Mkutano Mkuu wa 26 wa Shirika la Mkombozi Mtakatifu Sana: Karama
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Shirika la Mkombozi Mtakatifu sana; C.SS.R., “Congregatio Sanctissimi Redemptoris” Kwa Umombo “The Congregation of the Most Holy Redeemer” lilianzishwa rasmi na Mtakatifu Alfonso Maria wa Liguori hapo tarehe 9 Novemba 1732, huko Amalfi kwa ajili ya kuwainjilisha watu wa Mungu waliokuwa wanaishi vijijini nchini Italia. Shirika lilitambuliwa rasmi na Papa Benedikto XIV kunako mwaka 1749. Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa 26 umemchagua Mheshimiwa Padre Rogèrio Gomes, kuwa mkuu wa Shirika kwa kipindi cha miaka 6 ili kuweza kuliongoza Shirika katika mchakato wa kupambana na matatizo, changamoto na kutumia fursa zinazojitokeza kwa ajili ya kumtangaza na kumshuhudi kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Shirika lina wanachama 4, 617 wanaotekeleza dhamana na utume wao katika nchi 85 sehemu mbalimbali za dunia. Mkutano mkuu wa 26 wa Shirika umenogeshwa na kauli mbiu “Tazama, nayafanya yote kuwa mapya.” Ufu 21:5, huu ni mwaliko wa kuishi na kumwilisha Pentekoste, inayoyafanya yote kuwa mapya, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu “Kerygma” hadi miisho ya dunia. Huu umekuwa ni wakati wa kutafakari na kufanya upembuzi yakinifu kuhusu: Utambulisho na Utume wa Shirika; Maisha ya wakfu, malezi, majiundo na uongozi, ili kuiwezesha karama ya Shirika kusoma alama za nyakati na hivyo kutoa huduma makini kwa watu watakatifu wa Mungu, daima wakiwa wanazingatia Mamlaka fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium.”
Hii ni dhamana inayopaswa kutekelezwa kwa mwanga wa Mapokeo hai ya Kanisa kwa kutambua kwamba, Shirika lina amana na utajiri mkubwa wa Taalimungu maadili, tayari kujitoa na kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, daima wakiyainua macho yao kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Wajifunze kutoka kwa Kristo Yesu, Msamaria mwema na Mtumishi wa wote katika maisha na huduma yao kwa watu wa Mungu wanaowahudumia. Hii ni sehemu ya wosia ulitolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 1 Oktoba 2022 alipokutana na kuzungumza na Shirika la Mkombozi Mtakatifu sana “Congregatio Sanctissimi Redemptoris” kama sehemu ya maadhimisho ya Mkutano mkuu wa 26 wa Shirika. Baba Mtakatifu pamoja na mambo mengine, amekazia mchakato wa ubunifu na upyaisho wa karama ya Shirika huku wakiendelea kuwa waaminifu kwa karama ya Shirika lao. Ni wakati wa toba na wongofu wa ndani, ili kusoma alama za nyakati, ili hatimaye, kujibu kwa ufasaha changamoto zinazoibuliwa katika ulimwengu mamboleo, daima wakimsikiliza Roho Mtakatifu katika shughuli zao za kitume. Iwe ni fursa ya kutia divai mpya katika viriba vipya. Rej Mk 2:22.
Watambue kwamba, kiini cha Fumbo la Kristo kinasimikwa katika maisha ya kijumuiya, kama kielelezo makini cha kuendelea kujikita katika upendo, ili kuzaa matunda yanayotarajiwa, yaani kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Huu ni utume, ambao tangu mwanzo wake, umevaliwa njuga na watakatifu, mashuhuda na waungama imani, mwaliko na changamoto ya kuandika historia ya maisha na utume wa Shirika kwa watu wa nyakati hizi. Viongozi wapya waliochaguliwa na wanashirika, wawe ni mfano bora wa kuigwa kwa kutambua kwamba, wao ni watumwa wasiokuwa na faida; wanatekeleza yale wanayopaswa kufanya. Rej. Lk 17:10. Kristo Yesu aliyewaosha miguu Mitume wake, kielelezo cha huduma na upendo, awe ni mfano bora wa kuigwa, huku wakijitahidi kutomezwa na malimwengu, uchoyo na ubinafsi. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu amewaweka wanashirika wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Msaada wa daima, ili aweze kuwalinda na kuwaongoza, daima wakitoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.