Papa:Maria atusaidie kufuata mfano na utakatifu wa maisha ya Yohane Paulo I
Na Angella Rwezaula - Vatican
Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya misa Takatifu, Dominika tarehe 4 Septemba 2022, kwa kumtangaza kuwa Mwenyeheri, Papa Yohane Paulo I ameshiriki pia sala ya Malaika wa Bwana. Kabla ya sala hiyo Papa amependa kutoa salamu zake kwa wote kwa ushiriki wao. Amewashukuru Makardinali, maaskofu na mapadre ambao wametoka nchi mbali mbali.
Papa Francisko vile vile akawasilimia hata wajumbe rasmi waliofika hapo kutoa heshima kwa Mwenyeheri mpya, amesema: “Wazo langu la heshima linakwenda kwa Rais wa Jamhuri ya Italia na Waziri Mkuu wa Ukuu wa Monaco”. Baba Mtakatifu amewasalimia pia mahujaji, wote hasa waamini kutoka Venezia, Belluno na Vittorio Veneto, sehemu zinazofungamana na maisha ya kibinadamu, ya kipadre na ya kiaskofu ya Mwenyeheri mpya Albino Luciani, yaani Papa Yohane Paulo I.
Kwa kuhitimisha Papa Francisko ameomba "kusali kwa Bikira Maria, ili aweze kuwapatia wote zawadi ya amani duniani kote, hasa kwa ajili ya nchi ya Ukraine iliyokumbwa na vita" .Papa amesema kamba: “Yeye, ni mfuasi wa kwanza na mkamilifu wa Bwana, atusaidie kufuata mfano na utakatifu wa maisha ya Yohane Paulo wa Kwanza”.