Papa Francisko Aridhia Katiba Mpya, Atangaza Baraza Kuu la Mpito, Taasisi ya Hospitali ya Malta
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Papa Paschal II, tarehe 15 Februari 1113 alichapisha Waraka wa Kitume wa “Pie postulatio voluntatis” yaani “Hitaji la utashi wa dhati” uliyotambua na kuthibitisha uhuru wa Taasisi ya Huduma za Hospitali ya Mtakatifu Yohane wa Yerusalemu, Rodi na Malta. Waraka huu huu uliihkakikishia Taasisi hii ulinzi, haki na upendeleo; kwa kushughulikia utatuzi wa migogoro, ili kuendelea na shughuli zake katika ngazi za Kitaifa na Kimataifa. Tarehe 24 Januari 1953 Mahakama ya Makardinali iliyoanzishwa rasmi na Papa Pius XII 10 Desemba 1951 ilitambua huduma makini zilizokuwa zinatolewa na Taasisi hii, katika uhuru wake, lakini kwa kuzingatia kwamba hii ni taasisi pia yenye mwelekeo wa kidini, kumbe, ilitakiwa pia kufuata sheria, kanuni na maagizo kutoka Vatican. Hii ni sehemu ya tamko lililotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Taasisi ya Huduma za Hospitali ya Mtakatifu Yohane wa Yerusalemu, Rodi na Malta ambayo amekuwa akiifuatilia kwa umakini mkubwa hasa kutokana na mchango wake katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Hii ni Taasisi ambayo wanachama wake wengi ni wakujitolea, kumbe, kuna haja pia ya kujikita katika ushuhuda wa kanuni maadili na utu wema. Kutokana na changamoto za kimaadili zilizojitokeza ndani Taasisi hii, Baba Mtakatifu alimteua Kardinali Silvano Maria Tomasi kuwa mjumbe wake maalum katika kipindi cha mageuzi pamoja na Marekebisho ya Katiba pamoja na kubainisha Kanuni maadili na utu wema ambao ungefuatwa na wote. Lakini kwa bahati mbaya, Kardinali Silvano Maria Tomasi alikumbana na vikwazo, kiasi cha kushindwa kutekeleza vyema dhamana na wajibu wake. Baada ya Baba Mtakatifu kusikiliza maoni ya watu mbalimbali sasa kwa Tamko hili, amemua kuhakikisha kwamba, anakamilisha mchako uliokuwa umekwisha kuanza, ili kuendelea kujikita katika uaminifu kwa karama asilia ya Taasisi hii. Lengo ni kulinda na kudumisha umoja, mshikamano na mafungamano jamii ya Taasisi hii. Baba Mtakatifu anatoa Agizo kwamba, Katiba mpya iliyoidhinishwa naye, ianze kutumika mara moja. Ametengua pia nafasi zote za uongozi na Baraza kuu la Ushauri wa Taasisi na anaunda Baraza Kuu la Mpito linalowajumuisha wajumbe wafuatao:
Fra 'Emmanuel Rousseau - Kamanda Mkuu
Riccardo Paternò di Montecupo - Kansela Mkuu
Fra 'Alessandro de Franciscis – Mkurugenzi mkuu wa Hospitali
Fabrizio Colonna – Mweka Hazina.
Baraza Kuu la Mpito linaundwa na wajumbe wafuatao:
Frà Roberto Viazzo
Frà Richard Wolff
Bw. John Eidinow
Fra 'João Augusto Esquivel Freire de Andrade
Mathieu Dupont
Antonio Zanardi Landi
Michael Grace
Francis Joseph McCarthy
Mariano Hugo Windisch-Graetz.
Baba Mtakatifu Francisko ameagiza kwamba, Mkutano Mkuu wa Dharura utaadhimishwa tarehe 25 Januari 2023 wakati wa Sherehe ya Wongofu wa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa, kwa kufuata Kanuni mpya alizoidhinisha hivi karibuni. Mkutano huu utasimamiwa na kuendeshwa na Kardinali Silvano Maria Tomasi hadi kukamilika kwake. Utekelezaji wa Agizo hili unaanza mara moja kutumika.