Tafuta

Mkutano wa Urafiki kati ya Watu Nchini Italia huko Rimini Kuanzia tarehe 20-25 Agosti 2022 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Shauku kwa mwanadamu.” Mkutano wa Urafiki kati ya Watu Nchini Italia huko Rimini Kuanzia tarehe 20-25 Agosti 2022 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Shauku kwa mwanadamu.” 

Papa Francisko Ujumbe Mkutano wa 43 wa Urafiki Wa Watu Nchini Italia Agosti 2022: Mwanadamu

Upendo, huruma, utu, ukarimu, heshima na haki msingi za binadamu ni kielelezo cha Msamaria Mwema, tunu msingi katika ujenzi wa urafiki wa kijamii. Vita, kinzani na mipasuko inaendelea kusababisha majanga makubwa katika maisha ya mwanadamu. Urafiki wa kijamii ujenge na kudumisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Upendo, huruma, utu, ukarimu, heshima na haki msingi za binadamu ni kielelezo cha Msamaria Mwema, tunu msingi katika mchakato wa ujenzi wa urafiki wa kijamii miongoni mwa watu wa Mataifa. Vita, kinzani na mipasuko inaendelea kusababisha majanga makubwa katika maisha ya mwanadamu. Urafiki wa kijamii ujenge na kudumisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mkutano wa Urafiki kati ya Watu Nchini Italia huko Rimini: “Meeting per l’amicizia fra i popoli” unaofanyika kila mwaka sasa umeingia katika awamu yake 43 kuanzia tarehe 20-25 Agosti 2022 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Shauku kwa mwanadamu.” Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, katibu mkuu wa Vatican na kutumwa kwa Askofu Francesco Lambiasi wa Jimbo Katoliki la Rimini, nchini Italia anawatakia heri, baraka na mafanikio mema. Maadhimisho haya ni sehemu ya Kumbukizi la Miaka 100 tangu alipozaliwa Mtumishi wa Mungu Padre Luigi Giussani tarehe 15 Oktoba 1922 huko Desio, Italia. Alifariki dunia tarehe 22 Februari 2005 huko Milano, Italia.

Mkutano wa Rimini 20-25 Agosti: Shauku kwa Mwanadamu
Mkutano wa Rimini 20-25 Agosti: Shauku kwa Mwanadamu

Mtumishi wa Mungu Padre Luigi Giussani ni kiongozi aliyebahatika kuwa na karama, maono na tafakari ya kina kuhusu Ukristo na mchango wake katika ustawi, mafao na maendeleo ya binadamu: kiroho na kimwili. Alikazia kwamba, Ukristo si dini inayojikita tu katika muundo wa mafundisho sadikifu, kanuni maadili, bali ni sehemu ya mchakato wa kutaka kukutana na Yesu Kristo katika hija ya maisha ya mwanadamu, ili kumtolea ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kama alivyofanya Mtumishi wa Mungu Luigi Giussani. Ukristo unamwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu, ili kuwaonjesha ile furaha, mapendo, huruma na imani inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ushuhuda wenye mvuto unashinda yote, kwani hapa mwamini anaalikwa kwa namna ya pekee kabisa kumwangalia Yesu Kristo Mkombozi wa dunia, ili kuweza kuwashirikisha na kuwamegea wengine ile furaha ya Injili. Ni changamoto inayowasukuma, waamini kutoka katika ubinafsi wao ili kuwaendea maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, tayari kuwashirikisha: amana na utajiri ambao wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kanisa. Huruma ya Mungu inapaswa kuwa ni chachu ya mageuzi, toba na wongofu wa ndani katika maisha na utume wa Kanisa; sanjari na kuenzi mahusiano kati ya watu binafsi na jamii ya watu katika ujumla wake.

Kauli MBiu Shauku kwa Binadamu
Kauli MBiu Shauku kwa Binadamu

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, kuna watu bado wanataliwa kwa kiasi kikubwa na uchu wa mali na madaraka, kiasi kwamba, fedha imegeuzwa kuwa ni kipimo cha utu na ufanisi wa maendeleo fungamani ya mwanadamu na kusahau kwamba, fedha inapaswa kuwa ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu na wala si kumgeuza mwanadamu kuwa ni mtumwa wa fedha, matokeo yake ni utu na heshima ya binadamu kuwekwa rehani! Kristo Yesu ni mfano na kielelezo cha Msamaria mwema, ambaye amewafunulia binadamu wote huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka, mwaliko kwa waamini kuguswa na mahangaiko ya jirani zao, kwa kuonesha huruma na uwepo wao, kama kielelezo cha imani tendaji. Watu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kukombolewa na Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kumbe, hakuna mtu anayetengwa na upendo wa Kristo Yesu, changamoto ya kusimama kidete kulinda: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Vita na mipasuko mbalimbali ni mambo yanayoendelea kusababisha kinzani na utengano kati ya binadamu. Kumbe, kuna haja ya kujenga na kudumisha mshikamano na udugu wa kibinadamu, ili kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, kwa kusimama kidete kutafuta na kulinda: ustawi, maendeleo na mafao yao; kwa kuwapenda na kuwaheshimu na kuwathamini maskini. Rej. Evangelii gaudium, 199.

Umuhimu wa ushuhuda unaomwilishwa katika matendo adili
Umuhimu wa ushuhuda unaomwilishwa katika matendo adili

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa kusema, mfano wa Msamaria mwema uwe daraja la kuwaunganisha watu na kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu unaojali utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu anawataka waamini kujenga urafiki wa kijamii unaosimikwa katika ushuhuda wa Jumuiya inayoinjilisha kwa njia ya matendo yanayokumbatia maisha ya mwanadamu, yakigusa Mwili wa Kristo anayeteseka, ili kupyaisha matumaini yao. Fumbo la Umwilisho ni kielelezo makini cha huruma, upendo na mshikamano wa Mungu na binadamu. Waamini washikamane na watu wenye mapenzi mema kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, sanjari na kushirikiana na Kanisa la Kiulimwengu katika mchakato wa ujenzi wa urafiki wa kibinadamu na hivyo kupanua shauku ya binadamu sehemu mbalimbali za dunia.

Papa Rimini 2022
20 August 2022, 14:52