Tafuta

Papa Francisko anawapongeza na kutumaini kwamba, huduma ya upendo wa Kristo Yesu wanayoitekeleza, itasaidia katika mchakato wa ujenzi na ukuaji wa Ufalme wa Mungu hapa duniani. Papa Francisko anawapongeza na kutumaini kwamba, huduma ya upendo wa Kristo Yesu wanayoitekeleza, itasaidia katika mchakato wa ujenzi na ukuaji wa Ufalme wa Mungu hapa duniani.  

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Askofu mkuu Edgar Peña Parra, Katibu mkuu msaidizi wa Vatican, kwenda kwa Mama Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti wa WAWATA, Taifa, anawapongeza na kutumaini kwamba, huduma ya upendo wa Kristo Yesu wanayoitekeleza, itasaidia katika mchakato wa ujenzi na ukuaji wa Ufalme wa Mungu hapa duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) ni Dominika tarehe 11 Septemba 2022 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jijini Dar es Salaam kwa Ibada ya Misa Takatifu, ambayo imeongozwa na Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. WAWATA ni chombo cha kuwaunganisha Wanawake Wakatoliki Tanzania kilichoanzishwa kunako mwaka 1972 kwa lengo la kujitakatifuza na kuyatakatifuza malimwengu ikijishughulisha na shughuli zote za kuwaendeleza wanawake kiroho na kimwili ili kuwawezesha kutoa mchango wao kikamilifu kuliendeleza na kulistawisha Kanisa na jamii kwa ujumla katika nyanja za kiroho, matendo ya huruma na kiuchumi likiongozwa na Dhamira yake Kuu: Kwa Upendo wa Kristo Tutumikie na Kuwajibika. Licha ya WAWATA kuanzishwa rasmi mwaka huo wa 1972 baada ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kuridhia katiba yake, lakini pia chombo hiki ni mwanachama wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Duniani (WUCWO-World Union of Catholic Women Organization) iliyoanzishwa mwaka 1910 yenye makao yake makuu Paris, nchini Ufaransa.

Malezi kwa watoto na vijana yapewe kipaumbele cha kwanza
Malezi kwa watoto na vijana yapewe kipaumbele cha kwanza

Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa WAWATA, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Askofu mkuu Edgar Peña Parra, Katibu mkuu msaidizi wa Vatican, kwenda kwa Mama Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti wa WAWATA, Taifa, anawapongeza na kutumaini kwamba, huduma ya upendo wa Kristo Yesu wanayoitekeleza, itasaidia katika mchakato wa ujenzi na ukuaji wa Ufalme wa Mungu hapa duniani. Kwa upande wake, Mama Monique Faye Thiandoum, Makamu wa Rais wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Duniani, Kanda ya Afrika, (WUCWO-World Union of Catholic Women Organization), anawapongeza WAWATA kwa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya maisha na utume wao. Katika kipindi hiki WAWATA imekua na kukomaa na hivyo kusimama kidete katika mchakato wa maboresho ya maisha ya wanawake wa Tanzania, kwanza kabisa kama akina mama walioolewa, wanawake wa “shoka”, raia, vyombo na mashuhuda wa maendeleo fungamani ya binadamu. WUCWO inawapongeza WAWATA kwa ushiriki wao wa imani katika Kristo Yesu, Mwana wa Bikira Maria katika medani mbalimbali za kimataifa, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. WAWATA inapongezwa kuwa kushiriki katika ujenzi wa amani, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, malezi na makuzi sanjari na maboresho ya maisha ya wanawake.

Umoja, ushiriki na utume wa Watu wote wa Mungu ni muhimu sana kwa Kanisa
Umoja, ushiriki na utume wa Watu wote wa Mungu ni muhimu sana kwa Kanisa

Mengi yamefanyika katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, lakini, bado kuna changamoto, matatizo na fursa zinazopaswa kufanyiwa kazi na wanawake wote wakatoliki nchini Tanzania, kwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa WAWATA na kamwe wasiwe ni watazamaji. Malezi na makuzi ya watoto na vijana yapewe kipaumbele cha pekee kwani hawa ni tumaini na jeuri ya Kanisa kwa leo na Kesho iliyo bora zaidi. Kumbe, wanawake wanapaswa kusali, kutafakari na kushirikiana kutenda kama ndugu, ili mafanikio yanayopatikana yawe ni kwa ajili ya wote. Wanawake ni vyombo na mashuhuda wa Injili, dhamana na utume unaopaswa kuendelezwa na kudumishwa zaidi. Makamu wa Rais wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Duniani, Kanda ya Afrika, anawashukuru na kuwapongeza viongozi wa Kanisa la Tanzania kwa kushirikiana kikamilifu katika maisha na utume wa WAWATA katika kipindi cha Miaka 50 iliyopita, kwani mafanikio yote yaliyopatikana ni kutokana na umoja, ushiriki na utume wa watu wa Mungu nchini Tanzania. WAWATA vikongwe, waendelee kusimama kidete, kuhakikisha kwamba, wanawatia ari na moyo WAWATA vijana na Chipukizi katika ushiriki wao. Bikira Maria, Malkia wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Duniani, Kanda ya Afrika, aendelee kuwalinda kwa tunza yake ya kimama na kuwasindikiza katika maisha na utume wao kama WAWATA.

Papa WAWATA 50 Yrs

 

11 September 2022, 15:57