Hija za Maisha ya Kiroho Zisaidie Kupyaisha na Kuimarisha Imani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Utambuzi wa maisha kwa kawaida unafumbatwa katika msingi wa fasihi simulizi ya maisha ya mtu katika: huduma yake kwa Mungu na jirani, mchakato wa ujenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu; mambo msingi katika maisha bila kusahau mambo yanayoweza kuchefua roho na akili ya mtu. Kumbe, ni jambo muhimu sana, mwamini akipata nafasi ya kutulia na kuanza kujichunguza mwenyewe tayari kuandika Kitabu cha historia ya maisha kutoka katika undani wa mtu mwenyewe. Katekesi ya Baba Mtakatifu Jumatano tarehe 19 Oktoba 2022 imejikita katika mchakato wa mwamini kuandika historia ya kitabu cha maisha yake kama kigezo msingi cha kufanya utambuzi.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, utambuzi uwasaidie waamini kusoma maisha yao, kwa kutambua faraja, neema na baraka zinazobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, bila kusahau upweke na ukiwa unaoweza kujikita katika sakafu ya nyoyo zao. Waamini wajitahidi kutambua ukweli wa maisha yao, mintarafu mwanga wa Injili. Hii inaweza kuwa ni fursa inayotolewa na Mwenyezi Mungu kwa mwamini kujifahamu vyema zaidi, tayari kuandika na kusimulia kitabu cha maisha yako kama mwamini. Yataka moyo anakiri Baba Mtakatifu Francisko. Waamini wajenge utamaduni wa kusoma na kutafakari Injili, ili hatimaye, waweze kuchota humo vigezo vitakavyowasaidia kupyaisha maisha yao binafsi na katika jamii. Vijana, wagonjwa, wazee na wanandoa wapya waendelee kujiaminisha katika ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ambaye anaheshimiwa kwa namna ya pekee na Mama Kanisa katika Mwezi Oktoba, Mwezi uliotengwa kwa ajili ya Ibada ya Rozari Takatifu, Muhtasari wa historia nzima ya ukombozi.
Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza na kuwashukuru watu wa Mungu kutoka nchini Croatia wanaofanya hija ya maisha ya kiroho kwenye Makaburi ya Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani, ili waweze kupyaisha na kuimarisha imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Anawaalika watu wa Mungu kutoka Croatia kukaza macho yao ya imani juu ya Kristo Yesu aliyetundikwa Msalabani, anayepanua mikono yake, tayari kuwapokea na kuwakumbatia katika huruma na upendo wake wa daima. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kukita mizizi yao katika imani, wasali na kuombea amani duniani; umoja na mshikamano wa watu wa Mungu nchini Croatia.