Ujumbe wa Papa Francisko Siku 108 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani 25 Septemba 2022
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Chimbuko la Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani ni kutokana na mahangaiko pamoja na mateso ya watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia kutokana na madhara makubwa ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Papa Pio X, kunako mwaka 1914 akawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wakimbizi na wahamiaji duniani. Papa Benedikto XV akaanzisha siku hii rasmi na kunako mwaka 1952 ikaanza kusherehekewa na Kanisa la Kiulimwengu. Kunako mwaka 1985, Mtakatifu Yohane Paulo II akawa kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki kuanza kutoa ujumbe kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani, kama sehemu ya sera na mbinu mkakati wa Kanisa katika shughuli za kichungaji ili kusikiliza na kujibu kwa dhati kilio cha wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi na usalama wa maisha!
Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, sera na mikakati hii itaendelea kumwilishwa pia kwenye Makanisa mahalia, ili kuwasaidia watu hawa ambao mara nyingi wanajikuta wakitumbukia katika biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo na nyanyaso mambo ambayo kimsingi yanasigina: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Tangu mwaka 1952, Siku hii ilikuwa ikiadhimishwa Dominika baada ya Sherehe ya Tokeo la Bwana. Lakini kunako mwaka 2018, Baba Mtakatifu Francisko baada ya kusikiliza maoni na kuridhia maombi ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbalimbali za dunia akaamua kwamba, Siku hii iadhimishwe Dominika ya mwisho ya Mwezi Septemba na kwa mwaka huu inaadhimishwa tarehe 25 Septemba 2022. Maadhimisho ya Siku ya 108 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2022 yananogeshwa na kauli mbiu “Kujenga mustakabali wa wakimbizi na wahamiaji” kwa “Maana hapa hatuna mji udumuo, bali twautafuta ule ujao.” Ebr 13:14. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa maadhimisho haya anakazia kuhusu: Hatima ya maisha ya mwanadamu, mbingu na nchi mpya, kujenga mustakabali wa wakimbizi na wahamiaji; mchango wao; Yerusalemu mpya ni kwa wote pasi na ubaguzi; mchango maalum wa vijana na mwishowe ni sala kwa ajili ya waamini.
Mwanadamu hapa duniani ni msafiri anayeuendea Ufalme wa Mungu ulioanzishwa na Kristo Yesu na utimilifu wake ni pale atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu. Lakini Ufalme huu, uko kati ya waja wake lakini utapata utilimifu wake katika utukufu wa Kristo. Huu ni mji ambao umejengwa na Mwenyezi Mungu na kila mtu anashirikishwa kwa namna ya pekee. Lakini bado kuna changamoto kubwa kuweza kuifikia Yerusalemu mpya; maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu. Rej Ufu 21:3. Ni katika muktadha wa machafuko ya kisiasa yaliyojitokeza katika miaka ya hivi karibuni, watu wa Mungu wanahimizwa kujibidiisha kujenga mji wa Mungu kadiri ya mpango wa Mungu, ili watu waweze kuishi kwa amani na utu wema. Kama ilivyo ahadi ya Mwenyezi Mungu, tunatazamia mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa juu yake. Rej 2Pet 3: 13. Haki ni kati ya vifaa muhimu sana vya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Hii ni haki inayosimikwa katika: uvumilivu, sadaka na uthubutu ili wale wenye njaa na kiu ya haki waweze kutoshelezwa, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ndiye asili ya wema wote na hivyo binadamu anarejea tena kuwa mwema.
Lakini jambo la msingi, ni kukubali wokovu ulioletwa na Kristo Yesu na kusimikwa katika Injili ya Upendo, ili “kufyekelea mbali” mifumo yote ya ukosefu wa haki na ubaguzi. Mpango wa Mungu ni shirikishi na hasa kwa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya kijamii, kati yao anasema Baba Mtakatifu ni wakimbizi, wahamiaji na wale wote wanaotafuta hifadhi ya kisiasa; watu wasiokuwa na makazi maalum pamoja na waathirika wa mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo. Hawa ndio wale watakaourithi Ufalme wa mbinguni ambao umeandaliwa kwa ajili yao. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanamwilisha ndani mwao matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama kielelezo cha imani tendaji. Kwani katika hukumu ya mwisho, waamini wataulizwa jinsi walivyojibidiisha: kuwalisha wenye njaa, kuwanywesha wenye kiu, kuwakaribisha wageni; kuwavika walio uchi, kuwatazama wagonjwa na kuwatembelea wafungwa kifungoni. Rej Mt 25: 34-36. Baba Mtakatifu Francisko anasema “Kujenga mustakabali wa wakimbizi na wahamiaji” ni kutambua na kuthamini mchango unaoweza kutolewa na wakimbizi na wahamiaji katika ujenzi wa nchi inayowapatia hifadhi, kwani hawa pia ni wajenzi wa Yerusalemu mpya inayoangazwa na Mwenyezi Mungu na wageni watajenga kuta zake na malango yake yatakuwa wazi daima, ili watu wote wapate kuleta utajiri wa Mataifa yao. Rej Isa 60: 10-11.
Utabiri huu, uzoefu na mang’amuzi yanaonesha kwamba, wakimbizi na wahamiaji wamechagia kwa kiasi kikubwa katika mchakato wa ukuaji wa kiuchumi na kijamii. Ni watu ambao wamechangia nguvu kazi, ujana wao, ari na mwamko mpya. Wanaweza kuendelea kuchangia zaidi, ikiwa kama watapatiwa fursa. Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni changamoto na fursa ya ukuaji kitamaduni na kiroho, kwa watu wote; kwa kutambua na kuheshimu tofauti msingi zinazojitokeza; ili kujenga na kuimarisha ushirika. Kwa kuendelea kuwa wazi kati yao ili kupata maono na mapokeo tofauti na hatimaye, kuwa na mwelekeo mpya; kwa kutambua na kuthamini amana na utajiri unaofumbatwa katika dini za waamini wengine, tasaufi ambazo pengine ni mpya, kiasi cha kusaidia kuzamisha mizizi ya imani yao. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Yerusalemu mpya ni kwa ajili ya watu wote. Uzoefu unaonesha kwamba, wakimbizi na wahamiaji wakatoliki wamesaidia sana kupyaisha jumuiya za Kikristo zilizowapokea na kuwakaribisha kwa upendo. Wamekuwa ni chachu ya maboresho ya maadhimisho ya Mafumbo mbalimbali ya Kanisa, kiasi cha waamini wote kujisikia kuwa ni sehemu ya ukatoliki wa watu wa Mungu.
Ikiwa kama waamini wanataka kushiriki na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ujenzi wa mustabakali wa mwanadamu kwa siku za usoni, hawana budi kushirikiana na wakimbizi na wahamiaji na kwamba, kipaumbele cha pekee, wapewe vijana wa kizazi kipya. Mustakabali wa kesho, unaanza leo kwa kufanya maamuzi, ili kutekeleza mpango wa Mungu katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki, udugu wa kibinadamu na amani. Baba Mtakatifu katika sala yake kwa waamini anawataka wawe vyombo na mashuhuda wa matumaini na haki katika mchako wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu na kwamba, inapendeza kuishi vyema kama ndugu wamoja!