Tafuta

Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Pio XI alipoanzisha Utume wa Bahari, “Stella Maris” sanjari na kongamano la 25 la Utume wa Bahari Kimataifa. Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Pio XI alipoanzisha Utume wa Bahari, “Stella Maris” sanjari na kongamano la 25 la Utume wa Bahari Kimataifa. 

Jubilei ya Miaka 100 ya Utume na Maisha; na Kongamano la 25 la Utume wa Bahari 2022

Papa anapenda kuungana na wajumbe wa Utume wa Bahari, kumwimbia Mungu utenzi wa shukrani kwa mafanikio makubwa yaliyokwisha kupatikana katika kipindi cha miaka 100 iliyopita, kama sehemu ya mchakato wa utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu kwa kutambua kwamba, Mitume wa kwanza wa Kristo Yesu walikuwa ni wavuvi kutoka Galilaya. Rej Mt 4:19.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Pio XI alipoanzisha Utume wa Bahari, “Stella Maris” sanjari na Kongamano la 25 la Utume wa Bahari kuanzia tarehe 2-5 Oktoba 2022 huko mjini Glasgow, nchini Scotland. Maadhimisho haya yananogeshwa na kauli mbiu “Baada ya dhoruba, kuna haja ya kusonga mbele kwa ajili ya huduma kwa watakatifu wa Mungu Baharini.” Katika kipindi cha miaka 100 iliyopita kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika Utume wa Bahari na kwa Mama Kanisa kuendelea kusoma alama za nyakati, tayari kusikiliza na kujibu kilio cha mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao zinazoteseka na kunyanyasika kutokana na utume wao baharini! Pamoja na mambo mengine, Utume wa Bahari umeendelea kujizatiti ili kuhakikisha kwamba, mabaharia na wavuvi ambao wanajisadaka usiku na mchana ili kuchangia katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi wanapata pia fursa ya kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko anasema Mama Kanisa anapenda kutafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini! Papa Pio XI alitamani sana kuona kwamba, Utume wa Bahari unaendelezwa kwenye Bahari na fukwe mbalimbali za dunia. Roho Mtakatifu na kwa maombezi ya Bikira Maria aendelee kupyaisha utume na huduma hii mintarafu mahitaji ya watu wa Mungu katika ulimwengu mamboleo.

Neno Mpya ya Utume wa Bahari 2022
Neno Mpya ya Utume wa Bahari 2022

Huu ni utume ulioasisiwa na waamini walei ndani ya Kanisa kama sehemu ya mchango wao wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa tunu za Kiinjili. Ilikuwa ni tarehe 17 Aprili 1922 Papa Pio XI alipoidhinisha Utume wa Bahari. Leo hii kuna umati mkubwa wa Mapadre wanaowahudumia mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao. Kuna jeshi kubwa la watu wanaojitolea zaidi kuwahudumia mabaharia na wavuvi katika bandari 400 kwa kutembelea meli zisizopungua 70,000 kwa mwaka katika nchi ya zaidi ya 50. Mama Kanisa anawashukuru kwa dhati Mitume hawa wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma makini kwa mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao. Wamekuwa ni mashuhuda na vyombo vya uinjilishaji, kwa kuwafunulia watu sura pendelevu ya Mama Kanisa kwa kuonesha ukaribu wake kwa watu wa Mungu na hivyo kuwahamasisha kujisikia kuwa ni sehemu hai ya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Miaka 100 iliyopita, kimekuwa ni kipindi cha ujenzi wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni kutokana na mwingiliano wa watu kutoka katika dini, tamaduni na mataifa mbalimbali. Kumekuwepo na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia katika ulimwengu wa Utume wa Bahari. Lakini vitendo vya kiharamia, uhalifu wa magenge, tatizo la kutua nanga mbali na bandari, kutengwa na kutelekezwa na kwa sasa athari za janga Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 limepelekea wavuvi na mabaharia kukumbwa na ogonjwa wa Sonona.

Utume wa Bahari unatimiza miaka 100
Utume wa Bahari unatimiza miaka 100

Kanisa katika kipindi hiki pia limejitahidi kusoma alama za nyakati, kwa kusikiliza na kujibu kilio cha wavuvi, mabaharia na familia zao. Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 ya Utume wa Bahari, nembo imebadilishwa, ili kutoa utambulisho wa Utume wa Bahari kama nanga ya matumaini, kielelezo cha imani, wokovu na upendo kwa wote. Mwanga wa Kristo unafyekelea mbali ukosefu wa haki, dhuluma na nyanyaso na kwamba, hata wavuvi na mabaharia wanahamasishwa kutunza na kulinda mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuungana na wajumbe wa Utume wa Bahari, kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani kwa mafanikio makubwa yaliyokwisha kupatikana katika kipindi cha miaka 100 iliyopita, kama sehemu ya mchakato wa utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu kwa kutambua kwamba, Mitume wa kwanza wa Kristo Yesu walikuwa ni wavuvi kutoka Galilaya.  Rej Mt 4:19. Baba Mtakatifu anawataka wanachama wa Utume wa Bahari kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote. Wawasaidie wavuvi na mabaharia kushinda changamoto ya upweke, tayari kukua na kukomaa kwa ajili ya kuendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu.

Mabaharia na wavuvi wanachangia sana kwenye ustawi na maendeleo ya wengi
Mabaharia na wavuvi wanachangia sana kwenye ustawi na maendeleo ya wengi

Waathirika wakuu wa matumizi mabaya ya teknolojia na ukosefu wa usawa ni maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ikumbukwe kwamba, njia halisi ya kiikolojia daima ni njia ya jamii inayopaswa kuunganisha masuala ya haki katika midahalo ya mazingira, ili kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na kilio cha dunia. Rej. Laudato si, 48-52. Kwa hakika wajumbe wa utume wa Bahari wamekuwa ni vyombo vya huruma, upendo na mshikamano kwa mabahari, wavuvi pamoja na familia zao. Anawataka wawe na nguvu, furaha na amani ya Kristo Yesu iweze kuwatawala. Kwa upande wake Kardinali Michael Czerny, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu katika ujumbe wake kwa njia ya video, amegusia changamoto ambazo zinejitokeza katika kipindi cha miaka 100 iliyopita: UVIKO-19, Vita Kati ya Urussi na Ukraine; mambo yanayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Amewakumbuka wanachama wote walipoteza maisha kutokana na UVIKO-19 na kwamba kuna haja ya kudumisha usawa kwa watu wote, Bado kuna mabaharia wanaonyimwa ruhusa ya kutua nanga kwenye baadhi ya bandari pamoja na kukosa huduma msingi za kijamii. Takwimu zinaonesha kwamba, mabaharia wananyanyaswa, wanadhulumiwa na kutwezwa kutokana na vitendo vya kiharamia pamoja na kutumbukizwa katika mifumo mbalimbali ya ukoloni mamboleo. Pamoja na mambo mengine, wajumbe wanaendelea kujadili kuhusu: Usalama wa Mabaharia mintarafu uzalishaji na huduma kwa mabaharia; changamoto kwa Mabaharia; Tasaufi ya Mabaharia; Umuhimu wa Jumuiya Ndogondogo za Kikristo na Utume wa Bahari; familia za Mabaharia na Wavuvi pamoja na Dhoruba zilizoukumba utume wa Bahari.

Utume wa Bahari
03 October 2022, 16:27