Tafuta

Papa Francisko amewapongeza Mapadre wa Shirika la Schonstatt kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Papa Francisko amewapongeza Mapadre wa Shirika la Schonstatt kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. 

Papa Francisko: Ukoloni wa Kiitikadi ni Hatari Kwa: Tunu, Utu, Heshima na Haki Msingi

Mifumo mbalimbali ya ukoloni wa kiitikadi inaendelea kusigina tunu msingi za maisha ya mwanadamu. Kristo Yesu kwa Msalaba wake ameanzisha Agano Jipya na la milele, linalofumbata mahusiano ya huruma na upendo wa Mungu. Waimarishe huduma ya upendo kwa familia, kwa kuchuchumilia tunu msingi za maisha ya familia pamoja na kudumisha mshikamano kati ya watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Mapadre wa Schönstatt, lilianzishwa karibu na Vallendar, na Padre Josef Kentenich (1885-1968), wa Shirika la Kazi za Kitume la Wapalottini. Tarehe 18 ktoba 1914, akawasilisha mpango wa kutaka kulipyaisha Kanisa kwa kuwakusanya vijana na kuwaandaa katika huduma ya Kipadre, chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama mpendelevu! Mpango huo ukaidhinishwa tarehe 18 Julai 1919. Tarehe 12 Oktoba 1964 vuguvugu la Schönstatt lilijitenga na Shirika la Wapallotini na hatimaye, kutambuliwa rasmi na Vatican kama Taasisi ya Kipapa tarehe 24 Juni 1988. Shirika la Mapadre wa Schönstatt, hivi karibuni limeadhimisha mkutano mkuu wa sita wa Shirika, kwa kuwachagua viongozi watakaongoza kwa miaka sita. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 1 Septemba 2022 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Mkutano mkuu wa Shirika la Mapadre wa Schönstatt waliomtembelea mjini Vatican. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amesikitika kusema kwamba, mifumo mbalimbali ya ukoloni wa kiitikadi inaendelea kusigina tunu msingi za maisha ya mwanadamu. Kristo Yesu kwa mateso na kifo Msalabani ameanzisha Agano Jipya na la milele, linalofumbata mahusiano na mafungamano ya huruma na upendo kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Waimarishe huduma ya upendo kwa familia, kwa kuchuchumilia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia pamoja na kudumisha mshikamano kati ya vijana na wazee. Bikira Maria awe ni mfano bora wa huduma katika familia.

Ukoloni wa kiitikadi ni hatari kwa tunu, utu na heshima ya binadamu
Ukoloni wa kiitikadi ni hatari kwa tunu, utu na heshima ya binadamu

Baba Mtakatifu Francisko amempongeza na kumshukuru Padre Alexandre Awi Mello, Shirika la Mapadre wa Schönstatt, ambaye alikuwa ni Katibu Msaidizi, Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha. Huyu ni kiongozi ambaye amemfahamu na kufanya naye utume kwa miaka mingi, kielelezo cha ushirika na Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anawaombea neema na baraka za Roho Mtakatifu, ili maamuzi yaliyofikiwa kwenye maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa Sita wa Shirika, yaweze kuwa na manufaa kwa watoto wote wa Mungu. Kristo Yesu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu, ameanzisha Agano Jipya la upendo unaobubujika kutoka katika Msalaba. Huu ni upendo unaojengwa na kudumisha mahusiano na mafungamano kati ya mwanadamu na Mwenyezi Mungu. Hili ni Agano la Upendo na Ukombozi. Baba Mtakatifu analipongeza Shirika la Mapadre wa Schönstatt kwa kusimama kidete katika ulinzi na tunza makini ya familia zinazopitia magumu, changamoto na fursa mbalimbali kwani Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu.

Familia ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Wanandoa wanapaswa kudumisha maagano yao ya ndoa, kwani leo hii kuna ndoa nyingi ambazo zimesambaratika na nyingine nyingi zinayumba. Vijana wengi anasema Baba Mtakatifu wameshikwa na kishawishi cha kuendekeza “uchumba sugu”; kuna wazee ambao wamesahaulika na kutelekezwa kama “magari mabovu” na kwamba, kuna umati mkubwa wa watoto unaoteseka kutokana na kinzani na migogoro ya kifamilia. Katika patashika zote hizi, Shirika la Mapadre wa Schönstatt limejitahidi kuwa ni chombo cha faraja na matumaini kwa familia sehemu mbalimbali za dunia kutokana na mifumo mbalimbali ya ukoloni wa kiitikadi kuendelea kushambulia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, utu na haki msingi za binadamu.

Papa Francisko anawapongeza kwa kusimama kidete kutetea familia.
Papa Francisko anawapongeza kwa kusimama kidete kutetea familia.

Kanisa halina budi kuwa mstari wa mbele ili kulinda, kutetea na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Mshikamano wa kidugu kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee hauna budi kuimarishwa na kwamba, msingi wa ndoa na familia hauna budi kwenda kadiri ya mapenzi ya Mungu. Waamini wakumbuke kwamba, imani na tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa kutoka kwa kizazi kimoja kwenda kwa kizazi kingine kwa njia ya familia imara. Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ni mfano bora wa kuigwa katika huduma kwa wagonjwa, wanyonge na dhaifu katika familia. Utenzi wa Bikira Maria yaani “Magnificat” una mwelekea Mwenyezi Mungu, ambaye ni mkuu, mwingi wa huruma na mapendo, mtakatifu na enzi zote ni zake na kwamba, huruma yake kwa watu wanaomcha hudumu kizazi hata kizazi. Hiki ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Huruma inakita mizizi yake katika msamaha wa kweli kama unavyojidhihirisha katika historia nzima ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Huu ni utenzi unaoshuhudia: upendo, neema na hekima inayofumbatwa katika maisha ya Bikira Maria.

Kristo Yesu kwa njia ya Fumbo la Msalaba ameanzisha agano la upendo.
Kristo Yesu kwa njia ya Fumbo la Msalaba ameanzisha agano la upendo.

Utenzi wa Bikira Maria unaonesha mwelekeo mpya kuhusu ulimwengu. Amefanya mambo makuu kwa mkono wake, amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao; Amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi, akawakweza wanyenyekevu. Wenye njaa amewashibisha mema, matajiri amewaacha waende mikono mitupu. Itakumbukwa kwamba, Bikira Maria, Mama mpendelevu anaheshimiwa sana na Shirika la Mapadre wa Schönstatt. Kiungo kikuu hapa ni upendo wa kidugu na ushirika na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kujenga urafiki wa kijamii, kielelezo cha maisha mapya yanayofumbatwa katika huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kikomo. Anawakumbuka na ataendelea kuwaombea katika maisha na utume wao, daima waendelee kujipyaisha kwa nguvu na mwanga wa Roho Mtakatifu; huku wakiwa na ujasiri kwa ajili ya huduma ya upendo kwa familia, Agano la Upendo kati ya Mungu na binadamu. Mkutano mkuu hapo tarehe 3 Agosti 2022 uliwachagua viongozi wafuatao kuliongoza Shirika kwa kipindi cha miaka 6. Mkuu wa Shirika ni Padre Alexandre Awi Mello, kutoka Brazil, Makamu mkuu wa Shirika ni Ignacio Camacho, kutoka Chile, Mkurugenzi wa Jumuiya huru ni Padre Francisco da Cruz Sobral kutoka Ureno. Washauri wengine ni Padre Joy Puthussery kutoka India na Padre Arkadiusz Sosna kutoka Poland.

Ukoloni wa Kiitikadi
02 September 2022, 16:28