Papa Francisko Umuhimu wa Likizo Katika Maisha ya Mwamini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 10 Agosti 2022 amewakumbusha waamini na watu wenye mapenzi mema kwamba, likizo kwa watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia ni muda muafaka wa kujipatia nafasi ya kupumzika: kimwili na kisaikolojia, ili kupyaisha tena nguvu za kuweza kusonga mbele katika mapambano ya maisha ya kila siku. Ni fursa makini ya kutenga muda kwa ajili ya sala na kujitahidi kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ni wakati pia wa kujenga, kudumisha na kuimarisha mahusiano na ujirani wema, kwa kuwashirikisha wengine muda, karama na mapaji ambayo Mwenyezi Mungu amewakirimia waja wake. Ni muda wa kutafakari kazi ya uumbaji inayoshuhudia na kutangaza upendo wa Mungu kwa waja wake. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, likizo ni wakati muafaka wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa, shukrani, ukuu na uweza kutokana na kazi kubwa ya uumbaji. Mwanadamu katika ulimwengu mamboleo anayo kila sababu ya kulinda, kutunza na kuendeleza utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kwani mazingira bora na safi ni ufunuo wa: nguvu, wema, ukuu na utakatifu wa Mungu.
Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani: “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” ni dira na mwongozo makini katika mchakato wa wongofu wa kiikolojia. Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayokita mizizi yake katika misingi ya haki, amani, utu na heshima ya binadamu kwa sababu mazingira bora ni sehemu muhimu sana ya vinasaba vya maisha ya binadamu. Baba Mtakatifu ana matumaini makubwa kwamba, wanasiasa, wachumi na watunga sera, wataweza kujizatiti vyema zaidi, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa kazi kama utimilifu wa mtu binafsi, kijamii na kiikolojia. Katika ulimwengu mamboleo kuna haja ya kutengeneza na kulinda fursa za ajira kwa kuzingatia matumizi bora ya ardhi mintarafu mapokeo, rasilimali muda na teknolojia rafiki. Bila fursa za ajira, familia na jamii katika ujumla wake, haitaweza kusonga mbele hata kidogo. Baba Mtakatifu pamoja na mambo mengine watakayotekeleza wakati huu wa likizo anawataka zaidi kuendeleza utamaduni, ari na moyo wa sala katika maisha yao. Wawe tayari kumwiga Kristo Yesu katika ujana wake, ulioshuhudia mwanga angavu, amani na maridhiano kati ya watu. Likizo kiwe ni kipindi cha kupyaisha na kunogesha maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili!
Likizo ni muda muafaka ya kujenga, kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano ya dhati na Mwenyezi Mungu, kwa kusoma na kutafakari Maandiko Matakatifu, tayari kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha. Lakini zaidi kwa kuongozwa na Amri Kumi za Mungu bila shuruti! Mfano wa Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani na mapendo ulete hamasa katika kumfuasa Kristo Yesu. Ni nafasi ya kutafakari kuhusu maisha, ili kubainisha ikiwa kama maisha yao yana alama ya uwepo wa Mungu, ambaye kamwe hachoki kuwaongoza katika mapito ya maisha. Ni kipindi cha kukuza, kujenga na kudumisha urafiki; umoja na mafungamano ya kifamilia, ili kutangaza na kushuhudia kwamba, kwa hakika familia ni Kanisa dogo la nyumbani, linalojengwa na kuimarishwa na wanandoa wenyewe, katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku kwa kutambua kwamba, Kristo Bwana, yuko daima pamoja nao! Huu ni muda muafaka wa kufanya mazoezi na kumwilisha Injili ya huruma, upendo na msamaha katika maisha na vipaumbele vyao, tayari kumfuasa Kristo Yesu bila woga! Waamini wajifunze kutoka kwa Bikira Maria, kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya huduma kwa watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia.
Likizo ni muda muafaka wa kukaa pamoja na wanafamilia wote pale inapowezekana, ili kukazia malezi bora na utu wema. Ni wakati wa kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kusikilizana, kuheshimiana na kuthaminiana. Likizo ni muda wa kuratibu vyema rasilimali muda kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia nzima. Umefika wakati kwa wanandoa kuangaliana usoni bila kupepesa pepesa macho ili kujenga na kuimarisha upendo na urafiki wao wa dhati, daima wakimwachia nafasi Kristo Yesu ili aweze kuwafunda na kuwapyaisha katika maisha yao ya ndoa na familia. Mazoezi haya ya kiroho na kimwili yasaidie kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu. Ni muda wa uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Likizo si wakati wa kumweka Mwenyezi Mungu pembezoni mwa vipaumbele vya maisha ya mwanadamu kwani hii, ni hatari kubwa sana ya kuweza kumtokomea na hatimaye, kumezwa na malimwengu na huko kuna kilio na kusaga meno!