Papa Francisko: Vijana Ni Jeuri Na Chemchemi ya Matumaini Kwa Maisha na Utume wa Kanisa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Vikundi vya Vijana vya Mama Yetu “Youth of the Équipes Notre-Dame, YTOL” ni vuguvugu la vijana ndani ya Kanisa Katoliki kwa ajili ya vijana waseja wenye umri kati ya miaka 18-30, wengi wao ni wanafunzi, wafanyakazi na wataalam wa masuala ya malezi na makuzi kwa vijana wanaopenda kukuza na kuimarisha imani katika mwanga wa Roho Mtakatifu. Haijalishi uzoefu wa kibinadamu, maisha ya kiroho, hali ya uchumi na kijamii, utamaduni na shughuli zinazompatia kijana mahitaji yake msingi, kwani wote hawa wanakarisbishwa ili kupyaisha imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Mwaliko kwa vijana wote ni kuchuchumilia utakatifu na maisha adili. Vuguvugu hili lilianzishwa na Padare Henri Caffarel kunako mwaka 1930 huko Paris, nchini Ufaransa. Tarehe 8 Desemba 1947 vuguvugu hili likachapisha Katiba yake “Carta delle Équipes Notre-Dame” na kutambuliwa rasmi na Vatican kama Chama cha Kitume tarehe 19 Aprili 1992. Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 6 Agosti 2022 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa “Vikundi vya Vijana vya Mama Yetu, “Youth of the Équipes Notre-Dame, YTOL” mjini Vatican. Baba Mtakatifu katika hotuba yake, ametafakari pamoja nao kuhusu umuhimu wa kufanya kazi kama timu kama kielelezo cha kutegemeana na kukamilishana katika safari ya maisha.
Vijana wana thamani kubwa katika maisha na utume wa Kanisa na Kristo Yesu anawapenda upeo. Vijana watambue kwamba, wao ni matumaini ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Wanandoa na Makleri, wanahamasishwa kuwa ni wanyoofu, watulivu na mashuhuda wa upendo na huduma kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Maandiko Matakatifu yanaonesha upendeleo wa pekee ambao Kristo Yesu aliwaonesha vijana waliotamani kumfuasa katika maisha na utume wake kama inavyojionesha kwa yule kijana tajiri, ambaye Kristo Yesu, alimwona, akampenda na hatimaye, akamwita kumfuasa, lakini kwa bahati mbaya, yule kijana alizongwa mno na malimwengu kiasi cha kukataa kutikia wito wa Kristo Yesu. Rej Mk 10:21. Tangu mwanzo wa maisha na utume wake, Kristo Yesu alipenda kuandamana na vijana, kwa kujenga urafiki, matumaini na kuonesha ule umuhimu wa kutembea pamoja katika kutangaza na kushuhudia Ufalme wa Mungu kati ya watu wa Mataifa. Vijana ni chanzo na chemchemi ya matumaini ya maisha na utume wa Kanisa. Hii ndiyo changamoto kubwa kwa wanachama wa “Vikundi vya Vijana vya Mama Yetu, “Youth of the Équipes Notre-Dame, YTOL” katika maisha na utume wao, kwani wanahimizwa kujikita katika Mafundisho ya Kanisa kuhusu Ndoa na Familia, daima wakijitahidi kujenga mahusiano na mafungamano na Kristo Yesu pamoja na Bikira Maria, ili waweze kuwa wamisionari katika hija ya maisha yao ya kila siku.
Baba Mtakatifu anawataka wanachama wa vikundi hivi kujenga na kudumisha utamaduni wa kufanya kazi kama timu moja, kwa kutambua kwamba, wanategemeana na kukamilishana katika maisha na utume wao na wala hakuna mtu anayeweza kujiokoa peke yake. Kamwe vijana wasidhani na kufikiria kwamba, wao ni bora zaidi kuliko wengine, kwani kwa kufanya hivi ni dalili za kupekenywa na tabia ya uchoyo na ubinafsi, magonjwa hatari sana katika jamii ya mwanadamu. Uchoyo na ubinafsi, unawanyima vijana wengi upendo wa dhati, mahusiano na mafungamano ya kijamii, kiasi hata cha kushindwa kuwa na ndoto ya pamoja, kwa kuthubutu kufanya maamuzi magumu katika maisha, kwa kuteseka na kuserebuka na wengine katika maisha. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuthubutu na kamwe wasiogope kufanya maamuzi magumu katika maisha, kwani katika mzunguko wa maisha ya mwanadamu, daima watakumbana na kesi za: uonevu, dhuluma, nyanyaso, ukosefu wa uaminifu na hata pengine usaliti, jambo la msingi ni vijana kupiga moyo konde na kutokuogopa hata kidogo! Kristo Yesu anapenda kuandamana na vijana katika hija ya maisha yao na kamwe hatawaacha wapotelee kwenye ombwe, bali wajitahidi kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu na wajitahidi kufanya kazi kama timu kwa kushirikiana na wengine. Baba Mtakatifu ametafakari pamoja nao dhana ya “Notre Dame na Ujana” kwa kutambua kwamba, vijana wamepewa upendeleo wa pekee katika maisha na utume wa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Chini ya Msalaba Kristo Yesu, aliwakabidhi vijana wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria kwa njia ya yule mwanafunzi aliyempenda, yaani Mtakatifu Yohane. Rej. Yn 19:27.
Lakini ikumbukwe kwamba, Bikira Maria ni Mama ya wafuasi wote wa Kristo Yesu na kwa kukubali kwake wito wa kuwa ni Mama wa Mungu, akawa pia ni Mama wa Kanisa. Huu ni mwaliko kwa vijana na maskini wote kujikabidhi na kujinyenyeksha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili waonje upendo wake wa daima. Ibada kwa Bikira Maria, itawajengea vijana maisha adili na matakatifu, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani kama alivyofanya kwa binamu yake Elizabeth. Rej Lk 1:39. Ujumbe huu uwe ni mwaliko kwa vijana kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, kuanzia tarehe 1 hadi 6 Agosti 2023 Jimbo kuu la Lisbon, nchini Hispania kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha vijana kwamba wao ni matumaini na jeuri ya maisha na utume wa Kanisa, kumbe, wanapaswa kuwa makini zaidi katika maisha yao ya kila siku, huku wakiwa na ndoto na matamanio halali ya maisha. Kamwe vijana “wasimwagilie nyoyo na akili zao” kwa litania ya malalamiko yasiyokuwa na kichwa wala miguu. Wajenge na kudumisha utamaduni wa kushirikiana na kushirikishana na wengine amana na utajiri ambao Mwenyezi Mungu amewakirimia katika maisha. Wajenge ari na moyo wa kujadiliana na wengine katika ukweli na uwazi; wawe tayari kuwasikiliza wengine wanapozungumza, ili kuthamini mchango, hekima na busara yao.
Baba Mtakatifu kwa mara nyingine tena, amewataka wanandoa, makleri na wanachama wote wa “Vikundi vya Vijana vya Mama Yetu, “Youth of the Équipes Notre-Dame, YTOL”, kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika: utulivu, unyoofu wa moyo na mashuhuda wa upendo na huduma kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Wajenge pia utamaduni wa kusikiliza kwa makini, kujadiliana na vijana katika ukweli na uwazi, daima wakijitahidi kuboresha maisha yao kwa njia ya Sala, Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza kwa huduma na majitoleo yao kwa ajili ya malezi na makuzi ya vijana wa kizazi kipya katika maisha ya ndoa na familia.