Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, ameungana na wakleri kutoka Lombardia, Kaskazini mwa Italia katika maadhimisho ya Siku ya Nane ya Mapadre Wazee na Wagonjwa Kutoka mkoa wa Lombardia. Baba Mtakatifu Francisko, ameungana na wakleri kutoka Lombardia, Kaskazini mwa Italia katika maadhimisho ya Siku ya Nane ya Mapadre Wazee na Wagonjwa Kutoka mkoa wa Lombardia.  

Ujumbe wa Papa Francisko Siku ya 8 Mapadre Wazee na Wagonjwa 2022: Sadaka na Majitoleo Yao.

Baba Mtakatifu Francisko, ameungana na wakleri kutoka Lombardia katika maadhimisho ya Siku ya Nane ya Mapadre Wazee na Wagonjwa.Huu ni ushuhuda wa udugu unaopata chimbuko lake katika Daraja takatifu ya Upadre. Ilikuwa ni siku ya upendo na mshikamano katika sala na udugu wa Kikuhani kama njia ya kuwaenzi Mapadre wazee na wagonjwa ambao wamejisadaka sana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko daima ameonesha upendo na mshikamano wake wa udugu wa kibinadamu na Mapadre wazee na wagonjwa. Hawa ni mapadre ambao wengine wamechoka na kudhohofu kwa afya mbaya na changamoto za maisha; kuna baadhi yao wametumbukia katika mateso na mahangaiko makubwa ya ndani, kutokana na huduma yao kwa familia ya Mungu. Licha ya mambo yote hayo, Baba Mtakatifu anasema, Mapadre wanaendelea kuandika kurasa za maisha na utume wa Kipadre sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu anapenda kuwashukuru na kuwatia moyo Mapadre, wote wakitambua kwamba, wao kwa hakika ni marafiki wa Kristo Yesu katika maisha na utume wao. Baba Mtakatifu anasema, kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale, ameyaona mateso na mahangaiko ya watu wake, anasema haachi kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Mapadre, akiwakumbuka katika sala zake; anataka kuwafariji wote katika nyoyo zao, ili hatimaye, waweze kuimba ukuu na utukufu wa Mungu katika maisha na utume wao! Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko, ameungana na wakleri kutoka Lombardia, Kaskazini mwa Italia katika maadhimisho ya Siku ya Nane ya Mapadre Wazee na Wagonjwa Kutoka mkoa wa Lombardia. Huu ni ushuhuda wa udugu unaopata chimbuko lake katika Daraja takatifu ya Upadre. Ilikuwa ni siku ya upendo na mshikamano katika sala na udugu wa Kikuhani kama njia ya kuwaenzi Mapadre wazee na wagonjwa ambao wamejisadaka sana kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa.

Papa anawapongeza Mapadre Wagonjwa na Wazee kwa Maisha na Utume wao
Papa anawapongeza Mapadre Wagonjwa na Wazee kwa Maisha na Utume wao

Askofu Antonio Napolioni wa Jimbo Katoliki la Cremona, Kaskazini mwa Italia, ndiye aliyeongoza Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa “Caravaggio”. Hili ni tukio ambalo limeandaliwa na UNITALSI Lombardia. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake, amewakumbusha Mapadre wazee na wagonjwa kwamba, hata kama kimwili wanaonekana kuwa ni dhaifu, lakini bado wanatekeleza dhamana na utume wao wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa: sala na sadaka yao; kwa kusikiliza pamoja na majitoleo ya mateso na mahangaiko yao kimwili, kama sadaka safi na yenye kumpendeza Mwenyezi Mungu kwa ajili ya majimbo na mashirika yao. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu anawapongeza Mapadre wazee na ambao kwa sasa uzee huu unaandamana na magonjwa. Huu ni ushuhuda wa upendo mwaminifu kwa Mungu na kwa Kanisa. Ni kielelezo cha kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo katika hali ya ukimya; kumbukumbu hai na msingi thabiti wa ujenzi wa Kanisa la Kristo Yesu kwa siku za mbeleni. Katika uzee na changamoto za magonjwa, kamwe wasikate tamaa na kudhani kwamba, hawana tena thamani mbele ya Mungu na Kanisa, bali huu ni wakati wa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na Mapadre vijana, ili kuondokana na tabia, utamaduni na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine; huu ndio utamaduni wa kutupa. Kwa Mapadre wazee na wagonjwa ni muda wa sala, sadaka na tafakari ya Neno la Mungu. Kwa wale ambao bado wana nguvu wanaweza kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kusikiliza na kuwaungamisha waamini wanaokimbilia huruma, msamaha na upendo wa Mungu katika maisha yao. Wawe mashuhuda wa historia ya huruma na upendo wa Mungu katika maisha na utume wao.

Mapadre wazee na wagonjwa ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu
Mapadre wazee na wagonjwa ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu

Baba Mtakatifu anawashukuru watu wote wa Mungu na kwa namna ya pekee UNITALSI Lombardia, yaani Umoja wa Kitaifa wa Wasafirishaji wa wagonjwa Lourdes na kwenye Madhabahu ya Kimataifa. UNITALSI ni juhudi zilizoanzishwa kunako mwaka 1903 na Giovanni Battista Tomassi, wakati alipokuwa anakaribia kukata tamaa ya maisha kutokana na kuandamwa mno na magonjwa, aliamua kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Lourdes, Ufaransa, hapo ndipo alipoonja matendo makuu ya Mungu katika maisha yake. Kwa maombezi ya Bikira Maria wa Lourdes akaongoka na hivyo kufanikiwa kuguswa na kweli za maisha ya Kikristo. Aliporudi nchini Italia, akaandika Katiba ya UNITALSI na huo ndio ukawa ni mwanzo wa UNITALSI kuanza kuenea kwa kasi ya ajabu nchini Italia. Hiki ni kielelezo makini cha ushuhuda wa imani tendaji katika matendo ya huruma yanayojionesha katika Parokia na Majimbo mengi nchini Italia. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, watu wanatumia vyema rasilimali muda waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu, ili kufurahia nafasi ya kukutana na jirani na hatimaye, kuweza kuganga na kuponya “kirusi” cha kudhani kwamba, mtu peke yake anaweza kujitegemea na kujitosheleza. Katika kimya kikuu, watu wengi wamenyanyua nyuso zao kuelekea mbinguni. Kwa neema ya Mungu hii inaweza kuwa ni fursa ya utakaso hata kwa Mapadre. Hakuna sababu ya kuogopa mateso, kwani Kristo Yesu anaubeba Msalaba pamoja nao!

Papa Wagonjwa
19 Septemba 2022, 14:59