Tafuta

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, mwaka 2022 linaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, mwaka 2022 linaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. 

Jubilei ya Miaka 50 ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC

Kongamano la Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC, huko Bangkok, kuanzia tarehe 12 Oktoba hadi 30 Oktoba 2022 linanogeshwa na kauli mbiu “Kutembea pamoja kama watu wa Asia” … na wakaenda zao kwao kwa njia nyingine.” Mt 2:12. Shirikisho hili linaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Papa Francisko amewatumia ujumbe na pongezi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa linamheshimu Bikira Maria Malkia wa Amani na Mama wa Huruma, kwa kumzaa Kristo Yesu, ufunuo wa upendo na huruma ya Mungu kwa waja wake. Bikira Maria amekuwa ni Mwombezi wa daima wa watu wa Mungu mbele ya Kristo Yesu katika shida na mahangaiko yao, huku Bondeni kwenye machozi. Kristo Yesu rehema ya Mungu, aendelee kusikiliza na kujibu sala za waja wake katika umaskini na unyonge wao, awatie nguvu na kuwainua katika roho ya upendo, karama za ujenzi wa umoja na mshikamano wa upendo wa kidugu, ili amani ya kweli iweze kutamalaki katika uso wa dunia. Huu ni ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, kama Mwakilishi wake maalum katika hitimisho la Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC, huko Bangkok, nchini Thailand. Kardinali Tagle anajiunga na Kardinali Charles Maung Bo, S.D.S., Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC., katika maadhimisho haya. Ushiriki wa Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle ni kielelezo cha uwepo na ukaribu wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya. Kardinali Tagle, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Manila, ni kiongozi mwenye uzoefu na mang’amuzi makubwa katika maisha na utume wa Kanisa Barani Asia.

Vijana wa kizazi kipya Barani Asia wapewe kipaumbele katika utume wa Kanisa
Vijana wa kizazi kipya Barani Asia wapewe kipaumbele katika utume wa Kanisa

Baba Mtakatifu anapenda kuonesha furaha yake katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya utume na maisha ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC. Anapenda kumtia nguvu, ili aweze kuwasalimia na kufikisha baraka zake kwa watu wa Mungu Barani Asia. Baba Mtakatifu anamtaka Kardinali Tagle kuwatia shime watu wa Mungu Barani Asia, kwa kutambua kwamba, kwa njia ya upendo wa kimama wa Bikira Maria wanaweza kupata rehema kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Paulo VI tarehe 27 Novemba 1970 kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa alianza Hija ya Kitume ya Siku tatu nchini Ufilippini, kama kielelezo cha mshikamano wa udugu baada ya nchi hiyo kukumbwa na kimbunga kikali sana, kilichopelekea maafa ya watu na mali zao. Hii ilikuwa ni fursa kwa Maaskofu kutoka sehemu mbalimbali za Bara la Asia kukutana na Khalifa wa Mtakatifu Petro aliyekuwa amekuja kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo thabiti. Ni katika muktadha huu, Maaskofu Katoliki Barani Asia wakatia nia ya kuanzisha Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC, ili kujenga na kudumisha umoja na ushirikiano katika kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika maisha na utume wa Kanisa Barani Asia.

Utunzaji bora wa mazingira ni dhamana na wajibu wa watu wote
Utunzaji bora wa mazingira ni dhamana na wajibu wa watu wote

Kumbe, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ambao kwa mwaka 2022 unaadhimisha Miaka 60 tangu ulipofunguliwa rasmi tarehe 11 Oktoba 1962 na Mtakatifu Yohane wa XXIII, changamoto na mwaliko kwa watoto wa Mungu kutangaza na kushuhudia uaminifu wao kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kongamano la Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC, huko Bangkok, kuanzia tarehe 12 Oktoba hadi 30 Oktoba 2022 linanogeshwa na kauli mbiu “Kutembea pamoja kama watu wa Asia” … na wakaenda zao kwao kwa njia nyingine.” Mt 2:12. Shirikisho hili linaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, ingawa kilele rasmi kilikuwa ni mwaka 2020 lakini, kutokana na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 maadhimisho haya yakasogezwa mbele hadi Mwezi Oktoba 2022. Huu ni wakati muafaka wa kutafakari maisha na utume wa Kanisa Barani Asia katika muktadha: vita na kinzani sehemu mbalimbali za dunia; athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi pamoja na madhara yaliyosababishwa na UVIKO-19 bila kusahau jinsi ambavyo baa la njaa na utapiamlo wa kutisha linavyosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu sehemu mbalimbali za dunia.

FABC ni matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican
FABC ni matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican

Huu ni muda muafaka wa kufanya upembuzi yakinifu katika maisha na utume wa Kanisa, ili kufungua na kuandika ukurasa mpya wa utume wa Kanisa kwa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa Kanisa la Kimisionari na Kisinodi kujenga na kudumisha utamaduni wa kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa na kuendelea kujikita katika mchakato wa uinjilishaji na utamadunisho. Lengo ni kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili. Mchakato wa Uinjilishaji mpya unahitaji majiundo makini na endelevu yatakayowasaidia waamini kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo, kwani: ushuhuda, maisha na utume wa Kanisa ni mambo msingi katika kufufua imani ndani na nje ya Bara la Asia. Waamini wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanamwilisha imani katika uhalisia wa maisha yao sanjari na utamadunisho, vinginevyo, wanaweza kujikuta kwamba, imani inaelea katika ombwe pasi na kukita mizizi katika maisha, tamaduni na mila njema za watu husika.

Utamadunisho ni muhimu katika mchakato wa uinjilishaji
Utamadunisho ni muhimu katika mchakato wa uinjilishaji

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa washiriki wa Kongamano la Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC amegusia historia ya Shirikisho hili; umuhimu wa kuwatambua na kuwathamini vijana wa kizazi kipya katika maisha na utume wa Kanisa pamoja na kuendeleza mchakato wa uinjilishaji na utamadunisho kwani Bara la Asia linaundwa na watu wa dini na tamaduni mbalimbali. Ni wakati muafaka wa kusimamia utu, heshima na haki msingi za binadamu kwa njia ya majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Kanisa linawategemea sana maskini katika maisha na utume wake, kwani maskini ni amana na utajiri wa Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kimsingi, maskini ndio walengwa wakuu wa Injili. Dhana ya umaskini inajikita katika umaskini wa hali na mali; maadili na utu wema; kwani wote hawa, Kristo Yesu amejisadaka kwa ajili ya kuwatangazia Habari Njema ya Wokovu. Wakristo wanapaswa kuwajali, kuwathamini na kuwapenda maskini na watu wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama afanyavyo mama mzazi kwa watoto wake.

Maskini ni amana na utajiri wa Kanisa, walengwa wa uinjilishaji mpya.
Maskini ni amana na utajiri wa Kanisa, walengwa wa uinjilishaji mpya.

Kanisa linatoa huduma ya upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa maskini, kwa kujali na kuthamini utu, heshima na haki zao msingi, kwani hata wao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee, anawaalika Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujifunza kutoka kwenye shule ya maskini kwani kati ya maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum, humu humu kuna watakatifu na watu ambao wanaweza kuwafundisha wengine tunu msingi za maisha ya kijamii, kiutu na kiroho. Huu ni wakati wa ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu, ili kusikiliza na kutekeleza sauti ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya Kanisa la Mungu Barani Asia. Hii ni fursa ya kutoa kipaumbele cha kwanza kwa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa, ili kujenga umoja unaosimiwa katika tofauti. Waraka wa Kitume Injili ya Furaha, “Evangelii gaudium” uliochapishwa na Baba Mtakatifu Francisko unatoa kipaumbele cha kwanza kwa furaha ya Injili, kwa kuwaalika waamini kushirikisha furaha yao inayopata chimbuko kutoka katika huruma na upendo wa Mungu kwa wanadamu. Katika mwono huu, Kristo ni kiini cha Injili na kwamba, Kanisa linaalikwa kufanya mageuzi makubwa kama sehemu ya uinjilishaji mpya. Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki na amani kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Hiki ndicho kiini cha Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.”

Umoja, upendo na mshikamano wa kweli ni muhimu katika utume wa Kanisa
Umoja, upendo na mshikamano wa kweli ni muhimu katika utume wa Kanisa

Baba Mtakatifu anapembua kuhusu madhara ya uharibifu wa mazingira, umuhimu wa wongofu wa kiekolojia na teknolojia rafiki kwa mazingira. Anazungumzia kuhusu haki ya maji safi na salama. Mazingira ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, urithi unaopaswa kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu. Utunzaji wa mazingira hauna budi kwenda sanjari na uwajibikaji na wala maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yasitumike kama nguvu ya kiuchumi kwa ajili ya kunyonya Mataifa mengine wala kuyatumbukiza katika utamaduni wa kifo. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”, umetiwa mkwaju tarehe 3 Oktoba 2020 huko mjini Assisi, Italia na kuzinduliwa rasmi tarehe 4 Oktoba 2020 sanjari na Maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi aliyejikita katika: huduma bora kwa maskini, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Udugu na urafiki wa kijamii ni dira na mwongozo wa mchakato wa ujenzi wa ulimwengu ulio bora zaidi na unaosimikwa katika misingi ya haki, amani na utulivu, dhamana na wajibu wa: watu wote pamoja na taasisi mbalimbali. Baba Mtakatifu anapinga kwa nguvu zote vita na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Waraka huu unajikita zaidi katika masuala msingi ya kijamii katika maisha ya mwanadamu.

50 yrs FABC

 

28 October 2022, 17:16