Tafuta

Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi linaloadhimishwa mjini Kaza, Nur Sultan huko nchini Kazakhstan, kuanzia tarehe 13-15 Septemba 2022. Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi linaloadhimishwa mjini Kaza, Nur Sultan huko nchini Kazakhstan, kuanzia tarehe 13-15 Septemba 2022. 

Hija ya Papa Francisko Nchini Kazakhstan: Kongamano la Kidini

Baba Mtakatifu Francisko anashiriki katika Kongamano hili na akiwa nchini Kazakhstan kwa muda wa siku tatu, anatarajiwa kutoa hotuba tano. Hii ni hija ya 38 ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa, lengo ni kuendelea kuragibisha mchakato wa majadiliano ya kidini kwa ajili ya kujenga na kudumisha misingi ya: Maendeleo, haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi linaloadhimishwa mjini Kaza, Nur Sultan huko nchini Kazakhstan kuanzia tarehe 13-15 Septemba 2022, linanogeshwa na kauli mbiu “Mchango wa Viongozi wa Dini Duniani na Dini za Jadi katika mchakato wa maendeleo ya kijamii na kiroho baada ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.” Baba Mtakatifu Francisko anashiriki katika Kongamano hili na akiwa nchini Kazakhstan kwa muda wa siku tatu, anatarajiwa kutoa hotuba tano. Hii ni hija ya 38 ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa, lengo ni kuendelea kuragibisha mchakato wa majadiliano ya kidini kwa ajili ya kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Vatican News anabainisha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anakwenda nchini Kazakhstan kama hujaji wa amani na umoja. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”, Kardinali Parolin anasema udugu na urafiki wa kijamii ni dira na mwongozo wa mchakato wa ujenzi wa ulimwengu ulio bora zaidi na unaosimikwa katika misingi ya haki, amani na utulivu, dhamana na wajibu wa: watu wote pamoja na taasisi mbalimbali duniani. Baba Mtakatifu anapinga kwa nguvu zote vita na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Majadiliano ya kidini ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi
Majadiliano ya kidini ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi

Hati hii inajikita zaidi katika masuala msingi ya kijamii katika maisha ya mwanadamu. Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu ilitiwa mkwaju kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Huu ni mwaliko na changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu wa kibinadamu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Utamaduni wa amani duniani unahatarishwa na ubinafsi, uchu wa mali na madaraka; umaskini na athari za mabadiliko ya tabianchi. Amani ya kweli inajengwa katika msingi wa maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili; kanuni maadili na utu wema; utawala wa sheria na haki msingi za binadamu! Vita, kinzani na mipasuko ya kijamii ni sehemu ya hali halisi ya maisha ya binadamu yanayopswa kufanyiwa kazi kwa kujikita katika kanuni maadili, sheria za kimataifa sanjari na ujenzi wa siasa ya amani duniani inayofumbata majadiliano katika ukweli na uwazi.

Kongamano la VII la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi 2022.
Kongamano la VII la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi 2022.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwekeza katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa amani duniani; upendo na mshikamano wa dhati; majadiliano pamoja na kusimama kidete kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu, uhuru pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Jumuiya ya Kimataifa iwezeke katika uchumi unaojali na kuzingatia mahitaji msingi ya binadamu, utu na heshima yake. Vita itaendelea kuibuka sehemu mbalimbali za dunia, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa haitawajibika barabara kudhibiti biashara haramu ya silaha duniani inayoendelea kupandikiza mbegu ya kifo kwa watu wasiokuwa na hatia! Badala ya kuwekeza katika biashara ya silaha duniani, rasilimali fedha hii ielekezwe zaidi katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya wengi, tayari kupambana na umaskini wa hali na kipato! Jambo la msingi ni kujenga mshikamano kati ya mataifa kwa kuongozwa na kanuni auni, mchakato unaoweza kufanikisha hata utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia ifikapo mwaka 2030 kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya familia ya binadamu!

Kardinali Pietro Parolin anasema, Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi ni muda muafaka wa majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi. Nchi ya Kazakhstan ilikuwa ya kwanza kuwekeana Mkataba wa maelewano na Vatican kunako mwaka 1998 na nchi hii kutembelewa na Mtakatifu Paulo II kunako mwaka 2001. Mwaka 2022, Vatican na Kazakhstan zinaadhimisha Kumbukizi ya Miaka 30 ya Uhusiano wa Kidiplomasia na kwamba, hija ya kitume ya Papa Francisko inaweza kuwa ni fursa ya kuboresha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili. Ni matumaini ya Vatican kwamba, Serikali ya Kazakhstan itaboresha utoaji wa vibali kwa wamisionari wanaotaka kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu nchini humo. Uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko kati pamoja nao, utasaidia kupyaisha imani, matumaini na mapendo kati ya watu wa Mungu na kuendelea kujikita katika shuhuda za wafiadini na waungama imani kutoka nchini humo ili kujenga jamii inayosimikwa katika umoja, maridhiano, haki na amani.

Kardinali Parolin
12 September 2022, 15:48