Tafuta

Uzinduzi wa Kituo cha Majadiliano ya Kidini cha Abraham J. Heschel, Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mtakatifu Yohane Paulo II cha Lublin, Poland Uzinduzi wa Kituo cha Majadiliano ya Kidini cha Abraham J. Heschel, Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mtakatifu Yohane Paulo II cha Lublin, Poland 

Majadiliano ya Kidini Kati ya Wayahudi na Wakatoliki: Ustawi, Maendeleo na Mafao ya Wengi

Ni matumaini ya Papa Francisko kwamba, Kituo cha Abraham J. Heschel cha Mahusiano ya Kikatoliki na Kiyahudi katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mtakatifu Yohane Paulo II, Lublin kitasaidia kuboresha na kudumisha mahusiano na mafungamano kati ya Wakatoliki na Wayahudi, kwa kuthamini na kudumisha amana na utajiri wa dini na watu wa Mungu kutoka Israeli na Poland.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Imani, amani na matumaini ni fadhila ambazo zinapata chanzo na utimilifu wake mbele ya Mwenyezi Mungu, lakini binadamu amedhaminishwa tunu hizi ili kuzifanyia kazi katika maisha yake; kwa kuchagua na kuambata mapenzi ya Mungu, ili hatimaye, aweze kusimama kidete kulinda na kudumisha mafao ya wengi. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanahamasishwa kujichotea: hekima, amana na utajiri wa Neno la Mungu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Wayahudi yataweza kuzaa matunda mengi ya ushirikiano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Hija ya pamoja katika majadiliano ya kidini ni muhimu sana kwa ajili ya: Ustawi, maendeleo na mafao ya waamini wa dini hizi mbili, ili kufahamiana, kuheshimiana na kwa pamoja, kuweza kusimama kidete kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu kama sehemu muhimu sana ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu! Huu ni mchakato wa ujenzi wa fadhila ya upendo wa kidugu kati ya watu kwani Mungu ni asili na hitimisho la upendo. Tamko la Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu majadiliano na waamini wa dini mbalimbali duniani, “Nostra aetate” ni msingi wa mahusiano mema ambayo yameendelea kujengeka na kuimarika kama ndugu wamoja kwa kutambua kwamba, hii ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Miaka 60 ya Mtaguso Mkuu wa II wa Vatican: Majadiliano ya Kidini
Miaka 60 ya Mtaguso Mkuu wa II wa Vatican: Majadiliano ya Kidini

Urithi mkubwa ambao waamini wa dini mbalimbali wanaweza kuufanya katika maisha na utume wao ni kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha misingi ya upendo kwa Mungu na jirani. Kizazi baada ya kizazi kinapaswa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu anapaswa kupendwa kwa moyo wote, kwa roho yote na kwa nguvu zote. Upendo huu kimsingi, unapaswa pia kuelekezwa kwa jirani ambaye ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, kumekuwepo na mafanikio makubwa yanayofumbata amana na utajiri wa maisha ya kiroho; uelewa na udugu wa kibinadamu unaopania kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kati ya watu wa Mataifa. Majadiliano ya kidini ni nyenzo muhimu sana katika mapambano dhidi ya chuki na uhasama kwa Wayahudi; kwa kujikita katika mchakato wa kulinda na kudumisha misingi ya amani, kwa kuheshimiana na kuthaminiana. Waamini wa dini mbali mbali wanao wajibu na dhamana ya kulinda uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kukuza na kudumisha uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini pamoja na kujikita katika mchakato wa kutunza mazingira nyumba ya wote! Ikumbukwe kwamba, Wayahudi na Wakristo wanao utajiri na amana ya maisha ya kiroho pamoja na mambo mengi mazuri wanayoweza kushirikiana kwa pamoja kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Ushuhuda wa pamoja katika kutetea Uhai, Utu, Heshima na Haki msingi.
Ushuhuda wa pamoja katika kutetea Uhai, Utu, Heshima na Haki msingi.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 19 Oktoba 2022 amewaalika watu wa Mungu nchini Poland, kutambua historia ya maisha yao na ile ya nchi yao, ili kugundua uwepo angavu na endelevu wa Mungu katika maisha yao. Baba Mtakatifu anapongeza juhudi zilizofanyika za kufungua Kituo cha Abraham J. Heschel cha Mahusiano ya Kikatoliki na Kiyahudi katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mtakatifu Yohane Paulo II, Lublin. Hiki ni kitengo cha kisayansi na kielimu ambacho dhamira yake ni kujenga uhusiano na majadiliano ya kidini kati ya Wakatoliki na Wayahudi katika viwango vya kisayansi, kielimu na kitamaduni katika ngazi ya  Kimataifa. Kituo hiki kinaweka pamoja kazi za utafiti, kuadhimisha historia, kuelimisha na kuwashirikisha vijana wa kizazi kipya pamoja na kuunda ufahamu wa umma kupitia vyombo vya mawasiliano ya kijamii kwa kiwango cha kimataifa. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Kituo cha Abraham J. Heschel cha Mahusiano ya Kikatoliki na Kiyahudi katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mtakatifu Yohane Paulo II, Lublin kitasaidia kuboresha na kudumisha mahusiano na mafungamano kati ya Wakatoliki na Wayahudi, kwa kuthamini na kudumisha amana na utajiri wa dini na watu wa Mungu kutoka Israeli na Poland. Wayahudi na Wakristo wanahamasishwa kusimama kidete kuwalinda maskini, wagonjwa, watoto na wazee, bila kuwasahau wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Majadiliano ya kidini ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi
Majadiliano ya kidini ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi

Huduma kwa binadamu sanjari na majadiliano ya kidini ni mambo msingi ambayo pia vijana wa kizazi kipya wanapaswa kushirikishwa, ili kung’amua mambo mapya katika maisha yao. Changamoto hii inakwenda sanjari na majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya katika misingi ya majadiliano kati ya Wayahudi na Wakristo. Majadiliano ya kidini ni nyenzo msingi katika ujenzi wa amani ya kudumu kati ya waamini wa dini mbalimbali duniani! Kanisa Katoliki litaendelea kudumisha majadiliano ya kidini aa Waamini wa dini ya Kiyahudi, changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ili kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na mafao ya wengi. Kanisa litaendelea kushirikiana na waamini wa dini ya Kiyahudi ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo sanjari na kudumisha misingi ya haki, amani na ushirikiano na kamwe dini zisiwe ni chanzo cha kinzani na maafa kwa watu na mali zao. Haya yalisemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 17 Januari 2016 wakati alipotembelea Hekalu kuu la Waamini wa dini ya Kiyahudi mjini Roma. Baba Mtakatifu Francisko amekuwa ni Papa wa tatu kutembelea Hekalu kuu la Kiyahudi mjini Roma: Papa wa kwa kwanza alikuwa ni Mtakatifu Yohane Paulo II na baadaye Papa mstaafu Benedikto wa kumi na sita. Baba Mtakatifu Francisko anasema, majadiliano ya kidini yamekuwa kwake ni sehemu ya maisha na utume; mambo ambayo yamemsaidia kujenga na kudumisha urafiki na ushirikiano; kwani Wakristo na Wayahudi wanayo mambo mengi yanayowaunganisha pamoja hivyo, wanapaswa kujisikia kuwa ni ndugu wamoja. Hii inatokana na ukweli kwamba, wanao utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho unaopaswa kuendelezwa na kudumishwa na waamini wa pande hizi mbili.

Majadiliano ya kidini ni changamoto ya Mababa wa Mtagusso mkuu Vat.II
Majadiliano ya kidini ni changamoto ya Mababa wa Mtagusso mkuu Vat.II

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, Wayahudi na Wakristo ni ndugu katika imani na wanaunda familia ya Mungu ambaye anawasindikiza na kuwalinda watu wake. Kama waamini, wote kwa pamoja wanahimizwa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa Jiji la Roma, kila upande ukijitahidi kuchangia hasa zaidi katika tunu msingi za maisha ya kiroho, ili kutoa jibu makini kwa changamoto zinazojitokeza kwa wakati huu. Ni matumaini ya Kanisa Katoliki kwamba, majadiliano ya kidini yataendelea kukuzwa na kudumishwa; kwa kuheshimiana na kuthaminiana.  Baba Mtakatifu anakaza kusema, hivi karibuni, Kanisa Katoliki limeadhimisha kumbukizi la Miaka 60 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipotoa Tamko kuhusu majadiliano ya kidini, “Nostra aetate”; fursa makini ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani aliyewezesha kuwepo kwa mabadiliko ya mahusiano kati ya waamini wa dini hizi mbili. Hali ya kutothaminiana imetoweka na sasa waamini wa dini hizi mbili wanashirikiana. Hali ya kuangaliana kama maadui imefutika na kwa sasa waamini wanajisikia kuwa ni marafiki na ndugu wenye asili na urithi mmoja wa maisha ya kiroho. Kwa mara ya kwanza katika historia, Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walifafanua na kubainisha uhusiano kati ya Wakristo na Wayahudi, ingawa hawakuweza kutatua changamoto za kitaalimungu zilizopo, lakini imekuwa ni fursa ya kujenga majadiliano kwa siku za usoni.

Kunako tarehe 10 Desemba 2015, Tume ya Kipapa ya mahusiano na Wayahudi imechapisha Waraka mpya unaojishughulisha na majadiliano ya kitaalimungu yaliyojitokeza katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni tangu kuchapishwa kwa Tamko la Majadiliano ya kidini na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Baba Mtakatifu Francisko alitumia fursa hii kuhimiza mchakato wa majadiliano ya kidini kati ya Wakatoliki na Wayahudi, huku wakijikita katika mang’amuzi na udumifu, kwani Wayahudi na Wakatoliki wanayo mambo mengi yanayowaunganisha. Hata kama Kanisa linaungama kuhusu wokovu ulioletwa kwa njia ya imani kwa Yesu Kristo, lakini pia linatambua uwepo wa Agano la Kale; upendo endelevu wa Mwenyezi Mungu na uaminifu wake kwa Israeli. Baba Mtakatifu anawaalika waamini wa dini ya Kiyahudi kushirikiana na Kanisa katika kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu mamboleo, hususan katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kuna kinzani, vita, mauaji na ukosefu wa haki msingi za binadamu; mambo ambayo yanaacha madonda makubwa katika maisha ya binadamu. Haya ni mambo ambayo kimsingi yanapingana na mafundisho ya dini zinazoungama imani kwa Mungu mmoja. Maisha ni matakatifu na zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Majadiliano ya kidini ni changamoto pevu inayopaswa kuvaliwa njuga
Majadiliano ya kidini ni changamoto pevu inayopaswa kuvaliwa njuga

Amri ya tano ya Mungu inakataza kuua, kwani Mungu ni asili ya maisha, changamoto kwa waamini kusimama kidete ili kulinda na kudumisha uhai wa mwanadamu. Kila mwanadamu analindwa na kuongozwa na mkono wa huruma ya Mungu, hususan watu wenye shida zaidi. Hawa ni maskini, wagonjwa na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ikumbukwe kwamba, Mungu ni upendo na chemchemi ya uhai, kumbe, mauaji au kifo havina sauti ya mwisho. Waamini wanapaswa kuendelea kumwomba Mwenyezi Mungu ili awasaidie kumwilisha mantiki ya amani, upatanisho, msamaha na maisha sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, katika historia, Wayahudi wamekumbana na nyanyaso pamoja na dhuluma, kiasi hata cha kukumbana na mauaji ya kimbari wakati wa Shoah. Waamini millioni sita walipoteza maisha yao kwa vile tu walikuwa ni Wayahudi. Haya ni matokeo ya sera zilizotaka mwanadamu kuchukua nafasi ya Mungu. Tarehe 16 Oktoba 1943 zaidi ya waamini elfu moja walipelekwa uhamishoni kutoka Roma kwenda kwenye kambi ya mateso ya Auschwitz. Wote hawa wamekumbukwa na Baba Mtakatifu wakati wa hija yake kwenye Hekalu kuu la waamini wa dini ya Kiyahudi mjini Roma. Historia iliyopita isaidie kuboresha hali ya siku za usoni; tayari kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu wa mwanadamu sanjari na amani. Baba Mtakatifu amewakumbuka wahanga wa Shoah ambao bado wako hai hadi wakati huu. Baba Mtakatifu Francisko, mwishoni amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa yale yote aliyowawezesha kufanya katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita, kwani maelewano, umoja, udugu na urafiki vimekuwa zaidi. Amekumbusha kwamba, Mwenyezi Mungu amewawekea mbele yao wokovu, kumbe wanapaswa kuwa ni watu wa matumaini. Baba Mtakatifu amewapatia wote baraka na amani.

Majadiliano ya kidini
19 October 2022, 13:30