Tafuta

Mahujaji wa Kisalesian tarehe 8 Oktoba 2022 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu kama sehemu ya mkesha wa kutangazwa Mwenyeheri Artemide Zatti kuwa Mtakatifu. Mahujaji wa Kisalesian tarehe 8 Oktoba 2022 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu kama sehemu ya mkesha wa kutangazwa Mwenyeheri Artemide Zatti kuwa Mtakatifu. 

Mtakatifu Artemide Zatti: Baba wa Wahamiaji; Ndugu ya Wagonjwa na Maskini; Mwombezi wa Miito

Mtakatifu Artemide Zatti ni Baba wa wakimbizi na wahamiaji; ndugu na jamaa ya maskini na wagonjwa, Bruda na mmisionari mahiri wa Wasalesian wa Don Bosco na mwombezi wa miito mbalimbali ndani ya Kanisa Licha ya changamoto na matatizo ya wakimbizi wa wakati ule, familia iliendelea kusimama kidete katika: Imani, Sala, Sakramenti, Neno la Mungu na Upendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mahujaji wa Kisalesian kutoka sehemu mbalimbali za dunia, Jumamosi tarehe 8 Oktoba 2022 walikutanika mjini Vatican, ili kumshukuru na kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa wema na huruma yake ya daima, iliyomwezesha Mwenyeheri Artemide Zatti hatimaye, kutangazwa kuwa ni Mtakatifu. Mtakatifu Artemide Zatti, Bruda wa Shirika la Wasalesian wa Don Bosco alizaliwa tarehe 12 Oktoba 1880, nchini Italia. Akafariki dunia tarehe 15 Machi 1951 huko Viedma nchini Argentina. Utakatifu wake unapata chimbuko lake katika huduma kwa maskini kwa kuongoza hospitali na duka la dawa kwa ajili ya maskini kwa muda wa miaka 40. Tarehe 14 Aprili 2002 atakatangzwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa ni Mwenyeheri na hatimaye, tarehe 9 Oktoba 2022 anatangazwa kuwa Mtakatifu. Hili ni tukio ambalo limeadhimishwa kwa kishindo, kwa tafakari makini kuhusu historia ya maisha ya Mtakatifu Artemide Zatti. Hii ni changamoto kwa waamini na watu wote wanaofanya kazi katika sekta ya afya kutekeleza vyema wajibu wao kwa kuheshimu utu wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu sanjari na kuzingatia haki zake msingi.

Mtakatifu Zatti Baba wa Wakimbizi, Ndugu ya wagonjwa na mwombezi wa miito
Mtakatifu Zatti Baba wa Wakimbizi, Ndugu ya wagonjwa na mwombezi wa miito

Kanisa kama Mama na Mwalimu anawakumbusha watoto wake kuwa wakarimu na watu wenye upendo kwa wagonjwa. Wawe mstari wa mbele katika kuwajali na kuwatunza wagonjwa wanaohitaji kuonjeshwa utaalam na weledi; upole, unyoofu na unyenyekevu, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza, ili wagonjwa waweze kutambua kwamba, wanapendwa na kuthaminiwa kama alivyojitahidi kufanya Mtakatifu Artemide Zatti katika maisha na utume wake. Baba Mtakatifu Francisko anaonya kwamba, maisha ya binadamu kamwe hayawezi kubinafsishwa hasa kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi ya tiba ya mwanadamu na teknolojia inayotoa kishawishi cha watu kutaka kuchezea uhai wa binadamu! Anawataka waamini pamoja na wadau mbalimbali kumwilisha ndani mwao, mfano wa Msamaria mwema, ili kuwaganga kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini, wale wote wanaoteseka, wanaosumbuliwa na kunyanyasika kutokana na magonjwa: kiroho na kimwili.

Mtakatifu Zatti ni mwombezi wa miito ndani ya Kanisa
Mtakatifu Zatti ni mwombezi wa miito ndani ya Kanisa

Mahujaji pia wamesali na kuombea miito mitakatifu ndani ya Familia kubwa ya Wasalesiani, ili waweze kupata vijana wengi wanaojisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wagonjwa, sehemu mbalimbali za dunia. Wametafakari miujiza iliyotendwa na Mtakatifu Artemide Zatti kielelezo makini cha wito wa huduma inayosimikwa katika upendo. Alijitanabaisha kuwa ni ndugu ya maskini, akawasaidia kubeba mzigo wa gharama ya matibabu, wale waliokuwa na changamoto za kiuchumi. Kwa hakika alikuwa ni mtu mwema kwa wote, chachu ya Injili ya huruma na mapendo na leo hii kuna umati mkubwa wa watu wateule wa Mungu wanaomshukuru kwa huduma yake kwa wagonjwa na ndugu zao, leo hii amekuwa ni Mtakatifu mfano bora wa kuigwa na wengine. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amemwelezea Mtakatifu Artemide Zatti kuwa ni Baba wa wakimbizi na wahamiaji; ndugu na jamaa ya maskini na wagonjwa, Bruda na mmisionari mahiri wa Wasalesian wa Don Bosco na mwombezi wa miito mbalimbali ndani ya Kanisa.

Ni Mlinzi wa wakimbizi na wahamiaji; wagonjwa na maskini
Ni Mlinzi wa wakimbizi na wahamiaji; wagonjwa na maskini

Wazazi wa Mtakatifu Artemide Zatti kunako mwaka 1875 walihamia nchini Argentina, licha ya changamoto na matatizo ya wakimbizi wa wakati ule, familia iliendelea kusimama kidete katika imani na maisha ya Kikristo yaliyosimikwa katika: Sala na Sakramenti, mazingira yaliyochangia wito wake wa Kitawa ndani ya Shirika la Wasalesian wa Don Bosco. Mtakatifu Artemide Zatti alikuwa ni ndugu na jamaa ya maskini na wagonjwa, kiasi cha kuwawezesha wagonjwa kutambua kwamba, hii ilikuwa ni fursa ya kuonja wokovu wa Mungu. Akawa ni Msamaria mwema kwa wagonjwa na ndugu zao, huku akijitahidi kumwilisha Amri kuu ya upendo kwa Mungu na jirani. Alipyaisha maisha yake katika sala, Ibada ya Misa Takatifu, Sakramenti za Kanisa, Tafakari ya kina ya Neno la Mungu sanjari na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, akawa ni chachu na mfano bora wa kuigwa na wengine. Alikuwa ni Bruda wa Kisalesiani aliyejiaminisha kwa Bikira Maria Msaada wa Wakristo, kiasi cha kuaminisha kwake, akajiwekea ahadi ya kuwasaidia jirani zake, kiasi kwamba, Mwenyezi Mungu alisikiza kilio chake na kumponya na magonjwa yake yaliyokuwa yanamwandama katika maisha. Kwa hakika anasema Baba Mtakatifu Mtakatifu Artemide Zatti ni mwombezi wa miito mbalimbali ndani ya Kanisa.

Mtakatifu Zatti

 

 

 

08 October 2022, 14:15