Tafuta

Mtumishi wa Mungu Yohane Paulo wa Kwanza atatangazwa kuwa ni Mwenyeheri tarehe 4 Septemba 2022. Mtumishi wa Mungu Yohane Paulo wa Kwanza atatangazwa kuwa ni Mwenyeheri tarehe 4 Septemba 2022.  

Mwenyeheri Papa Yohane Paulo wa Kwanza: Siku 33 : Ameacha Ujumbe Mzito

Mtumishi wa Mungu Yohane Paulo wa Kwanza anatangazwa kuwa ni Mwenyeheri, 4 Septemba 2022. Jumamosi tarehe 3 Septemba 2022 kunafanyika mkesha kwenye Kanisa kuu la Yohane wa Lateran Jimbo kuu la Roma. Tarehe 11 Septemba 2022, Jimbo la Belluno-Feltre litaadhimisha Misa Takatifu kumshukuru Mungu kwa kulipatia Kanisa Mwenyeheri mpya, Yohane Paulo wa kwanza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko baada ya kukutana na kuzungumza na Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu tarehe 13 Oktoba 2021 ameridhia kwamba, Mtumishi wa Mungu Yohane Paulo wa Kwanza atangazwe kuwa ni Mwenyeheri tarehe 4 Septemba 2022. Ibada hii inaadhimishwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro Mjini Vatican. Jumamosi tarehe 3 Septemba 2022 kunafanyika mkesha kwenye Kanisa kuu la Yohane wa Lateran Jimbo kuu la Roma. Tarehe 11 Septemba 2022, Jimbo Katoliki la Belluno-Feltre litaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kumshukuru Mungu kwa kulipatia Kanisa Mwenyeheri mpya, Papa Yohane Paulo wa kwanza. Itakumbukwa kwamba, muujiza uliopelekea hata Kanisa likaamua kumtangaza kuwa ni Mwenyeheri ni tukio la mtoto mmoja mgonjwa aliyekuwa kwenye hatari ya kufa huko Buenos Aires, Argentina, kutokana na kuandamwa na ugonjwa wa kifafa cha hatari kwa muda mrefu. Paroko wa Parokia iliyokuwa karibu na hospitalini hapo aliamua kuwahusisha wazazi wake na watu wenye mapenzi mema kusali na kuomba msaada kutoka kwa maombezi ya Papa Yohane Paulo wa Kwanza aliyejulikana pia kama Papa Albino Luciani, akapona kunako tarehe 23 Julai 2011 kwa muujiza.

Mwenyeheri Papa Yohane Paulo wa Kwanza alikuwa na karama nyingi.
Mwenyeheri Papa Yohane Paulo wa Kwanza alikuwa na karama nyingi.

Papa Yohane Paulo Kwanza alizaliwa tarehe 17 Oktoba 1912 huko “Forno di Canale” eneo linalojulikana leo kama “Canale d’Agordo” Jimbo la Belluno, nchini Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 2 Februari 1935 akapewa Daraja takatifu ya Ushemasi na tarehe 7 Julai 1935 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 15 Desemba 1958, Mtakatifu Yohane XXIII akamteuwa kuwa Askofu na ilipogota tarehe 15 Desemba 1969, Mtakatifu Paulo VI akampandisha hadhi na kuwa Patriaki wa Venezia. Tarehe 5 Machi 1973 Mtakatifu Paulo VI akamteuwa na kumtangaza kuwa Kardinali na kuongozwa na kauli mbiu yake ya Kikardinali “Humilitas” yaani “Unyenyekevu.” Papa Yohane Paulo wa kwanza alikuwa ni kiongozi mwenye imani thabiti, alionesha upendeleo wa pekee kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Alishiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na kusimama kidete kupinga utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika kifolaini na utoaji mimba. Baada ya kifo cha Mtakatifu Paulo VI, tarehe 26 Agosti 1978 akateuliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Papa wa 263 kuliongoza Kanisa Katoliki. Huu ni uchaguzi uliofanyika kwa muda wa siku moja tu na waamini wakaona moshi mweupe, alama kwamba, Papa mpya amepatikana.

Alibahatika kuliongoza Kanisa Katoliki kwa siku 33
Alibahatika kuliongoza Kanisa Katoliki kwa siku 33

Alikuwa ni kiongozi aliyekirimiwa karama na uwezo mkubwa, kiasi kwamba, wakati wa Katekesi yake, hakuwa na haja ya karatasi, yote yalimiminika kutoka kichwani! Waswahili wanasema "kwa hakika Baba huyu alikuwa anatema madini." Alibahatika kutoka mara moja tu mjini Vatican kwenda kusimikwa kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma. Tarehe 28 Septemba 1978 akafariki dunia, akiwa na umri wa miaka 65 huku akiwa ameliongoza Kanisa Katoliki kwa muda wa siku 33 tu na kuzikwa kwenye Makaburi yaliyoko chini ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ni Siku 33 za maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, lakini siku ambazo zimeacha alama ya kudumu katika akili na nyoyo za watu wengi. Kuna mengi ambayo yameandikwa na hata kutungiwa Sinema kuhusu kifo cha Papa Yohane Paulo wa Kwanza. Watu wengi waliguswa na utakatifu wa maisha yake, kiasi cha kuanza kumkimbilia katika sala. Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2017 akaridhia kwamba, atangazwe kuwa ni Mtumishi wa Mungu.

Yohane Paulo wa kwanza

 

02 Septemba 2022, 15:43