Tafuta

Papa Francisko Kipindi cha Kuombea Kazi ya Uumbaji ni kuanzia tarehe 1 Septemba hadi tarehe 4 Oktoba, Kumbukumbu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi: Amani, Mazingira na Maskini. Papa Francisko Kipindi cha Kuombea Kazi ya Uumbaji ni kuanzia tarehe 1 Septemba hadi tarehe 4 Oktoba, Kumbukumbu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi: Amani, Mazingira na Maskini. 

Papa Francisko: Kipindi cha Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira 1 Sept- 4 Oktoba 2022

Ni matumaini kwamba Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) utakaofanyika nchini Misri, Mwezi Novemba 2022, pamoja na Mkutano wa 15 wa Umoja wa Mataifa wa Bioanuwai (COP-15) utakaofanyika tarehe 7 – 19 Desemba 2022 huko Canada, itasaidia kuunganisha familia ya binadamu katika mchakato wa kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira kwa upande wa Kanisa Katoliki inayoadhimishwa tarehe 1 Septemba 2022 inanogeshwa na kauli mbiu “Sikilizeni Kilio cha Kazi ya Uumbaji” na kilele chake ni hapo tarehe 4 Oktoba 2022. Hii ni Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hii ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hiki ni kipindi muafaka cha kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kazi kubwa ya uumbaji sanjari na kujibu kwa vitendo kilio cha Mama Dunia na Maskini, hawa ndio wale “Akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi.” Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa ajili ya Siku ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira kwa mwaka 2022 anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema akisema: “Sikilizeni Kilio cha Kazi ya Uumbaji.” Anakazia wongofu wa kiikolojia katika maisha ya kiroho, Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) utakaofanyika nchini Misri, Mwezi Novemba 2022, Umuhimu wa utunzaji wa bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na deni kubwa la kiikolojia. Wongofu wa kiikolojia ni changamoto iliyotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II wakati ambapo wongofu wa janga la kiikolijia ni dhana iliyovaliwa njuga na Mtakatifu Paulo VI, mwaliko wa kusikiliza na kujibu kilio cha Mama Dunia na Maskini, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 31 Agosti 2022 ameanzisha Mzunguko mpya wa Katekesi Kuhusu Utambuzi. Hili ni tendo muhimu sana linalomwathiri kila mtu, kwa sababu kupanga ni kuchagua mambo mbalimbali katika maisha; ambayo kimsingi yanapaswa kufanywa kwa uthabiti mkubwa kwa kutambua kwamba, kuna pia mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kutoa wito kwa watu wote wa Mungu “Kusikiliza Kilio cha Kazi ya Uumbaji” kwa kuwahamasisha watu wote kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote, dhidi ya ulaji wa kupindukia hali inayopelekea uchafuzi na uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) utakaofanyika nchini Misri, Mwezi Novemba 2022, pamoja na Mkutano wa 15 wa Umoja wa Mataifa wa Bioanuwai (COP-15) utakaofanyika kuanzia tarehe 7 – 19 Desemba 2022 huko Montreal, Canada, itasaidia kuunganisha familia ya binadamu katika mchakato wa kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi.

Sikilizeni kilio cha kazi ya uumbaji
Sikilizeni kilio cha kazi ya uumbaji

Baba Mtakatifu Francisko anasema, ikolojia ya maisha ya kiroho iwahamasishe waamini kuwa na shauku ya kulinda mazingira, kwa kufungamanisha maisha ya kiroho na utunzaji bora wa mazingira, kwa kutambua uwepo angavu wa Mungu katika kazi ya uumbaji, kwa kuonesha moyo wa ukarimu na kujali kwa kutambua kwamba, ulimwengu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, mwaliko wa kujitoa sadaka kwa ajili ya matendo ya huruma. “Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakukifanyika chchote kilichofanyika. Hiki ni kipindi kwa ajili ya kusifu ukuu wa Mungu na kuombea utunzaji bora wa mazingira, kazi ya uumbaji, kama ilivyokuwa kwa Mtalkatifu Francisko wa Assisi, kila mwenye pumzi na amsifu Bwana. Rej. Zab. 150:6. Kuna kilio kikubwa cha Mama Dunia na maskini, kutokana na ulaji wa kupindukia unaosababisha majanga makubwa katika maisha ya mwanadamu. Wajibu kwa ajili ya dunia ya Mwenyezi Mungu maana yake ni kwamba, wanadamu kwa kujaliwa akili, wanapaswa waheshimu sheria za maumbile na uwiano uliopo kati ya viumbe vya dunia hii. Kazi ya uumbaji na kilio cha maskini ni mambo yanayopaswa kupewa msukumo wa pekee, bila kuwasahau watu mahalia ambao kimsingi wamekuwa wahanga wa athari za mabadililo ya tabianchi kama vile: ukame wa kutisha, mafuriko, vimbunga pamoja na ongezeko kubwa la kiwango cha joto duniani. Lakini, ikumbukwe kwamba, kilio cha maskini kina nguvu kwani kinapanda hadi mbinguni.

Uchoyo na ubinafsi ni sababu kubwa ya kilio cha Mama Dunia na maskini na kwamba vijana wanawataka watu wazima, kusimama kidete kulinda ikolojia ya ulimwengu huu, kwa kuheshimu kazi ya uumbaji; kwa toba na wongofu wa ndani, kwa kujenga na kudumisha urafiki mpya na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani. Changamoto ya utunzaji bora wa mazingira haina budi kupewa kipaumbele cha pekee kama ilivyo pia kwa sekta ya afya na vita sehemu mbalimbali za dunia, wito kwa wote ni wongofu wa kiikolijia unaosimikwa katika wongofu wa kijumuiya ili kuleta mabadiliko ya kudumu; mambo yanayopaswa pia kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa. Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) utakaofanyika nchini Misri, Mwezi Novemba 2022 ni sehemu ya mchakato kwa Jumuiya ya Kimataifa kutekeleza kwa vitendo Makubaliano ya Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, COP21. Kwa hakika kizazi cha Karne ya 21 kitakumbukwa kwa kubeba dhamana na wajibu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kiwango cha wastani wa nyuzi joto 1.5C ndicho kinachotakiwa vinginevyo, Jumuiya ya Kimataifa itakuwa inakabiliana na janga kubwa la uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote. Kumbe, changamoto ya kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa kwa asilimia 45% ifikapo mwaka 2030 ni muhimu sana. Umoja wa Mataifa unabainisha kwamba, kuna haja ya kutekeleza kwa vitendo upunguzaji wa nyuzi joto 1.5C kama ilivyobainishwa kwenye Makubaliano ya Paris chini ya mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi.

Changamoto ni kupunguza kiwango cha nyuzi joto 1.5.C
Changamoto ni kupunguza kiwango cha nyuzi joto 1.5.C

Kila nchi itaamua kiwango cha mchango wake katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Kiwango hicho kitategemea uchumi wa nchi husika na pia kiasi cha uzalishaji wa gesijoto. Kuongeza uwekezaji wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa angalau asilimia 50% ya fedha za jumla za ufadhili wa umma wa mabadiliko ya tabianchi. Yote haya yanahitaji wongofu wa kiikolijia, unaojikita katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; maendeleo fungamani ya binadamu, mshikamano wa udugu wa kibinadamu sanjari na upendo. Wongofu wa kiikolojia unahitaji haki jamii hasa kwa watu maskini ambao wanaathirika vibaya kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Mkutano wa 15 wa Umoja wa Mataifa wa Bioanuwai (COP-15) utafanyika kuanzia tarehe 7 – 19 Desemba 2022 huko Montreal, Canada. “UN Biodiversity Conference (COP 15) 7 - 19 December 2022 Montreal, Canada.” Huku zaidi ya spishi milioni moja za wanyama na mimea zikitishiwa kutoweka na robo tatu ya mfumo wa ikolojia wa Dunia kubadilishwa na shughuli za binadamu, COP-15 lazima ianzishe mfumo mpya wa kimataifa ili kukomesha mmomonyoko wa bayoanuwai ifikapo mwaka 2030.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, mintarafu hekima ya kale, maadhimisho ya Jubilei ni muda muafaka wa: "kukumbuka, kurudi, kupumzika na kurejesha.” Lengo ni kudhibiti kuporomoka zaidi kwa bayoanuwai, inayojenga “mtandao wa maisha” ambao mwanadamu amekirimiwa na Mwenyezi Mungu. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kufikia makubaliano juu ya Kanuni Nne Muhimu: 1. kujenga msingi wa kimaadili wazi kwa ajili ya mabadiliko yanayohitajika ili kuokoa viumbe hai; 2. Kupambana na upotevu wa viumbe hai, kusaidia uhifadhi na ushirikiano, na kukidhi mahitaji ya watu kwa njia endelevu; 3. Kukuza mshikamano wa kimataifa kwa kuzingatia ukweli kwamba, bayoanuwai ni mafao ya pamoja ya Kimataifa yanayodai dhamira ya pamoja; na 4. Kutoa kipaumbele cha kwanza kwa watu walio katika mazingira magumu, ikiwa ni pamoja na wale walioathirika zaidi na upotevu wa viumbe hai, kama vile watu asilia, wazee na vijana. Baba Mtakatifu Francisko anarudia kusema: “Kwa jina la Mwenyezi Mungu, naomba makampuni makubwa ya uchimbaji madini na mafuta; uvunaji misitu, mali isiyohamishika, pamoja na biashara ya kilimo kuacha kuharibu misitu, ardhi oevu na milima; kuacha kuchafua mito na bahari, kuacha kutia sumu kwenye chakula sanjari na kujali watu na mazingira. Je, tunawezaje kushindwa kukiri kuwepo kwa "deni la kiikolojia" (Laudato si', 51) lililofanywa na nchi tajiri kiuchumi, ambazo zimechafua zaidi katika karne mbili zilizopita; hii inadai kwamba wachukue hatua kabambe zaidi katika COP27 na COP15.

Mshikamano wa upendo na maskini.
Mshikamano wa upendo na maskini.

Mbali na hatua zilizoamuliwa ndani ya mipaka yao, hii ina maana ya kuweka ahadi zao za msaada wa kifedha na kiufundi kwa Nchi maskini zaidi kiuchumi, ambazo tayari zinakabiliwa na mzigo mkubwa wa mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi. Inafaa pia kuzingatia kwa haraka msaada zaidi wa rasilimali fedha kwa ajili ya uhifadhi wa bayoanuwai. Hata zile nchi tajiri kidogo kiuchumi zina majukumu makubwa japokuwa zinatofautiana katika suala hili; kuchelewa kwa upande wa wengine kamwe hakuwezi kuhalalisha kushindwa kwetu sisi wenyewe kuchukua hatua. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kufanya maamuzi magumu kwani hali ni tete sana. Kipindi hiki cha Sala kwa ajili ya kuombea Kazi ya Uumbaji, waamini wamwombe Mwenyezi Mungu, ili kwamba, Mikutano ya COP27 na COP15 iweze kutumika kuunganisha familia ya binadamu katika kukabiliana barabara na athari za mabadiliko ya tabia nchi sanjari na kupunguza bayoanuwai. Jumuiya ya Kimataifa ikumbuke himizo la Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa: la kufurahi pamoja na wale wanaofurahi na kulia pamoja na wale wanaolia (Rej. Rum 12:15), watu waguswe na sala ya uchungu kuhusu kazi ya uumbaji na kutikia sala hii kwa vitendo, ili kizazi hiki na vizazi vijavyo viendelee kumshangilia na kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa wimbo mtamu wa Kazi ya Uumbaji, Uhai na Matumaini.

Papa Kazi ya Uumbaji
01 September 2022, 16:32