Tafuta

Mchakato huu wa uinjilishaji unapaswa kusimikwa katika ushuhuda, yaani maneno na matendo yamwilishwe katika uhalisia wa maisha ya watu, ili kuunda ushirika unaomfanya Kristo Yesu. Mchakato huu wa uinjilishaji unapaswa kusimikwa katika ushuhuda, yaani maneno na matendo yamwilishwe katika uhalisia wa maisha ya watu, ili kuunda ushirika unaomfanya Kristo Yesu. 

Papa Francisko: Uinjilishaji Katika Ulimwengu wa Kidigitali: Huruma!

Papa Francisko anasema, hii ni changamoto kwa Mama Kanisa kusoma alama za nyakati na kuwa tayari kutafuta njia mpya za kutangaza na kushuhudia kiini cha Injili, yaani huruma na upendo wa Mungu. Huu ndio ubunifu wa shughuli za kichungaji, wenye uwezo wa kuwafikia watu wanakoishi, ili waweze kupata fursa ya kusikiliza, kuona na kushiriki katika mchakato huu wa Uinjilishaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro anajitahidi kuwashawishi watu kutilia maanani na kuweka katika utendaji ujumbe wa Injili ya huruma, upole na upendo wa Mungu kwa watu wote. Upole unaweza kuwa kipengele msingi cha ujumbe wa Injili na mrefeji wa mawasiliano hai miongoni mwa watu wa Mataifa. Katika ulimwengu wa kidigitali, Baba Mtakatifu anawaalika watu wote, wabatizwa kwa namna ya pekee kuwa; wajenzi wa madaraja ili kuwaunganisha watu na kuwatia matumaini katika utamaduni huu mpya. Anawataka kuwa ni Manabii ili kuhubiri ukweli, kufichua na kulaani udhalimu; Wawe wamisionari ili kubeba huruma na furaha ya Injili, tayari kuwaendea watu popote pale walipo. Anawaalika kuwa ni wachungaji wema ili kuwatafuta kondoo waliopotea, wenye huzuni, waliokata tamaa, wakavunjika na kupondeka moyo, ili waweze kuwarudisha tena zizini. Kwa namna ya pekee anawahimiza vijana wa kizazi kipya kuwa ni wasamaria wema, watakatifu na wanyenyekvu ili Kuganga, kupangusa na kuponya madonda ya walioumizwa na madhalimu. Anasema Baba Mtakatifu, katika zama za kidigitali watu wa Mungu wanahitaji mapinduzi ya: upendo, huruma, upole na unyenyekevu.

Uinjilishaji katika ulimwengu wa kidigitali usimikwe katika ushuhuda wa imani
Uinjilishaji katika ulimwengu wa kidigitali usimikwe katika ushuhuda wa imani

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video, kwa wajumbe wa mkutano wa Wainjilishaji wa Kidigitali Kimataifa, “Hechos 29” huko Monerrey, Mexico, anawapongeza katika hatua hii muhimu ya utume katika mazingira ya ulimwengu wa kidigitali. Mkutano huu, uwasaidie kujisikia kuwa ni wanajumuiya, sehemu muhimu sana ya utume na maisha ya Kanisa na kwamba, Mama Kanisa daima yuko tayari kutoka na kuwaendea watu kwa mwelekeo na upeo mpana zaidi; kwa ubinifu na ujasiri mkubwa, ili kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa watu wa Mataifa. Hii ni changamoto kwa Mama Kanisa kusoma alama za nyakati na kuwa tayari kutafuta njia mpya za kutangaza na kushuhudia kiini cha Injili, yaani huruma na upendo wa Mungu. Huu ndio ubunifu wa shughuli za kichungaji, wenye uwezo wa kuwafikia watu wanakoishi, ili waweze kupata fursa ya kusikiliza, kuona na kushiriki katika mchakato huu wa Uinjilishaji. Baba Mtakatifu anawataka wainjilishaji kupiga moyo konde na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu na kamwe wasiogope kuteleza na kuanguka. Baba Mtakatifu anaonesha upendeleo wa pekee kwa Kanisa ambalo limejeruhiwa, lakini linathubutu kutoka ili kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu.

Uinjilishaji mpya unasimikwa katika ushuhuda wa imani katika matendo.
Uinjilishaji mpya unasimikwa katika ushuhuda wa imani katika matendo.

Hii ndiyo dhamana inayotekelezeka kwa njia ya uinjilishaji unaotekelezwa katika ulimwengu wa kidigitali ambao kimsingi unapaswa kusimikwa katika ubinadamu. Wamisionari wainjilishaji katika ulimwengu wa kidigitali wajitahidi kuwa ni Wasamaria wema, ili kuwainjilisha watu hawa wapate kumfahamu Mungu, waonje tumaini la Kristo Yesu kwa kuwashirikisha sababu msingi ya tumaini linalobubujika kutoka katika undani wa maisha yao. Mchakato huu wa uinjilishaji unapaswa kusimikwa katika ushuhuda, yaani maneno na matendo yamwilishwe katika uhalisia wa maisha ya watu, ili kuunda ushirika unaomfanya Kristo Yesu aweze kutambulikana katika tamaduni za watu mbalimbali. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewapatia wamisionari hawa katika ulimwengu wa kidigitali baraka zake za kitume.

Ulimwengu Kidigitali

 

 

 

07 August 2022, 15:41