Tafuta

Shirikisho la Wanahabari Wakatoliki, SIGNIS, liliundwa kunako mwaka 2001 na kutambuliwa rasmi na Vatican tarehe 24 Oktoba 2014 Shirikisho la Wanahabari Wakatoliki, SIGNIS, liliundwa kunako mwaka 2001 na kutambuliwa rasmi na Vatican tarehe 24 Oktoba 2014  

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Kongamano la Dunia la SIGNIS 2022, Seoul, Korea ya Kusini

SIGNIS kuanzia tarehe 15-19 Agosti 2022 huko mjini Seoul, Korea ya Kusini, linaadhimisha Kongamano la Dunia la SIGNIS 2022 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Amani katika ulimwengu wa kidigitali” linalohudhuriwa na wajumbe kutoka sehemu duniani kote. Huu ni mkutano unaofanyika kwa wajumbe kuhudhuria mubashara na wengine kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya jamii

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Wanahabari Wakatoliki, SIGNIS, liliundwa kunako mwaka 2001 na kutambuliwa rasmi na Vatican tarehe 24 Oktoba 2014 baada ya kuunganisha Mashirika ya OCIC, lililoanzishwa mwaka 1928 na UNDA mwaka 1945 kushughulikia masuala ya tasnia ya mawasiliano ya jamii ndani ya Kanisa. Lengo kuu ni kuhakikisha kwamba, SIGNIS inashiriki katika mchakato wa kutetea, kulinda na kudumisha utu, heshima ya binadamu na haki zake msingi. SIGNIS inapaswa kujielekeza zaidi katika masuala ya haki, amani na upatanisho, kama sehemu ya utume wake ulimwenguni ili kuhakikisha kwamba, SIGNIS inashiriki kikamilifu katika kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa kweli na mwanga wa Kiinjili. Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia baadhi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii vimekuwa na mwelekeo hasi dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Kutokana na changamoto hii, Kanisa lina wajibu wa kuhakikisha kwamba, watu wanapata habari muhimu na za kweli kuhusiana na masuala mbalimbali yanayowazunguka, kwa kuzingatia haki na upendo, kwani ulimwengu umeumbwa kutokana na upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kukombolewa na Kristo Yesu, aliyejisadaka kwa ajili ya mwanadamu, ili kumrudishia tena mwanadamu hadhi yake iliyokuwa imepotea kutokana na dhambi.

SIGNIS inachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, inashiriki kikamilifu katika majiundo makini ya wanahabari, ili kweli waweze kuwa ni mwanga wa mataifa na chumvi ya dunia kwa maneno na matendo yao yanayoonesha imani tendaji kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha wanahabari kwamba, kazi yao inahitaji maandalizi makini, uzoefu na mang'amuzi ya ndani kwa kutafuta daima kile kilicho: kweli, chema na kizuri katika maisha ya mwanadamu. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo mwamini anapata neema ya utakaso, changamoto ya kuchuchumilia utakatifu wa maisha, dhamana inayopaswa kuendelezwa na SIGNIS katika maisha na utume wake ulimwenguni, kwa kuwajengea uwezo wanahabari ili kweli waweze kuwa ni watakatifu wanapotekeleza nyajibu zao za kila siku. Wanahabari watafute daima: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi wanapomhudumia mwanadamu na kwamba, SIGNIS inalo jukumu la kuwatangazia pia Watu wa Mataifa Habari Njema ya Wokovu. Kumbe, SIGNIS inawajibika kuwafunda wanahabari, kuwaunga mkono katika utekelezaji wa majukumu yao pamoja na kusambaza habari kadiri ya mwanga wa Injili, ili kweli wanahabari waweze kuwa ni wahudumu makini wa binadamu katika mahitaji yake msingi: kiroho na kimwili.

Wanahabari wawe ni wasanii na wajenzi wa utamaduni wa kusikiliza kwa makini.
Wanahabari wawe ni wasanii na wajenzi wa utamaduni wa kusikiliza kwa makini.

SIGNIS kuanzia tarehe 15-19 Agosti 2022 huko mjini Seoul, Korea ya Kusini, inaadhimisha Kongamano la Dunia la SIGNIS 2022 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Amani katika ulimwengu wa kidigitali” linalohudhuriwa na wajumbe kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Huu ni mkutano unaofanyika kwa wajumbe kuhudhuria mubashara na wengine kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Korea ni nchi ambayo vyombo vya mawasiliano ya jamii vimesaidia sana katika mchakato wa uinjilishaji, dhamana iliyotekelezwa kwa kiasi kikubwa na waamini walei. Hadithi za Mtakatifu Andrea Kim na wenzake, zilizosimuliwa na kuchapishwa zisaidie kuleta hamasa na kukoleza uinjilishaji katika lugha ya vyombo vya mawasiliano ya jamii. Mabadiliko makubwa katika ulimwengu wa mawasiliano kwa njia ya kidigitali yameonesha ile nguvu ya kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano katika ushirika sanjari na majadiliano katika familia ya binadamu. Dhamana hii imejionesha kwa namna ya pekee kabisa wakati wa maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 wakati watu wengi walipolazimika kukaa katika karantini. Ulimwengu wa kidigitali umekuwa ni chimbuko la taarifa msingi, lakini pia ulimwengu huu umesaidia familia na jumuiya za waamini kujumuika pamoja katika sala na ibada mbalimbali.

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa washiriki wa Kongamano la Dunia la SIGNIS 2022 huko mjini Seoul, Korea ya Kusini. Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anagusia masuaala ya maadili na utu wema; utamaduni wa kusikiliza na kujadiliana katika ukweli na uwazi na kwamba, kusikiliza ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Baba Mtakatifu Francisko anasema, ulimwengu wa mawasiliano ya kidigitali na hasa mitandao ya kijamii imeibua masuala mazito mintarafu kanuni maadili na utu wema, mwaliko kwa wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kufanya mang’amuzi ya busara, ili kujenga mahusiano na mafungamano ya kweli na bora katika mahusiano ya kibinadamu. Baadhi ya tovuti zimekuwa ni kero na sumu, kwa kuchochea na kupandikiza chuki; pamoja na kusambaza habari porofu. SIGNIS inaweza kuwasaidia hasa vijana wa kizazi kipya kukuza elimu na akili timamu na dhamiri nyofu ya kuweza kuchambua na kujifunza kutofautisha kati ya habari potofu na zile za kweli; mema na mabaya pamoja na kujikita katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika haki, upatanisho wa kijamii na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

SIGNIS ihamasishe utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote
SIGNIS ihamasishe utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote

Ni matamanio halali ya Baba Mtakatifu Francisko kuona kwamba, Ulimwengu wa kidigitali unakuwa shirikishi zaidi, kuliko hali inavyoonekana kwa sasa kwa baadhi ya Jumuiya kujikuta kwamba, ziko nje ya ulimwengu wa kidigitali. SIGNIS inapaswa kujiwekea mikakati itakayoziwezesha jumuiya hizi pia kuingizwa katika ulimwengu wa kidigitali na kwamba, mchango wao maalum uwe ni uenezaji wa utamaduni wa amani unaojikita katika ukweli wa Injili. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya 56 ya Upashanaji Habari Ulimwengu kwa mwaka 2022, umenogeshwa na kauli mbiu “Kusikiliza kwa Sikio la Moyo.” Baba Mtakatifu katika ujumbe huu, anakazia umuhimu wa kusikiliza kama tunu na amana katika tasnia ya mawasiliano ya jamii na kama njia ya kunogesha majadiliano katika ukweli na uwazi; majadiliano kati ya Mungu na waja wake kama kielelezo cha neema, ingawa mwanadamu ana tabia ya kutaka kuziba masikio yake. Baba Mtakatifu anasema, kusikiliza ni kielelezo cha mawasiliano bora zaidi yanayosimikwa katika: ukweli na uwazi; imani na uaminifu. Kumbe, kusikiliza ni kati ya sifa kuu za majadiliano na mawasiliano bora yanayofumbatwa katika uvumilivu ili kugundua ukweli wa mambo katika ukuaji wa uchumi, changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, ili hatimaye kuondokana na maamuzi mbele na ugumu wa mioyo.

Baba Mtakatifu anawataka wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kuwa ni “Mitume wa Sanaa na Utamaduni wa Kusikiliza” na hasa kama ni wanahabari wa Kanisa. Watambue kwamba, upashanaji habari si tu taaluma, bali ni huduma inayojikita katika majadiliano na maelewano kati ya watu na jumuiya kubwa katika ujumla wake, ili kujenga na kudumisha amani, utulivu na maridhiano kati ya watu. Sanaa na utamaduni wa kusikiliza ni muhimu sana katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, linaloadhimishwa na Mama Kanisa kwa sasa. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, SIGNIS itawasaidia watu watakatifu na waaminifu wa Mungu katika ujenzi wa sanaa na utamaduni wa kusikilizana, kusikiliza mapenzi ya Mungu na kukua katika ushirika, unaowaunganisha na kuwajumuisha pamoja. SIGNIS isaidie kukoleza juhudi za kukuza na kudumisha amani katika ulimwengu wa kidigitali ili hatimaye, kuunda ushirika unaosimikwa katika maridhiano na utakatifu. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu anawatakia heri na baraka washiriki wa Kongamano la Dunia la SIGNIS 2022 huko mjini Seoul, Korea ya Kusini, ili hatimaye, Kongamano hili liweze kuzaa matunda ya kiroho yanayokusudiwa yaani amani katika ulimwengu wa kidigitali.  

Papa SIGNIS 2022
13 August 2022, 16:11