Nia za Papa Francisko Kwa Mwezi Oktoba 2020: Umisionari na Sinodi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mama Kanisa katika kipindi cha Mwezi wa Oktoba anapenda kuwahamasisha waamini kushiriki kikamilifu katika shughuli za kimisionari pamoja na kuchangia kwa hali na mali, mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Waamini wasali zaidi, wajifunze kudumisha ukimya ndani mwao, ili kukutana na Kristo Yesu, anayewakirimia waja wake njia na mbinu za kuwa waaminifu katika wito wao kama mitume wamisionari. Huu ni mwamko na ushuhuda wa kimisionari kama kielelezo cha imani tendaji na mapendo kamili kwa Mungu na jirani zao. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 96 ya Kimisionari Ulimwenguni, Jumapili tarehe 23 Oktoba 2022 unanogeshwa na kauli mbiu: “Mtakuwa mashahidi wangu” (Mdo 1:8). Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi katika ngazi ya Kimabara ni kuanzia mwezi Septemba 2022 hadi kabla ya tarehe 31 Machi 2023. Katika awamu hii, Mama Kanisa anapenda kukazia kwa namna ya pekee ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza pamoja na kukuza utambuzi wa watu watakatifu wa Mungu kutoka katika Makanisa mahalia. Hiki ni kipindi cha kukuza na kudumisha utambuzi wa watu waliochaguliwa kuwakilisha Makanisa mahalia katika maadhimisho ya ngazi ya Kimabara. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, litaadhimisha Sinodi kwa Kanisa la Bara la Afrika kuanzia tarehe 1 hadi 7 Machi 2023 huko mjini Addis Ababa, nchini Ethiopia.
Awamu ya Pili ni muhimu sana katika mchakato wa utambuzi wa dhana ya Sinodi, jinsi ambavyo Kanisa linatembea katika umoja sanjari na kupembua vipaumbele vya Makanisa mahalia, ili hatimaye, kuweza kupata mang’amuzi ya pamoja na kuendelea kuimarisha mafungamano na mshikamano wa udugu kati ya watu wa Mungu. Mama Kanisa anatambua fika kwamba kuna: shida, changamoto na mivutano inayosimikwa katika tamaduni pamoja na historia za watu mahalia. Lengo ni kuendeleza mchakato wa ujenzi wa mshikamano na mafungamano ya watu wa Mungu wanaounda Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika Nia zake za Jumla kwa Mwezi Oktoba 2022, katika ujumbe wake kwa njia ya video, inayosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, anawaalika waamini kusali kwa ajili ya Kanisa, aminifu na jasiri daima katika kutangaza na kushuhudia Injili. Lengo ni kuliwezesha Kanisa kuwa ni Jumuiya ya mshikamano na mafungamano ya dhati; udugu wa kibinadamu na ukarimu. Kanisa lijitahidi kuishi daima katika mazingira ya Kisinodi, yaani kwa kutembea pamoja. Hii ndiyo maana halisi ya Neno Sinodi.
Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, anatarajia kuona ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Hili ni Kanisa linalosimikwa katika utamaduni wa kusikiliza na kusikilizana; ujenzi wa umoja katika utofauti wake. Ni ujenzi wa Kanisa lenye ukarimu, kwa kuwakaribisha wale walioko nje, kuweza kuingia ndani na hivyo kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu anaonya kwamba, Sinodi si “Bunge” linalokusanya maoni ya wananchi. Maadhimisho ya Sinodi ni wakati muafaka wa kumsikiliza kwa makini Roho Mtakatifu ambaye ndiye mhimili mkuu wa Uinjilishaji anataka kuliambia nini Kanisa. Hiki ni kipindi cha sala, kwani bila sala na maombi Sinodi si mali kitu! Sinodi ni mchakato wa ujenzi na ushuhuda wa uwepo angavu wa Mungu katika maisha ya waja wake. Huu ni ukaribu unaoshuhudiwa na maaskofu, mapadre pamoja na watu wote wa Mungu. Mama Kanisa akiwa mwaminifu kwa Injili, daima ataweza kuwa na ujasiri katika kuitangaza na kuihubiri sanjari na ujenzi wa mshikamano, udugu na ukaribu. Huu ni mwaliko wa kuwa ni mahujaji wa upendo na Injili, tayari kujiweka wazi kwa ajili ya mshangao wa Roho Mtakatifu. Maadhimisho ya Sinodi ni fursa zinazokuja baada ya watu wa Mungu kukutana, kusikilizana na kufanya utambuzi wa pamoja.