Mwenyeheri Benigna Cardoso Da Silva: Shuhuda Dhidi ya Nyanyaso za Kijinsia na Ukatili kwa Watoto
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mwenyeheri Benigna Cardoso da Silva (15 Oktoba 1928 - 24 Oktoba 1941) alikuwa mtoto Mkatoliki kutoka nchini Brazil. Katika utoto wake alilelewa kama mtoto yatima kufuatia vifo vya wazazi wake, na alijulikana kwa kujisadaka sana kwa kazi za nyumbani na huduma kwa wazee waliokuwa wanamtunza pamoja na kuhudhuria Ibada ya Misa Takatifu mara kwa mara. Lakini alijulikana na kupata umaarufu zaidi kwa kuuawa baada ya kukataa matamanio ya kingono ya Raimundo Alves Riberio, ambaye alikuwa karibu na umri wake, ili kulinda ubikira na usafi wake wa moyo. Alisimama kidete na kujitetea kwa nguvu zake zote, lakini Riberio akamuua kikatili sana tarehe 24 Oktoba 1941, akiwa na umri wa miaka 13 tu. Raimundo Alves Riberio alitiwa pingu na vyombo vya ulinzi na usalama, akapatikana na kosa la mauaji na kufungwa kwenye Gereza la Watoto Wadogo huko Fortaleza. Baada ya kumaliza kifungo chake, miaka hamsini baadaye, akatembelea eneo la mauaji na kutubu makosa yake. Kutokana na sababu na ukatili ulioneshwa kwenye mauaji ya Benigna Cardoso da Silva, waamini wengi walivutwa na ujasiri pamoja na ushuhuda wa msichana huyu, kiasi kwamba, eneo hili likageuka na kuwa ni mahali pa hija, toba na wongofu wa ndani. Mchakato wa kumtangaza Benigna Cardoso da Silva kuwa ni Mwenyeheri ulizinduliwa kunako mwaka 2013 na tarehe 24 Oktoba 2022 atangazwa kuwa ni Mwenyeheri. Hii ni Ibada ambayo imeongozwa na Kardinali Leonardo Steiner, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manaus, nchini Brazil, kama Mwakilishi wa Baba Mtakatifu Francisko. Huyu ni Mwenyeheri wa kwanza kutangazwa rasmi na Kanisa kutoka katika eneo la Crato, Mkoa wa Cearà, Kusini Mashariki wa Brazil.
Mwenyeheri Benigna Cardoso da Silva “Benigna” maana yake ni mtu aliyezaliwa vizuri” ni kati ya watoto mashuhuda wa imani wanaoendelea kusadaka maisha yao kutokana na vitendo mbalimbali vya kikatili dhidi ya utu, heshima na haki zao msingi. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 26 Oktoba 2022 amemtaja Mwenyeheri Benigna Cardoso da Silva kuwa ni shuhuda kijana aliyesimika maisha yake katika Neno la Mungu; akalinda ubikira na usafi wake wa moyo; akasimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima yake kama kijana. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mwenyeheri Benigna Cardoso da Silva, awasaidie na kuwaombea waamini ili waweze kuwa ni wafuasi wakarimu wa Kristo Yesu katika maisha yao. Wawe kweli ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili sehemu mbalimbali za dunia. Kardinali Leonardo Steiner, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manaus, katika mahubiri yake, amemtaja Mwenyeheri Benigna Cardoso da Silva kuwa ni kielelezo makini dhidi ya nyanyaso na dhuluma kwa watoto na vijana. Jamii inapaswa kusimama kidete kulinda: utu, heshima na haki msingi za watoto na vijana dhidi ya nyanyaso na dhuluma mbalimbali. Ni Mwenyeheri aliyethubutu kutangaza na kushuhudia upendo wake katika kifo; upendo ambao umesimikwa katika uaminifu, ukweli na usafi kamili. Ni upendo ambao umeonesha nguvu dhidi chuki na uhasama.
Hii ni amana na utajiri mkubwa unaojikita katika katika nguvu, kiasi na uaminifu mbele ya nyanyaso za kijinsia na vurugu ya maisha. Ni kielelezo cha amana ya imani inayohifadhiwa katika upendo na hivyo kuwa ni chemchemi ya utakatifu wa maisha. Leo hii bado ukatili na nyanyaso za kijinsia zinaendelea kusikika sehemu mbalimbali za dunia. Kuna vipigo na mauaji ya wanawake, mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuanza safari ya maisha ya kiroho katika Kristo Yesu, na hivyo kuendelea kuwa ni mashuhuda na watangazaji wa furaha ya Injili; kwa kukimbilia ulinzi na tunza katika Kristo Yesu, ili kupata maisha angavu na matumaini. Mwenyeheri Benigna Cardoso da Silva ni chemchemi na mfano wa kuigwa katika mchakato wa toba, wongofu wa ndani na upatanisho kama ilivyokuwa kwa Raimundo Alves Riberio baada ya miaka 50 akapata nafasi ya kutubu na kumwongokea Mungu. Mwenyeheri Benigna Cardoso da Silva ni mfano bora wa kuigwa na wanawake wote katika kusimamia utu, heshima na haki zao msingi, ili kuonesha kwamba, tendo la ndoa linaheshima yake. Vijana wajifunze kusimika maisha yao katika Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Jamii ijifunze kuwathamini, kuwatunza na kuwahudumia wazee kwa moyo wa huruma na upendo. Hii ni changamoto kwa jamii kuhakikisha kwamba, inaunda mazingira yatakayosimamia utu, heshima na haki msingi za binadamu.