaungana na watu wa Mungu nchini Thailand kuwaombolezea watoto waliouwawa kikatili.

Mauaji Thailand
07 October 2022, 14:36