Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025: Mwaka wa Kwanza: Nyaraka
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anasema, Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ilikuwa ni Pentekoste mpya kwa Kanisa Katoliki, kwa kutaka kusoma alama za nyakati, kusahihisha mapungufu yake, ili hatimaye, kuliwezesha Kanisa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kumletea mwanadamu maendeleo endelevu ya: kiroho na kimwili. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, lilikuwa ni tukio la matumaini ndani ya Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, wakatambua dhamana, wajibu na changamoto iliyokuwa mbele yao, wakaamua kujadili vipengele mbalimbali na hatimaye, kuvipigia kura. Ni Mtaguso uliowakusanya viongozi kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kujadili maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, chini ya uongozi na usimamizi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, wakati huo akiwa ni Mtakatifu Yohane XXIII; Ukatafsiriwa kwa vitendo na Mtakatifu Paulo VI pamoja na Mtakatifu Yohane Paulo II. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akapyaisha mafundisho yake kwa Katekesi makini kuhusu: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na Sala. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kujipambanua kwa kutaka ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu ili kuchangia katika maisha na utume wa Kanisa la Kristo Yesu kila mmoja kadiri ya karama, wito na dhamana yake ndani ya Kanisa.
Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Miaka 60 tangu kuzinduliwa kwa Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican tarehe 11 Oktoba 1962, katika mahubiri yake, amekazia kuhusu upendo ambao Kristo Yesu ameonesha kwa Kanisa lake, licha ya dhambi, udhaifu na mapungufu ya kibinadamu n ahata wakati mwingine, kumezwa na malimwengu, changamoto na mwaliko kwa Kanisa kurejea tena katika chemchemi ya upendo ule wa awali ulioneshwa na Kristo Yesu kwa Kanisa lake: Moja, takatifu, katoliki na la mitume. Hili ni Kanisa linalotumwa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili inayomwilishwa katika imani tendani. Kanisa katika upendo, unyenyekevu na sadaka, linakabidhiwa utume wa kutangaza na kushuhudia Ufalme wa Kristo na wa Mungu; kutangaza Habari Njema ya Wokovu sanjari na utamadunisho, ili kushiriki: furaha na matumaini; uchungu na fadhaa ya walimwengu.
Baba Mtakatifu amekazia ushiriki mkamilifu wa ukuhani wa waamini wote unaowawezesha kushiriki sadaka ya Ekaristi Takatifu, kwa kupokea Sakramenti za Kanisa, kwa kusali na kwa njia ya ushuhuda wa maisha matakatifu, toba, wongofu wa ndani, kwa kujikana na kwa upendo wenye utendaji; Umoja wa watu wa Mungu ukipewa kipaumbele cha kwanza. Kanisa litambue kwamba, maskini wanao upendeleo wa pekee mbele ya Mwenyezi Mungu. Kanisa ni Sakramenti ya umoja inayowaunganisha watu kiundani na Mwenyezi Mungu na hivyo kuleta umoja kati ya wanadamu wote. Ni jukumu la Mama Kanisa kuendelea kujikita katika Mapokeo, sera na mikakati ya shughuli za kiuchungaji. Mwaliko wa kuendeleza majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Ni mwaliko wa kujenga na kudumisha ushirika wa Kanisa, ili wote wawe na umoja kama Kristo Yesu alivyojisadaka kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Maadhimisho ya kumbukizi ya Miaka 60 tangu kuzinduliwa kwa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican imekuwa ni fursa ya maandalizi ya Mwaka wa kwanza wa Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025. Hiki ni kipindi cha Kanisa kujikita zaidi katika Nyaraka Kuu 4 za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican yaani: “Dei verbum” yaani “Ufunuo wa Kimungu”, “Sacrosanctum concilium” yaani “Juu ya Liturujia”; “Lumen gentium” yaani “Fumbo la Kanisa” pamoja na “Gaudium et spes” yaani “Kanisa katika ulimwengu mamboleo.”