Tafuta

Mapigano makali kati ya washabiki wa mpira huko Indonesia ulisababisha vifo na majeruhi. Mapigano makali kati ya washabiki wa mpira huko Indonesia ulisababisha vifo na majeruhi. 

Papa amekumbuka waathirika wa Indonesia na kimbunga huko Cuba&Florida!

Baada ya sala ya Malaika wa Bwana Dominika Oktoba 2,Papa Francisko aliwakumbuka waathirika wa kimbunga kilichopiga kwanza kisiwa cha Cuba na baadaye Florida,Marekani,kwa maana hiyo amewakikishia maombi yake pia kwa ajili ya marehemu na majeruhi katika uwanja wa michezo wa Mpira wa Malang nchini Indonesia.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 2 Oktoba 2022 kwa waamini na mahujaji waliofika katika uwanja wa Mtakatifu Petro, jijini Vatican, ameonesha ukaribu kwa watu wa Kisiwa kikubwa cha Cuba na Florida nchini Marekani  ambao  wamepata pigo kubwa na kimbunga kikali. Papa amesema Mungu awapokee wahanga, awape faraja na matumaini wale wanaoteseka na kuunga mkono jitihada ya mshikamano. Baba Mtakatifu akiendelea katika mutadha huo pia amewaombea waliopoteza maisha na kujeruhiwa katika mapigano yaliyozuka mara baada ya mechi ya mpira wa miguu huko Malang nchini Indonesia.

Kimbunga kikali huko Floria na Cuba
Kimbunga kikali huko Floria na Cuba

Sura ya Mtakatifu Petro na utume wake

Papa Francisko amewajulisha kuwa usiku  wa tarehe 2 Oktoba, katika ukuta wa mbele ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro wataoneshwa kazi moja kwa sauti na picha juu ya sura ya Mtakatifu Petro. Maonesho hayo yatarudiwa hadi tarehe 16 Oktoba 2022 kila jioni kuanzia saa 3 usiku hadi saa 5 usiku. Papa Francisko amewashukuru wote walioanzisha na kufanikisha kazi hiyo na ambayo inazindua mchakato wa kichungaji unaojikita juu ya Sura ya Mtakatifu Petro na utume wake.

Mbele ya Mtakatifu Petro Yatafanyika maonesho ya Nifuate kuhusu sura ya Mtakatifu Petro 2-16 Oktoba kila saa 3 hadi 5 usiku
Mbele ya Mtakatifu Petro Yatafanyika maonesho ya Nifuate kuhusu sura ya Mtakatifu Petro 2-16 Oktoba kila saa 3 hadi 5 usiku

Hatimaye amewasalimia warumi na mahujaji kutoka pande za dunia kama vile familia nyingi, makundi ya parokia na vyama. Kwa namna ya pekee amewasalimia kundi kutoka majimbo ya Nanterre (Ufaransa) na Utume katoliki wa Italia wa Karlsruhe huko (Ujerumani). Waamini wa Cordenons, Corbetta, Arcade Povegliano, Formia, Grumo Appula na Cagliari. Kwa wote amewatakia Dominika njema na kuwaomba wasisahau kusali kwa ajili yake.

Papa amekumbuka wathirika wa kimbunga Florida na Cuba na waathirika wa mapigano Indonesia
02 Oktoba 2022, 13:06