Tafuta

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa anamwakilisha Papa Francisko kwenye mazishi ya Malkia Elizabeth II. Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa anamwakilisha Papa Francisko kwenye mazishi ya Malkia Elizabeth II. 

Papa Francisko: Mazishi ya Malkia Elizabeth II wa Uingereza: Askofu mkuu Gallagher Mwakilishi Wake

Baba Mtakatifu Francisko amemteuwa Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa kumwakilisha kwenye mazishi ya Malkia Elizabeth II, Jumatatu tarehe 19 Septemba 2022. Mazishi yanafanyika kwenye Westminster Abbey, hili ni Kanisa la kihistoria ambapo Wafalme na Malkia wa Uingereza wanatawazwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Malkia Elizabeth II wa Uingereza alifariki dunia tarehe 8 Septemba 2022, huku akiwa amezungukwa na wanafamilia wake, waliomsindikiza katika usingizi wa amani, baada ya kuwatumikia watu wa Mungu kwa muda wa miaka 70, huku akiwa ametimiza umri wa miaka 96. Baba Mtakatifu Francisko katika salam zake za rambirambi alimwelezea Malkia Elizabeth II wa Uingereza kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika moyo wa huduma na kujitoa bila ya kujibakiza kwa familia ya Kifalme, Watu wa Uingereza na Jumuiya ya Madola katika ujumla wake. Alikuwa ni shuhuda amini wa imani kwa Kristo Yesu na matumaini kwa ahadi zake za daima. Baba Mtakatifu aliiweka roho ya Hayati Malkia Elizabeth II chini ya huruma ya Baba wa milele. Katika maisha na utume wake, Hayati Malkia Elizabeth II alibahatika kukutana na kuzungumza na Mababa Watakatifu watano, kuanzia kwa Papa Pio XII mwaka 1951 hadi kwa Baba Mtakatifu Francisko tarehe 3 Aprili 2014.

Askofu mkuu Gallagher kumwakilisha Papa kwenye Mazishi ya Malkia
Askofu mkuu Gallagher kumwakilisha Papa kwenye Mazishi ya Malkia

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko amemteuwa Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa kumwakilisha kwenye mazishi ya Malkia Elizabeth II, Jumatatu tarehe 19 Septemba 2022. Mazishi yanafanyika kwenye Westminster Abbey, hili ni Kanisa la kihistoria ambapo Wafalme na Malkia wa Uingereza wanatawazwa. Hili ni Kanisa ambalo mwaka 1953 Malkia Elizabeth II wa Uingereza alivikwa taji na kutawazwa kuwa ni Malkia na kufunga pia pingu za maisha kunako mwaka 1947 na Mfalme Philip. Mazishi ya kitaifa yanayohudhuriwa na viongozi wakuu wa Serikali kutoka sehemu mbalimbali za dunia, yanafanyika kuanzia saa 5: 00 asubuhi, kwa kutanguliwa na maandamano makubwa na hatimaye, Malkia Elizabeth II atazikwa kwenye Kikanisa cha “King George VI Memorial Chapel” kilichopo Windsor.

Watu wengi wamejitokeza kutoa salam zao za mwisho kwa Malkia.
Watu wengi wamejitokeza kutoa salam zao za mwisho kwa Malkia.

Kutokana na kusuasua kwa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Urussi, Belarus, Mynamar na Zimbabwe, hakutakuwa na mwakilishi yeyote kutoka katika nchi hizi. Uhusiano kati ya Uingereza na Urussi ulivunjika mara baada ya Urussi kuivamia Ukraine. Hata hivyo Rais Vladimr Putin, hakuwa na wazo la kuhudhuria mazishi kutokana na vikwazo alivyowekewa na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya. Uingereza ilivunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Myanmar tangu mwezi Februari 2021 baada ya mapinduzi ya kijeshi kufanyika nchini humo na hivyo kupelekea machafuko ya kisiasa.

Hayati Malkia Elizabeth II
17 September 2022, 18:03